Wako Ndugu Kumi Wa Kike Na Wa Kiume Kwa Mama Mbali Mbali- Vipi Igaiwe Mirathi Ya Baba Yao?

SWALI:

 

kwa jina la Allaah,mwingi wa Ruhuma, Mrahiim

 

Assalaam alaikum wa Rahma tu Llahi wa Barakatuh

 

Tafadhali, nataka kujua ikiwa mtoto wa kike amefiliwa na babake na babake amewacha mali mengi na wao wako ndugu kumi; ndugu wa kiume ni wa nne na wa kike ni sita,lakini mama ni mbali mbali. Sasa ugawanyo wa urathi huu ni vipi kwa sheria ya kiIslam? Maanake hao ndugu wa kiume wa mama mwengine wameshike mali na hawataki kunigaiya pande langu la urathi kiIslam. Sasa mimi yataka ni fanye nini kwa kisheria ya kiIslam?

 

Ahsateni sana kwa msaada wenu na Allah awabarik.Aamiin.Amani ziwe juu yenu na ruhuma za Allaah na Barakah-Mimi ndugu wenu wa kiIslam


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu Miyraath ya watoto waliofiliwa na baba.

 

 

Hakika ni kuwa swali hili halijakamilika kwani hujatutajia warithi wengine wa aliyefariki. Je, aliyefariki aliacha mzazi au wazazi na je, aliacha mke au wake? Kwa njia yoyote ile ni lazima nao kama wapo warithi kisheria kwani Uislamu unampatia haki kila mmoja – mwanamme au mwanamke. Nawe unastahiki haki yako vilevile ya hiyo Miyraath.

 

Tutajaribu kuangazia hayo ili tuweze kukusaidia kwa njia iliyo nzuri. Ikiwa baba yako ameacha mke au wake ilhali wazazi wameaga dunia, mgao utakuwa kama ufuatavyo:

 

1.     Mke au wake atapata au watapata thumuni (1/8).

2.     Baki ya wirathi (7/8) itagaiwa watoto wa aliyefariki, mwanamme akipata sehemu mbili ilhali mwanamke sehemu moja. Kwa njia hiyo, wewe ambaye ni mwanamke utapata 1/16 au 6.25%.

 

Ikiwa wazazi wote wa aliyefariki wapo hai, mgao utakuwa:

 

  1. Wazazi wawili kila mmoja atapata sudusi (1/6).
  2. Mke au wake atapata au watapata thumuni (1/8).
  3. Baki ya wirathi kwa watoto (13/24), hivyo wewe utapata 13/336 au 3.87%.

 

Ikiwa mzazi aliyebaki ni mmoja, mgao utakuwa kama ufuatao:

 

  1. Mzazi atapata sudusi (1/6).
  2. Mke au wake atapata au watapata thumuni (1/8).
  3. Baki ya wirathi kwa watoto (17/24), hivyo wewe utapata 17/336 au 5.06%.

 

Ikiwa mpaka sasa hujapata haki yako inabidi uende katika ofisi ya Qaadhi kama wapo unapoishi au kwa Shaykh mwenye kushughulikia mambo ya Waislamu ili upate haki yako.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share