Simu Katika Shariy'ah Ya Kiislamu - 1

 

Simu Katika Shariy'ah Ya Kiislamu-1

Imekusanywa Na: Sulaymaan ‘Iysaa

 

 

Alhidaaya.com

 

 

BismiLLaahir Rahmaanir Rahiym

 

 

Simu katika lugha ya kiarabu inaitwa “HAATWIF” au “AL-JAWWAAL” au “TILFUUN” vyovyote iwavyo simu ni chombo kitumikacho kwa ajili ya kuwasiliana.

 

Uislamu upo pamoja na wakati (Yaani haujapitwa na wakati kama wanavyodhani wasioujua Uislamu au maadui wa Uislamu kadhalika. Wakati upo na Uislamu.)  Tazama watu wakisema nani wa kwanza kufika mbinguni? (si kwenye sayari kama tunavyosikia na kuona katika vitabu). Basi jawabu si mwengine bali ni Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Vile vile wakisema ni nani wa kwanza kufanyiwa upasuwaji? Basi jibu si mwengine bali ni Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); bali kafanyiwa upasuaji mara mbili. Al-Muhim, mambo ya utumaji wa barua toka sehemu kwenda sehemu nyengine, mawasiliyano haya ya simu au mfano wake japo si katika sura iliyo sasa duniani ya mtandao huu wa simu ni vitu ambavyo Uislamu umetangulia zaidi – someni mkitaka historia ya Uislamu.

 

Mnamo mwaka 1865 liliasisiwa shirika la Nokia na mwaka 1972 ilitoa simu ya kwanza na ilikuwa simu hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya askari tu. Na mnamo mwaka 1981 ikatoka simu nyengine tena, na mwaka 1992 ikatoka simu nyengine tena -hata nyakati zote hizi ilikuwa simu ikiuzwa bei ghali mno kwa kipindi hicho– hivyo ikapelekea kutomiliki chombo hichi muhimu katika mawasiliano baina ya mtu na mtu ila watu wenye uwezo kama vile wafanya biashara na watu wenye vyeo au nyadhi fulani. Kisha baada ya hapo ikawa simu inapatikana katika baadhi ya miji na nchi lakini bado ni kwa bei ya juu vile vile.

 

 

Hata hivyo kuna maswali ya kujiuliza kama Mwafrika wa Afrika Ya Mashariki lini iliingia simu kwako?  Runinga (Television) ilivumbuliwa mwaka 1944, kwako iliingia lini?

 

Al-Muhim, yakupasa uelewe kuwa Uislamu upo na zama na zama, hali kadhalika upo na Uislamu -kuna baadhi ya simu zina mambo makubwa na ajabu na bei yake ni kubwa, hata hivyo hilo si lengo, lengo ni kuielezea simu na adabu zake katika shari’ah ya Kiislamu nianze kwa kusema.

 

 

Kila sifa njema anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Swalah na salamu zimuendee Rasuli wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Swahaba zake na wote walioongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya Qiyaamah.

 

Ama baada ya utangulizi huo, hakika adabu ya simu kwa mujibu wa shari’ah tukufu ya Kiislamu haiepukiki kabisa na kuchukuliwa kifiqh katika adabu za ziara (yaani kutembeleana), na adabu za katika idhini (yaani kubisha hodi), na adabu za kuzugumza baina ya mtu  na mtu kwa kulingana na hadhi na nafasi yake, kwa kulingana kadhalika na wakati na sehemu yenyewe. Vyote hivi vimeelekezwa na Uislamu kinaga ubaga (wazi wazi) kwa ajili ya kuyajenga maisha ya Muislamu chini ya tabiya zilizojaa upole na ulaini, na hakika pamethibiti katika Sahihi Muslim kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Hakika hauwi upole (ulaini) katika kitu ila hukipamba kitu hicho, na hauondolewi upole (ulaini) katika kitu ila hukiaribu.” 

 

Na katika Hadiyth nyingine:

 

“Aliyenyimwa upole amenyimwa kheri zote” [Imepokelewa na Muslim.]

