Thuluthi Ya Mali Kumpa Mtoto Wa Adoption Na Mgao Wa Mali Nyingine

SWALI:  

Mtu katoa thuluthi ya mali yake kumpa mtoto wake wa “Adoption”. Vipi kugawa mali yaliobakia. Anaye mke, mama, ndugu wa kiume khalisa, ndugu wa kike wawili khalisa na ndugu wanaume wawili si khalisa kwa mama tu. Na wako watoto wa kiume wawili wa aliyefariki ndugu yake kwa baba tu si khalisa. Please tujibuni.

 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Swali zuri sana kutoka kwa ndugu yetu. Na mas’ala ya mirathi ni mas’ala magumu na ilimu ambayo imepotea kwa Waislamu. Ni jambo muhimu sana mwanzo kueleza kwamba uislamu haukubali mas’ala ya adoption (mtoto wa kupanga) kwa aya ambayo ipo wazi kabisa. Allaah Anasema:

 

ادْعُوهُمْ لِآبَائِهِمْ هُوَ أَقْسَطُ عِندَ اللَّهِ فَإِن لَّمْ تَعْلَمُوا آبَاءهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ وَمَوَالِيكُمْ وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

“Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Allaah. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu” (33:5).

Hii aya iliteremka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa na mtoto wa kupanga mpaka jina lake likawa ni Zayd bin Muhammad badala ya Zayd bin al-Haarithah (Radhiya Allaahu 'anhu). Allaah Alimkataza kufanya hivyo na jina la Zayd likarudi kama awali kuitwa kwa jina la babake.

Uislamu unahimiza sana kuwalea na kuwatizama watoto wa masikini na hasa mayatima na kuna ujira mkubwa sana katika kufanya hivyo. Lakini inatakiwa majina ya wazazi wake yabakie vile vile yasiwe yatabadilika kwa kutumia jina lako kama mama au baba mzazi.

Na kwa hawa watu ambao hawana wirathi basi mtu anaweza kuusia apatiwe thuluthi ya mali yake na thuluthi pia ni nyingi. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema ya kwamba kabla ya kugawanywa kwa mirathi ni lazima litolewe lile fungu alilousia:

 

مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا

 “Haya ni baada ya kutolewa alicho usia…” (4: 11).

 

Haya ni kwa mujibu wa Hadithi ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Imepokewa na Abi Ishaaq Sa‘d bin Abi Waqqaas Maalik bin Uhayb bin ‘Abdi-Manaaf bin Zuhrah bin Kilaab bin Murrah bin Ka‘b bin Lu’ay al-Qurashiy az-Zuhriy (Radhiya Allaahu 'anhu), mmoja wa wale Masahaba kumi waliobashiriwa Pepo (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kwamba: “Alikuja kunizuru mimi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwaka ule wa Hijjatul Wida ambapo nilikuwa mgonjwa sana”. Nikamwambia: “Ee Mjumbe wa Allaah! Umenifikia mimi ugonjwa huu kama unavyoniona na mimi ni tajiri na hakuna anayenirithi isipokuwa binti yangu mmoja. Je, naweza kutoa sadaka kwa thuluthi mbili ya mali yangu?” Akasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Hapana”. Nikasema: “Kwa nusu ya mali yangu, ewe Mjumbe wa Allaah?” Akasema: “La (Hapana)”. Nikasema: “Thuluthi, ewe Mjumbe wa Allaah?” Akasema: “Thuluthi ni sawa, japokuwa thuluthi pia ni nyingi. Ni bora uwaache warithi wako wakiwa matajiri kuliko kuwaacha huku wanawaomba watu wengine ili kutekeleza haja zao. Jua kwamba chochote unachotumia kwa kutaka radhi za Allaah isipokuwa unapata thawabu, hata kumlisha chakula mkeo”. Nikasema: “Ee Mjumbe wa Allaah! Je, nitaachwa nyuma baada ya Masahaba kuondoka?” Akasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Kwa hakika hutaachwa nyuma. Chochote utakachofanya kutaka radhi za Allaah, itanyanyua cheo chako katika jamii. Nina hakika ya kwamba utaishi sana mpaka watu wafaidike (Waislamu) kutoka kwako na wengine wadhurike (wasiokuwa Waisalmu)”. Baadae Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaomba: “Ewe Mola wangu! Ikamilishe Hijrah ya masahaba zangu na wala usiirudishe nyuma ya migongo yao”. Lakini yule wakuonewa huruma ni Sa‘d bin Khawlah ambaye aliachwa nyuma na akaaga dunia Makkah na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea apewe rehema na huruma na Allaah” (al-Bukhari na Muslim, pia tazama Riyadhus Salihiin, Hadithi nambari 6).

