Amejimai Na Mumewe Akiwa Katika Hedhi Kwa Kughafilika Je, Afanyeje?

ASSAALAAM ALAYKUM,

 

MIMI NINA SWALI MOJA AMBALO NINANITATIZA MIE NA MUME WANGU. KWA BAHATI MBAYA, SIKU MOJA WAKATI NILIKUWA KATIKA SIKU ZANGU ZA HEDHI TULIFANYA TENDO LA NDOA ILIKUWA BAHATI MBAYA WALA HATUKUSUDIA. TULIZIDIWA NGUVU WOTE WAWILI. NILIKUWA KATIKA SIKU YANGU YA MWISHO NA ILIKUWA SIKU YA PILI TU NIJITOHARISHE, LAKINI BAADA YA KUFANYA TENDO HILO NIMEJIKUTA NIMETOKA DAMU TENA KWA WAKATI ULE ILA HAIKUENDELEA. MUME WANGU SIKU YA PILI HAKUWA NA RAHA NA KUJILAUMU KWA NINI TULIJISAHAU. JAMBO HILI LIMEKATAZWA NA S.W JEE TUFANYE NINI ILI TUOMBE MAGHFIRA KWA MOLA WETU?

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kujimai na mume, mke akiwa katika hedhi.

Haifai kwa mume kujamiiana na mkewe akiwa katika hedhi au nifasi mpaka atwaharike (al-Baqarah [2]: 222). Hata hivyo, Uislamu umemuacha huru mume na mke kufanya mengine yote mbali na jimai. Ikiwa mke atakuwa amefunga sehemu zake za siri basi mumewe anaweza kufanya naye mengine yote ambayo mume anaweza kufanya na mkewe ila kumuingilia mbele au kwa nyuma. Kufanya moja ya hayo mawili ni madhambi kwa wenye kufanya hilo.

Inayotakiwa kwa mume kujitahidi sana asiingie katika kufanya tendo la ndoa wakati mke yuko katika hedhi ili wasiingie katika haramu kama mlivyofanya. Ni vyema muweze kushindana na matamanio, kwani matamanio yakiwa hayatawekewa vikwazo yatampeleka mtu katika ushirikina...wakawa kama wale waliofanya matamanio yao kuwa ndio mungu wao! Ikiwa mume na mke wanaona hawawezi kujizuilia ni vyema wachukue tahadhari ya ziada ili wasiingie katika haramu na madhambi.

Nyinyi wanandoa ndio mnaojua kuwa hilo tendo mlilofanya ni bahati mbaya au vinginevyo. Ikiwa kweli ni bahati mbaya basi mtatubia kwa kutimiza masharti yafuatayo:

 

1.     Kuacha dhambi hilo, usilirudie tena.

2.     Kujuta kwa kutekeleza kosa hilo.

3.     Kuazimia kutorudia tena dhambi hilo.

 

Kulingana na swali lako ni kuwa mmetekeleza masharti hayo tuliyoyataja hapo juu. Mbali ya hayo ya kutubia iko kafara kama anavyotueleza Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika uhusiano wa mtu atakayemuingilia mkewe wakati yuko kwenye hedhi kama ifuatavyo: “Mwache atoe dinari moja katika sadaka au nusu ya dinari” (at-Tirmidhiy, Abu Daawuud na atw-Twabaraaniy, nayo ni Swahiyh).

Kwa hiyo, yeyote aliyeteleza akafanya kosa la jimai na mkewe wakati yuko katika hedhi na kabla ya kuwa ametohirika, itampasa atoe thamani ya uzito wa dinari ya dhahabu au kwa wakati huu ni kiasi cha thamani ya gramu 4.25 ya dhahabu au nusu yake.

Bonyeza viungo vifutavyo kwa malezo zaidi:

Hukmu Ya Kitendo Cha Ndoa Katika Hedhi

Nimemuingilia Mke Wangu Akiwa Katika Hedhi. Je, Ndio Sababu Ya Kukosa Uzazi/Watoto?

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share