 

Adabu za simu ni adabu zitakikanazo kujulikana baina ya pande mbili:

1.     Mpigaji simu

2.   Mpokea simu japokuwa mpiga simu kwake ni muhimu zaidi kujipamba na adabu hizo kuliko mpokea simu.

 

Ndugu msomaji, bila shaka ni jambo lisilojificha kwako na mwengine kuwa simu ni chombo kinachosimamia mambo mengi na makubwa katika maisha ya kila siku yahusiyanayo na dini na pamoja na dunia. Sehemu ambayo ingeligharimu gharama ya muda wa kwenda na kurudi, mali nyingi, nguvu nyingi, kwa kupitia simu yamekuwa mambo hayo sasa yawezekana kufanyika kwa gharama chache bila kutumia nguvu nyingi katika hilo.

 

Hakika si mwengine anayestahiki kushukuriwa kwa neema hii ila Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kumpa mwana Aadam akili iliyomuwezesha kuvumbua na hatimaye kutengeneza chombo hichi.

 

 

Tuanze basi kutaja adabu moja baada ya nyengine:

 

 

1.    Kuhakikisha namba ya unayempigia

Hakikisha namba ya unayempigia kwanza kabla ya kuruhusu simu iite upande wa pili (kwa mwenzio) ili usje kufanya makosa kumwamsha aliyelala na asiyekuwa yule unayemuhitaji, au kumsumbua mgonjwa na kadhalika. Hivyo, hakikisha namba kwanza au tazama vyema simu yako katika sehemu ya majina na namba.

 

Na kwa upande wa mpokeaji ni vizuri pindi atakapogundua kuwa mpiga simu huyo hakuwa anakukusudia wewe, ni kumsamehe kwa usumbufu ambao utakua umeupata na kumfahamisha kuwa namba si hiyo umekosea, kama alikusudia kukuudhi basi utakua umepenyesha mshale katika moyo wake nawe una malipo na madhambi ni kwake.

 

 

2.    Wakati wa kufanya mawasiliano

Pindi unapofanya mawasiliano -kumbuka kuwa- kama ilivyo kwako kuwa ni mwenye shughuli nyingine basi kadhalika wenzio mambo ni hivyo hivyo, wanahitajia muda wa mapumziko kwa sababu ya mihangaiko yao ya kimaisha, wanahitaji kulala, kula na kadhalika.

Kwa kuzingatia hayo, shari’ah ya Kiislamu tukufu ikampa fursa mwenye kutembelewa na mfano wake -katika hili mpigiwa simu-, ikampa haki ya udhuru (huwenda amelala, huenda ana jambo analisimamia, huenda… huenda… huwenda…) pasi na kusababisha aingie katika kusema uongo ambao umeharamishwa na shari’ah ya Kiislamu. Ndio utakuta mtu yupo ndani lakini kwa kuwa amelala amepumzika au ana mgonjwa anamhudumia –anajilazimisha kusema uongo “mwambie baba hayupo”, hali ya kuwa yupo mtu hajui kama anamfundisha mwanae uongo!! Mwanae huyu pengine naye aseme uongo au ashindwe na aseme kama alivyoambiwa “baba anasema hayupo”!!

Hivyo shariy’ah ya Kiislamu ili haya yasitokee ikasema,

وَإِن قِيلَ لَكُمُ ارْجِعُوا فَارْجِعُوا ۖ هُوَ أَزْكَىٰ لَكُمْ ۚ

 

Na mkiambiwa: Rejeeni! Basi rejeeni. Huo ni utakaso zaidi kwenu. [An-Nuwr: 28]

 

Ni juu yako kutafuta wakati muafaka ukichunga nyakati za kazi, nyakati za kula na mapumzko ya mchana (Qayluulah). Tazama tu kwa mfano vile shari’ah tukufu ya Kiislamu ilivyowaamrisha watumwa na wajakazi pamoja na watoto wadogo chini ya umri wa baleghe katika idhini katika nyakati tatu:

  • Kabla ya Swalah ya Alfajiri
  • Wakati wa Dhwahira (wakati wa Qayluulah)
  • Wakati baada ya Swalah ya ’Ishaa.

