Anaweza Kushika Mimba Akifanya Maasi Ya Zinaa Bila Ya Jimai?

SWALI:

 

Assallamu allaykum nashukuru sana kwa kuweza kusaidiana sisi waislamu wenyewe mungu wazidishie, mie nilikuwa na swali nataka munisaidie kunijibu, nini maana ya zinaa, na pia nini maana ya romance tofauti yake nini, na swali langu jengine mwanamke anapata mimba mpaka afanye zinaa au akifanya romance anaweza kupata mimba. Inshallah mungu atujalie atuepushe na mambo mabaya ameen


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kufanya mapenzi na bila jimai.

 

Allaah Aliyetukuka Atuepushe na maasi ya zinaa na mengine yote.

 

Ama neno zinaa lina maana mbili kama ilivyotufahamisha sheria yetu ya Kiislamu. Nazo ni:

 

  1. Kukutana baina ya mwanamme na mwanamke katika kitendo cha jimai ambao hawakuona kisheria, na sehemu utupu wa mwanaume ukaingia katika utupu wa mwanamke.

  2. Kufanya matendo kwa viungo kwa njia ya matamanio hata bila ya jimai. Kwa mfano kutazama jinsia nyingine kwa matamanio, kutembea kwa ajili ya zinaa, kusikiliza, kushika asiyekuwa maharamu yako na kadhalika. Kwa hivyo, kwa mujibu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) macho, masikio, miguu, mikono, mdomo na kadhalika vinazini na sehemu za siri zinasadikisha. Kwa ajili hiyo ndio Allaah Aliyetukuka Akatukataza hata kuikaribia zinaa: “Wala msikaribie zinaa hakika hiyo zinaa ni uchafu mkubwa na njia mbaya kabisa” (Al-Israa: 32).

 

Ama maana ya Romance ni mapenzi ambayo mwanamme atafanya na mwanamke bila ya jimai yenyewe. Kwa mfano, kuzungumza maneno ya mapenzi, kushikana, kupigana busu na mfano wa hayo.

 

Kushika mimba kwa mwanamke si lazima watende tendo la jimai ikiwa ni kwa kuzini au kufanya kwa njia ya halali. Inayoleta mimba ni kuingia manii (mbegu za kiume) katika utupu wa mwanamke. Na ikiwa mwanamme atafanya romance na mwanamke na maji hayo kama yatapenya kwenye utupu wa mbele wa mwanamke basi mwanamke anaweza kupata mimba.

 

 

 Mwanamke wa Kiislamu anapaswa kujiepusha na maasi hayo ambayo ni desturi za makafiri zisizopasa kuigwa. Pia maasi hayo hatimaye yatampelekea kutumbukia katika zinaa na kushika mimba, kisha matokeo yake ni hasara kwake na kwa mtoto. Juu ya hiyo atabaki kuwa katika majuto ya milele, na itamletea taathira na madhara yeye mwenyewe, mtoto, jamaa zake na jamii nzima.  Vilevile maasi hayo adhabu yake ni kali mno endapo yatafanyika.

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awaepushe wanawake wasipate mimba nje ya ndoa wala jinsia hizo mbili zisikaribie zinaa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share