004-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Miongoni Mwa Mapenzi, Ni Wewe Kufurahi Kwa Furaha Yake Na Kuhuzunika Kwa Huzuni Yake

 

MIONGONI MWA MAPENZI NI WEWE KUFURAHI KWA FURAHA YAKE NA KUHUZUNIKA KWA HUZUNI YAKE

 

Kwa hakika jambo kubwa alichukialo mwanamme ni kumuona mke wake akifurahi wakati yeye yupo katika huzuni, au wakati yeye akiwa katika huzuni basi mke wake anakuwa katika furaha. Mambo kama haya yanakuwa ndio sababu ya mume kumchukia na kumtenga mke wake, huenda jambo kama hili likapelekea katika mambo makubwa zaidi hakuna ajuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). 

 

Mwenyezi Mungu Amrehemu mwanamke ambaye kwa kumuangalia tu mume wake na kujua hali yake aliyokuwa nayo basi hujaribu kuwa katika hali yake na akawa ni msaada wake, na jambo hilo la mumewe likawa kubwa katika nafsi yake ikiwa mume wake yupo katika hali ya furaha basi naye atatabasamu mbele ya mumewe na ikiwa ni kinyume chake basi naye huwa kama vile na kujaribu kupunguza kwa kumliwaza mumewe, kumuondolea matatizo, kumpa utulivu wa moyo wake. Hali hii inafanana na ile hali aliyokuwa nayo Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pindi alipojiwa na mume wake; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na habari ya Wahyi akiwa anatetemeka na kusema,

“Nifunike nifunike kisha akasema, Khadiyjah nina nini? Kisha akamuelezea habari za kule, kisha akasema, ‘Nilikuwa najihofia’. Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema, sivyo kabisa, hiyo ni bishara njema. Mwenyezi Mungu kamwe Hatokutupa, kwa hakika wewe unaunga udugu waliokukata, unasema maneno ya kweli, hauongopi hata mara moja, na unawakirimu wageni, na kumsaidia mtu kupata haki yake.”[1]

 

Je, Umeona ewe mke Muumini, majibu bora kuliko majibu haya? Kwa hakika Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) amestahiki pepo kwa kumliwaza kwake Mtume wa Mwenyezi Mungu na kumpunguzia matatizo yaliyokuwa yakimkabili. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Niliamrishwa kumpa bishara Khadiyjah kuwa atapata pepo ambayo nyumba yake na nguzo zake ni za lulu ziliyo wazi ndani yake, hamna kelele humo wala usumbufu”[2] 

 

Kwa tendo lile na matendo mengine ya Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilibidi Mtume ahifadhi wema wa Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) yake yote.

Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) anasema,

“Sikuwahi kumuonea wivu mwanamke yeyote kama nilivyokuwa namuonea wivu Khadiyjah kutokana na kutajwa sana kwa wema na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), siku moja nilimtaja kwa kusema, ‘Una nini kwa mwanamke yule mkongwe mtu mzima’? Si ya kuwa Mwenyezi Mungu Amekuruzuku kilichokuwa cha kheri zaidi?!” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “WAllaahi hakunibadilishia aliyekuwa mbora kuliko yeye, kwa hakika yeye ndiye aliyeniamini waliponikana watu, aliyenisadiki na kunikubali waliponikadhibisha, akaniliwaza kwa mali yake watu waliponinyima. Na kwa Khadiyjah Allaah Akaniruzuku watoto kinyume cha wanawake wengine.”[3]

 



[1] Al-Bukhaariyna Muslim

[2] Al-Bukhaariyna Muslim

[3] Al-Bukhaariy amepokea Hadiyth hii kwa ufupi na kadhalika wamepokea Hadiyth hii Ahmad na At-Twabaraaniy

Share