003-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Upendo Unamaanisha Nini Katika Maisha Ya Ndoa

 

UPENDO NI FUNGUO ZA NYOYO

 

UPENDO UNAMAANISHA NINI KATIKA MAISHA YA NDOA?!!

 

Kwa hakika maisha haya ni:

1- Ikhlaas

2- Upaji

3- Kumpendelea mwenzako

 

Kwa hakika ni kutanguliza haki ya mume kuliko haki yako, ni kujiteremsha ni kujishusha na kiburi chako katikati ya mivutano ili upendo na kufahamiana yachukue nafasi ya ugomvi na mijadala (msuguano).

 

Swahaba Mtukufu Abu Dardaa (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimwambia mke wake maneno yafuatayo:

 

Samehe, utadumisha mapenzi yangu,

                              Wala usizungumze kwa kunibishia ninapo ghadhibika.

 

Wala usinigonge kama mgongo wa dufu hata mara moja,

                                                     Kwani wewe hujui vipi itakavyokuwa.

 

Wala usizidishe malalamiko yakapotea kwa nguvu,

                           Na moyo wangu ukaanza kukukataa na nyoyo hugeuka.

 

Mimi nimeona upendo na maudhi,

                                       Vinapokutana basi mapenzi hayakai huondoka.

 

 

Fahamu ewe dada Muumini kuwa mume wako hatokupenda hadi ahisi kuwa nawe unampenda, mapenzi ni hisia za pande mbili na kubadilishana, siku zote mtu huelekea katika kumpenda mtu kwa kadiri mtu yule atakapoonesha anampenda na kumjali. Maamkizi yenye uchangamfu, kubadilishana zawadi, kuitana kwa majina mazuri na kutabasamu, yote haya hufungua kwa mke upeo mpana wa mapenzi ya kweli na furaha isiyo na kifani na hivyo kumfanya mume kuwa ni kipenzi kizuri zaidi kwa mke wake, kama ilivyo kwa mume kwa mke wake anatakiwa awe ndie kipenzi chake zaidi.

 

Kuna wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa na mtu mmoja anampenda nani zaidi? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu, kuwa ni Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

‘Amruu bin Al-‘Aasw amesema,

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam.) alinituma na Jeshi tukiwa pamoja na Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) niliporejea nilisema, “Ewe Mtume wa Allaah ni mtu gani unayempenda zaidi”?![1]

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu kwa kusema ni, ‘Aaishah, Nikasema: Nakusudia unayempenda kwa wanaume, akajibu, kuwa anampenda Baba yake ‘Aaishah[2]

 

Mapenzi ni mahusiano mazuri, furaha, mahaba, huruma, usamehevu na maghfira, na sio mapenzi kama wanavyosawirisha watu katika baadhi ya visa, wakatengeneza maigizo na kuchora picha (akilini mwao) za kijana kana kwamba ni Nabii katika Manabii au Malaika waliokurubishwa kwa Mwenyezi Mungu kiasi cha kuwa mke atakapoona kwa mumewe kitu kinachomchukiza basi hudhani kuwa maisha ya ndoa yameshindikana na ndoto aliyokuwa nayo imeondoka.

 

Sivyo hivyo kabisa Ewe mke, kwani mifano hiyo haipatikani kabisa katika maisha.

 

Maisha haya ya duniani ni maisha halisi si ya kufikirika au kusadikika, bali ni maisha ambayo kila mtu ana aibu zake, inamtosha mtu kujifakharisha kwa kuhesabika aibu zake.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Hambughudhi Muumini mwanamme kumbughudhi Muumini mwanamke kwa tabia yake, kwani akichukizwa na tabia moja ataridhishwa na tabia nyingine”[3]

 

Kadhalika nawe mke utakaposikitishwa na tabia mojawapo ya mume wako basi utaridhika na tabia zake zingine, kumbuka maneno ya Al-Hakiym aliposema,

“Mke anasemaje kuhusu mumewe ambae ameacha wanawake wote na akamchagua yeye tu? Na mwanamke anamfanyia nini mume wake aliyewaacha wazazi wake, marafiki na jamaa zake na hakuridhia kumpata mwenye kumliwaza mwengine zaidi yake”

 

Wewe ndie liwazo la mume wako, mwenza wa mpenzi wako, uzuri ulioje wa ibara ya Qur-aan inayosema,

“…Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao…. (2:187)

 

Katika Aayah nyingine kadhalika,

Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri. (30:21)

 [1]‘Amruu bin Al-‘Aasw wakati huo alikuwa bado mgeni katika Uislam, na akadhani maadamu amepewa uongozi wa jeshi basi yeye ni bora kuliko Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) siku moja ‘Amruu alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mtu anayempenda, Mtume Akamjibu kuwa ni Abu Bakr, ‘Umar, ‘Aliy na ‘Uthmaan. ‘Amruu akatamani asingeuliza swali lile.

[2] Al-Bukhaariy na Muslim

[3] Imepokewa na Muslim

Share