Je, Unamshukuru Allaah ('Azza wa Jalla) Ipasavyo Kwa Neema Zake Nyingi Zisizohesabika?

Je, Unamshukuru Allaah ('Azza wa Jalla) Ipasavyo Kwa Neema Zake Nyingi Zisizohesabika?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

وَآتَاكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ ۚ وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ الْإِنسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ ﴿٣٤﴾

“Na Akakupeni kila mnachomuomba. Na mkihesabu neema za Allaah hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. Hakika insani ni mwingi wa dhulma, mwingi wa kukufuru akasoye shukurani.” [Ibraahiym: 34] 

 

 

Tukizingatia Kauli hizo za Allaah (‘Azza wa Jalla),  tutaona kwamba hakika hatuwezi kamwe kuhesabu neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   

 

Hebu angaza na fikiria neema zilizo katika ulimwengu, kuanzia ardhi jinsi Alivyoitandaza ikatulia, Akaweka ndani yake mito, milima, mimea, Akateremsha mvua ya kustawisha hiyo miti na mimea na bustani za kupendeza. Kisha angaza na zingatia jua linalotupatia mwanga na faida kadhaa,  na pia zingatia mwezi ambao unatuwezesha kujua idadi ya hesabu za miaka, miezi na siku,  na mwanga wa kusafiria. Kisha zingatia jinsi Allaah (‘Azza wa Jalla) Alivyotuumbia wanyama wa kunufaika nao kwa kila aina ya faida kutokana nao. Almuhimu hatuwezi kabisa     kuhesabu neema Alizozijaza katika huu ulimwengu.  

 

Vile vile hatuwezi kuhesabu neema ambazo Allaah (‘Azza wa Jalla) Amezijaalia katika nafsi zetu na miili yetu, ndipo Anapotuambia:

 

 

وَفِي أَنفُسِكُمْ ۚ أَفَلَا تُبْصِرُونَ﴿٢١﴾      

“Na katika nafsi zenu je hamuoni?” [Adh-Dhaariyaat: 21]

 

 

Anasema pia  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuhusu umbo letu:

 

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ﴿٤﴾

“Kwa yakini Tumemuumba mwana-Aadam katika umbile bora kabisa.” [At-Tiyn: 4]

 

Basi inatupasa tumshukuru Allaah (‘Azza wa Jalla)    kila mara kwa kadiri tunavyoweza, na kila tunapomshukuru Yeye Hutuzidishia hizo neema kama Anavyosema:

 

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ 

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (neema Zangu).” [Ibraahiym: 7]

 

Na Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Ghannaam (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) kwamba  Rasuli wa Allaah  (Swalla-Allaahu ‘('alayhis-salaam) wa aalihi wa sallam) amesema:

مَنْ قَالَها حين يصبح

 

Atakayesema anapoamka asubuhi:

 

اللّهُـمَّ ما أَصْبَـَحَ بي مِـنْ نِعْـمَةٍ أَو بِأَحَـدٍ مِـنْ خَلْـقِك، فَمِـنْكَ وَحْـدَكَ لا شريكَ لَـك، فَلَـكَ الْحَمْـدُ وَلَـكَ الشُّكْـر

Allaahumma maa aswbaha biy min ni’-matiy aw biahadim min Khalqika faminka Wahdaka laa shariyka Laka, falakal-Hamdu walakash-shukru

Ee Allaah, sikuamka na neema yoyote au kati ya kiumbe Chako chochote, na neema ila inatoka Kwako hali ya kuwa peke Yako Huna mshirika, ni Zako  Himdi na ni Zako shukurani.

Jioni useme:

 

اللّهُـمَّ ما أَمْسَى بِي مِـنْ نِعْـمَةٍ أَو بِأَحَـدٍ مِـنْ خَلْـقِك، فَمِـنْكَ وَحْـدَكَ لا شريكَ لَـك، فَلَـكَ الْحَمْـدُ وَلَـكَ الشُّكْـر

Allaahumma maa amsaa biy min ni’-matiy aw biahadim min khalqika faminka Wahdaka laa shariyka Laka, falakal-Hamdu walakash-shukru

 

فَقَدْ اَدَّى شُكر يَوْمِهِ وَمَنْ قَالَ مِثْل ذلِكَ حِينَ يُمْسي فَقَدْ أّدَّى شُكْر لَيْلَتِه

Basi atakuwa ametekeleza shukurani ya siku nzima, atakayesema jioni atatekeleza shukurani ya usiku mzima. [Abu Daawuwd (4/318) [5073], An-Nasaaiy katika ‘Amal Al-Yawm wal-Laylah [7]. Ibn As-Sunniy [41], Ibn Hibbaan “Mawaarid” [2361] na isnaad yake ameipa daraja ya Hasan Ibn Baaz (رحمه الله) katika Tuhfat Al-Akhyaar (Uk. 24)]

 

 

 

Na Hadiyth ya ibn 'Umar kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth ya Al-Qudsiyy:

 

 

إن عبدًا من عباد الله قال: يا رب، لك الحمد كما ينبغي لجلال وجهك وعظيم سلطانك، فعضلت بالملكين فلم يدريا كيف يكتبانها، فصعدا إلى السماء فقالا يا رب، إن عبدا قد قال مقالة لا ندري كيف نكتبها، قال الله  وهو أعلم بما قال عبده : ماذا قال عبدي؟ قالا يا رب إنه قد قال: يا رب لك الحمد كما ينبغي لجلال وجهك وعظيم سلطانك. فقال الله لهما: اكتباها كما قال عبدي حتى يلقاني فأجزيه بها -   إبن ماجه

Mja katika waja wa Allaah alisema: “Ee, Rabb wangu! Zako wewe tu Himdi  Unayestahiki kushukuriwa kama inavyopasa Ujalali wa Wajihi Wako na Utukufu wa Usultani Wako.”  Malaika wawili walibabaika hawakujua vipi waandike maneno hayo (jinsi alivyomtukuza utukufu wa Rabb wake) Wakaenda kwa Allaah wakasema: Ee Rb wetu! Hakika mja wako kasema aliyoyasema na wala hatujui vipi tuyaandike. Akasema Allaah   Kwani kasema nini mja wangu? (Na Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anajua aliyoyasema mja Wake bila ya Malaika kumwelezea) Wakasema amesema: “Ee, Rabb wangu! Zako wewe tu Himdi  Unayestahiki kushukuriwa kama inavyopasa Ujalali wa Wajihi Wako na Utukufu wa Usultani Wako.” Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Akasema: “Yaandikeni kama alivyosema mja Wangu mpaka atakaponikuta (siku ya malipo) basi nitampa jazaa yake kwa hayo (aliyoyasema).”  [Ibn Maajah 2:1249]

 
Adhkaar nyingi za kumshukuru Allaah (‘Azza wa Jalla) zimo katika mafunzo ya Qur-aan na Sunnah, hivyo basi tusiache daima kumshukuru Allaah (‘Azza wa Jalla), kwa kukiri kwanza moyoni neema Zake, kisha kutamka kwa ndimi zetu, na  kutumia neema Alizotujaalia Allaah (‘Azza wa Jalla) katika yanayomridhisha.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida nyenginezo:

 

Shukurani Kwa Allaah - Kisa Katika Hadiyth Kuhusu Mkoma, Kipara Na Kipofu

 

Share