 

Mawarithi hawana ruhusa ya kurithi mpaka zilipwe:

 1. Deni zote anazodaiwa maiti: Deni ni haki ya mwanadamu na ni muhimu alipiwe deni hilo kwani Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa haswalii maiti mpaka ajue kama ana deni au la. Ikiwa hana deni vyema ikiwa ana deni ni lazima mtu achukue jukumu hilo kabla ya kumswali. Na Allaah Anasema:

 

... أَوْ دَيْنٍ ...

“...Au kulipa deni...” (4: 11)

 

 1. Zitolewe nyasia alizousia: Hii tumeilezea hapo juu.

 

 • Wasiwe warithi wepesi kupapia mali ya kurithi. Sharti haya yatolewe kwanza. Wasiya pia haufai kuwa ni wa kuwadhuru hao mawarithi wake, na mtu hana ruhusa kuusia zaidi ya thuluthi. Baada ya kutoa madeni, wasiya, gharama za mazishi, kile kitakachobaki kitagawanya kwa mawarithi, nao ni:

 

 • Akifa mtu akamwacha mama tu na nduguze – wakiwa makhalisa au wa kuumeni au wa kukeni, wanaume au wanawake au mchanganyiko – mama atachukua sudusi ya mali. Haya ni kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

... فَإِن لَّمْ يَكُن لَّهُ وَلَدٌ وَوَرِثَهُ أَبَوَاهُ فَلأُمِّهِ الثُّلُثُ فَإِن كَانَ لَهُ إِخْوَةٌ فَلأُمِّهِ السُّدُسُ...

“Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi” (4: 11).

 

 • Akifa mume akamwacha mke bila bila kuacha mtoto wala mjukuu, basi mke atapata robo ya mali ya mume, kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka:

 

 

.... وَلَهُنَّ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْتُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّكُمْ وَلَدٌ فَإِن كَانَ لَكُمْ وَلَدٌ فَلَهُنَّ الثُّمُنُ مِمَّا تَرَكْتُم مِّن بَعْدِ وَصِيَّةٍ تُوصُونَ بِهَا أَوْ دَيْنٍ ...  

 

Na wake zenu watapata robo mlichokiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha, baada ya wasia mlio usia au kulipa deni” (4: 12)

 

 Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

فَإِن كَانَتَا اثْنَتَيْنِ فَلَهُمَا الثُّلُثَانِ مِمَّا تَرَكَ وَإِن كَانُواْ إِخْوَةً رِّجَالاً وَنِسَاء فَلِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الأُنثَيَيْنِ يُبَيِّنُ اللّهُ لَكُمْ أَن تَضِلُّواْ وَاللّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

 

 “Na ikiwa wao ni ndugu wa kike wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho acha maiti. Na wakiwa ndugu wanaume na wanawake, basi mwanamume atapata sehemu iliyo sawa na ya wanawake wawili. Mwenyezi Mungu anakubainishieni ili msipotee; na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu” (4: 176).

 

Hapa Allaah Anatuelezea warithi wa ndugu wa kwa baba au wale ambao ni khalisa. Hivyo ni kutueleza kuwa ikiwa wenye kurithi ni ukhti wawili au zaidi, watapata thuluthi mbili. Na ikiwa wenye kurithi ni ndugu wa kiume na wa kike kwa baba tu au khalisa, basi kila mwanamme atapata mafungu ya wanawake wawili. Na katika suali wapo madada wawili na kaka mmoja khalisa, hivyo wao watapata thuluthi mbili (2/3). Lakini hawa wanaingia katika fungu la asaba ambao ima hupata kingi au kidogo au mara nyengine hawapati kabisa. Na wao ni wale ambao huchukua kinachobaki katika mirathi.

 

 • Na ndugu wa kwa mama wanaume au wanawake au mchanganyiko nao pia wanapata wirathi wao kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka:

وَإِن كَانَ رَجُلٌ يُورَثُ كَلاَلَةً أَو امْرَأَةٌ وَلَهُ أَخٌ أَوْ أُخْتٌ فَلِكُلِّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا السُّدُسُ فَإِن كَانُوَاْ أَكْثَرَ

 مِن ذَلِكَ فَهُمْ شُرَكَاء فِي الثُّلُثِ

 

“Na ikiwa mtu mwanamume au mwanamke anayerithiwa ni mkiwa (naye hana mtoto wala wazazi), lakini anaye ndugu mume au ndugu mke (wa kwa mama), basi kila mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi watashirikiana katika thuluthi” (4: 12).

 

Hivyo kwa mujibu wa Swali wale ambao watapata wirathi ni wafuatao:

 

 • Mama - Sudusi (1/6).
 • Mke - Robo (1/4).
 • Ndugu wa kwa Mama - Thuluthi (1/3).
 • Ndugu Khalisa (Kilichobaki)       - Robo (1/4).
 • (Ndugu wa kiume hupata sehemu ya dada wawili).  Hivyo Ndugu khalisa wa kiume atapata thumuni(1/8).  Kila dada khalisa atapata nusu ya thumuni (1/16).

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share