Kuswali Ndani Ya Basi Akiwa Ameketi Karibu Yake Mwanamke Asiye Mahram Wake Inajuzu?

 

 

SWALI:

 

ASSALAAM ALLAEYKUM WARAHMATULLAH WABARAKAT,

Sheikh nashukuru sana kwa majibu yako mazuri kwa hakika nimepata faida kubwa ambayo sikua nayo kabla, kwakweli nimekuelewa vizuri sana ila kuna swali moja limenijia baada ya hayo maelezo sasa mfano nimekua nina udhu wangu vizuri kabla ya safari lakini kwa bahati mbaya katika siti nimekaa na mwanamke ambae hajajisitiri na wakati wa swala umenikuta katika basi ambalo halikusimama je? Inajuzu nikaswali nikiwa katika basi hali ya kua nipo na mwanamke siti moja mwanamke ambae hajajisitiri, hilo ndo swali langu la nyongeza nitashukuru sana sheikh ukinipa ufafanuzi.

 

Wahadha assalaam allaeykum warahmatullah wabarakatu

 

 


 

 

JIBU:

 

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuswali katika basi ilhali umekaa kiti kimoja na mwanamke asiye Mahram yako ilhali hajajisitiri vyema.

 

 

Ilivyo, ni kuwa Swalah ya fardhi mtu anatakiwa ajitahidi kuiswali amesimama, akishindwa kabisa basi kwa kukaa, na huko kuswali kwa kukaa ni nusu ya aliyesimama kwa daraja na fadhila. Hivyo, ni wajibu wako kufanya bidii kusimamisha basi ili uweze kuiswali Swalah yako vizuri. Kama ambavyo watu wanaweza kusimamishiwa basi kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo n.k. kadhalika nawe unaweza kusimamishiwa basi ukitaka au ukisisitiza.

 

Ama iiwa itashindikana kabisa baada yaw ewe kujaribu juhudi hizo, basi unaweza kuswali kwa kukaa, na ikiwa hakuna zaidi ya hapo ulipo karibu na mawanamke, basi unaweza kuswali katika hali hiyo na ujiingize katika khushui (unyenyekevu) wa Swalah yako bila kushawishika au kushughulishwa na huyo mwanamke. Bila shaka kuwa karibu na mwanamke kunaweza kukushawishi usiwe ni mwenye kunyenyekea katika Swalah.

 

Hiyo ni hali ya dharura na Swalah yako ni sahihi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share