Hadiyth Kuhusu Wepesi Katika Dini: Ufafanuzi Wake

SWALI:

 

 

Nimesoma katika page ya madrasa hii hadithi lakini sijailewa ina maana

Imepokewa kutoka kwa Ibn Masoud (ر) kuwa Mtume (ص) amesema, “Wameangamia na kupotoka wenye kuweka mikazo zaidi katika ibada zao”. Na alisema hayo mara tatu. (Muslim)


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu  (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah,  (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu maana ya Hadiyth hiyo iliyo juu ambayo ni sahihi kabisa.

Hakika ni kuwa Uislamu ni Dini yenye msingi wa katikati, bila kuvuka mipaka katika aina zote za ‘Ibaadah. Kwa ajili hiyo, Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na vivyo hivyo Tumekufanyeni umati bora wa katikati” (2: 143).

 

Allaah Aliyetukuka Anasema yafuatayo kuhusu kula na kunywa:

Na kuleni na kunyweni, lakini msipite kiasi” (7: 31).

 

Na kuhusu matumizi Anasema:

Na wale ambao wanapotumia, hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo” (25: 67).

 

Ama kuhusu Hadiyth hiyo ina maana ya kuwa Muislamu hafai kuweka mkazo na kupita kiasi kinachohitajika katika ‘Ibaadah. Hiyo ni kwa maslahi yako mwenyewe kwani amri inatoka kutoka kwa Allaah Aliyetukuka, Muumba wa walimwengu. Ili kueleweka ni kuwa tuchukue mfano wa Muislamu anayeswali usiku mzima bila mapumziko. Jambo hilo litampelekea yeye kutoweza kufanya ‘Ibaadah nyingine ambazo pia Ameamrishwa na Mola Mlezi. Itabidi alale asubuhi na mchana, hivyo kumpelekea kutoweza kufanya kazi ambayo pia ni ‘Ibaadah kwa Muislamu. Ndio kwa ajili hiyo, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza wale Maswahaba watatu walioweka nia ya mmoja wao kutooa, mwingine kufunga kila siku na wa mwisho kutolala usiku kucha kwa ajili ya ‘Ibaadah.

 

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza kufanya hivyo kwa kuwaambia kuwa yeye ni mbora kuliko wao lakini pamoja na hayo anaswali na kulala, anafunga na kula na ameoa wake. Akamalizia kwa kusema:

 

Yeyote mwenye kukengeuka na Sunnah zake si katika yeye” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Hadiyth nyingine inayoelezea hiyo iliyo juu ni ile nasaha ya Salmaan al-Faarisiy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa nduguye Abu Dardaa’ (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipotaka kuswali Swalah ya usiku mapema alimuashiria alale. Baadaye asubuhi alimwambia:

 

Allaah Ana haki juu yako, nafsi yako ina haki juu yako na mke wako ana haki juu yako. Kila mmoja mpe haki yake” (al-Bukhaariy).

 

Ni kwa ajili ya hiyo ndiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

Amali inayopendwa na Allaah ni ile yenye kudumu japokuwa ni kidogo”. Kwa minajili hiyo ndio, ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhuma) akajuta sana alipokuwa mzee kwa kuwa alikuwa amejiwekea kuswali usiku muda mrefu, kufunga siku nyingi na kumaliza kusoma Qur-aan kwa siku saba baada ya kuwa alinasihiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asifanye hivyo kwani huenda akaishi miaka mingi naye akashindwa kufuatilia hayo. Kweli alipata umri mkubwa na akajuta sana kwani ‘amali hizo zikawa ngumu sana kwake (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Kwa muhtasari ni kuwa inatakiwa Muislamu afanye ‘Ibaadah kwa kiasi anachoweza asipindukie mpaka mwishowe akashindwa kuzitekeleza.

 

Lakini vilevile ieleweke kuwa hiyo haina maana mtu aache kutekeleza faradhi zake na Sunnah zilizokokotezwa na zote zilizothibiti kwa kuchukulia kigezo cha Hadiyth hiyo kwani hayo si katika mafhumu ya Hadiyth ilivyo. Mafhumu ya Hadiyth ni kama inavyofahamisha hiyo mifano ya matukio ya hao Maswahaba watatu waliokuwa hawataki kuoa, kulala au kula kwa kukithirisha ‘Ibaadah kuliko inavyotakikana. Maana kuna watu wakishafanya ya faradhi basi ya Sunnah hawayataki na wanatoa dalili ya Hadiyth hiyo kuwa dini usiikaze sana utashindwa!

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share