Anaswali Swalaah Zote Mpaka Tahajjud, Ila Swalaah Za Asubuhi Zinampita

SWALI:

 

Alhamdulilah namshukuru mola kwa kunipa afya na kidogo japo si sana elimu ya dini yetu, nasali na napanda sana mambo ya dua na kujisomea Qur'an kila mara. Ninasali alhamdulilah lakini tatizo langu ni sala ya subhi, yaani ni mtihani, kila njia najaribu nashindwa. Naomba msaada ila sala za tahajud na sunna za usiku naamka ila subhi labda mara 4 mpaka 5 kwa mwezi.

 

jazaka Allahu

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuswali Tahajjud lakini kukosa Swalah ya Subhi.

 

 

Uislamu na sheria zake zimeipatia kipaumbele ‘Ibaadah za fardhi mwanzo kabla ya za Sunnah. Ikiwa utakuwa unafanya ya Sunnah na kushindwa ya fardhi basi itakuwa hujafanya lolote. Inavyotakikana ni kutanguliza ya Fardhi kwanza kisha Sunnah, na ni bora zifuatane zote kwa pamoja; yaani Fardhi na Sunnah uzitekeleze sambamba. Isiwe unafanya pia ya Fardhi ukawa umeridhika kabisa na ukaacha ya Sunnah.

 

Hadiyth hii ifuatayo inatuonyesha umuhimu mkubwa sana wa Swalah za Fardhi:

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) anatuelezea kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi aalihi wa sallam) amesema: Imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alisema kwamba: Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema ((Kitu cha kwanza kinachohesabiwa katika ‘amali za mja wa Allaah siku ya Qiyaamah ni Swalah zake. Zikiwa zimetimia, hapo tena atakuwa kaneemeka na kafuzu, na zikiwa zina kasoro atakuwa kaanguka na kala khasara. Ikiwa pana upungufu katika Swalah zake za fardhi Allaah ‘Azza wa Jallaَ Atasema: Angalia ikiwa mja Wangu ana Swalah zozote za Sunnah ambazo zinaweza kufidia zile zilizopungua, hapo tena ‘amali yake iliyobaki itaangaliwa hivyo hivyo)) [At-Tirmidhiy, Abu Daawuud, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Ahmad]

Nasaha yetu ni kuwa ujitahidi sana kuswali Swalah ya Subhi mwanzo. Na hilo linaweza kufikiwa kwa kufuata moja katika ya haya mambo:

 

1.     Inuka kwa ajili ya Swalah ya Tahajjud nyakati zake za mwisho karibu sana na Subhi, ili ukimaliza Sunnah uswali Swalah ya Fardhi.

 

  1. Punguza kuinuka kuswali Swalah ya usiku ili upate nafasi ya kulala vya kutosha na kuinuka kwa ajili ya Subhi.

 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

 

 

Kutimiza Swalah Za Fardhi Kabla Za Sunnah

 

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupe hima na Akuwezeshe uswali Swalah zote – mwanzo za Fardhi na kisha ya Sunnah bila tatizo lolote.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share