Ama ambao si watumwa wala wajakazi na ambao ni baleghe mfano wangu mimi na wewe, ikatutaka shari’ah ya Kiislamu kutaka idhini (kubisha hodi) kila wakati – kama Alivyoeleza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa mapana na marefu kuanzia Aayah ya 58 mpaka Aayah ya 59 Suwrah-Nuwr. Na kama haitoshi, akakataza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mtu kuja usiku wa manane nyumbani kwake pasina kutoa taarifa.  Yote haya ni ili asije akakutana na yatakayomkera na kumuudhi kama vile kutokuwepo na usafi wa kuridisha upande wa nyumba yake, wanawe na kadhalika. Hali kadhalika kwa upande wake yeye asije akawakera kwa kuwakatiza usingizi wao na kadhalika.

 

Kwa ufupi ni kwamba chunga mnaasaba na muafaka wa kufanya mawasiliano na kama akakutaka udhuru mpaka wakati mwengine basi kubali kwa moyo mkunjufu. Na kama akakuambia subiri, basi subiri bila kuchukia juu ya hilo. 

 

Hata hivyo hili la kuchunga wakata muafaka wa kufanya mawasiliyano si kwa kila mtu na kila ofisi na mashirika na makampuni _ kwani maeneo ya huduma ya jamii ambapo huwa wazi kwa ajili ya kuihudumia jamii usiku na mchana hawaingii katika hukumu hii – hili limechukuliwa Qiyaas (kipimo) katika faida ya Aayah ya kutaka ya kutaka idini “si vibaya kwenu mkaingia (bila ya kutaka idhini) katika nyumba ambazo hazikaliwi na watu ndani yake mna mahitajio yenu – na Allaah anajua mnayo ya dhihirisha na mnayo yaficha” 29 Suwrah An-Nuwr hapo inaingia kufanya mawasiliano wakati wowote ule na maeneo yatoayo huduma ya jamii kama vile – vituo vya afya  vituo vya usalama (polisi, zima moto) vituo vya usafiri, mahoteli na kadhalika.

 

 

3       Muda wa miito ya simu

Yatakikana kulazimiana na sifa ya kati  na kati; kuwa na dhana ya juu kabisa kuwa unayewasiliana naye kwa muda wote wa uitaji simu yake itakua amejua na kupata taarifa kuwa una haja ya kuzungumza naye, na wala haizingatiwi idadi ya miito ya simu kuwa iite mara tatu au uwasiliane naye mara tatu kama inavyoelekeza Hadiyth sahihi katika [Sahihi Al-Bukhaariy na Sahihi Muslim kuwa amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Atakapobisha hodi (kutaka idhini) mmoja wenu mara tatu kisha hakukaribishwa basi na aondoke.”

kwani Hadiyth hii imebainishwa hekma ya kubisha hodi, nayo ni kwa ajili ya kuyahifadhi macho yasije yakaona yale ambayo mwenye nyumba au aliye ndani hakupenda yaonwe na mwengine. Akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Hakika si vinginevyo kubisha hodi (kutaka idhini ya kuingia) ni kwa ajili ya kuyahifadhi macho.” Imepokewa na Al-Bukhaariy

 

Na hili la kuifadhi macho halipo katika simu, hata hivyo jiepushe na kukariri na kurudia rudia kumpigia simu “eti mpaka apokee”. Huenda akawa anaswali hivyo ukamuudhi yeye pamoja na kumtia tashwishi na wasiwasi katika Swalah yake na hata wenzake -kama ni Swala ya jamaa-. Au yupo katika kikao au mkutano pamoja na wenzake, kwani tunaona alikuja mwanamke mmoja kwa Imaam Ahmad (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akagonga mlango kwa nguvu na kwa muda mrefu, akatoka Imaam naye akiwa anasema “ugongaji gani huu? huu ni ugongaji wa kiaskari, naye akiwa amechukizwa na kitendo hicho.

 

Bali angalia wema waliotangulia, swahaba (Radhwiya Allaahu ’anhum) katika ukubwa wa ajabu zao pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “walikua wakibisha hodi na kutaka idhini katika milango ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ncha za vidole ya mikono yao” ameipokea Hadiyth hii Imaam Al-Bukhaariy katika ktabu chake “Al-Adabul-Mufrad ” na Al-Qurtwubiy katika tafsiri yake (12/218).

 

Mfano wa hili la kupiga mlango kwa nguvu katika zama zetu hizi, ni kengele zilizowekwa katika milango na mageti yetu.

 

 

(inaendelea.../2)

 

 

 

 

Share