Kila Zikija Posa Baba Anazitia Ila Hata Haniulizi Mwenyewe Nami Nataka Kuolewa Nifanyeje?

 

SWALI:

 

A.a sheikhe nawapa shukran alihidaya kwa kuweza kuturekebisha na kutunfunza mambo yote yakidunia tulio na tashwishi nayo...jaza yenu iko kwa allah.me nimsichana 24, niko na shida moja kila nikija kuposwa haifiki mbali nitaona kimya hakuna tena lolote kuhusu ndowa.me natamani nianze maisha yangu ya ndowa lakini naona kheri zangu zina tashwishi. Babangu akija mtu kuniposa yeye lazima amtie mtu kasoro na ilaaa mpaka sasa kama wanaume kumi wote ameshawatia ila...and yeye huzijibu hizo posa bila kuniuliza lolote hata hajawahii kuniuliza wala kutaja mambo ya harusi yangu..Me naona sio haki hapo hajui mwenyewe nataka wala sitaki...Hazungumzi na mimi kuhusu ndowa kabisa...yeye anatupenda sanaa sikatai tena sana kila tutakalo anatufanyie alahmdulilah,, lakini kila wakati ukipita na umri nao wapita. Kama hivi mimi napendana mtu amekuja kuleta maneno ya uposi sasa ni miezi miwili babangu ananyamaza tuuuu hajibu lolote. Sijui itakuwaje na huyo mtu ni Muislamu ananipenda sana nani mtu mzuri sanaaa.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu posa zinazo kuja na kukataliwa na babako kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe. Suala hili na shida uliyo nayo ni katika masuala nyeti sana katika jamii kwa kiasi ambacho la mwanamme na mwanamke hawana Imani basi wanaweza kuingia katika madhambi ya uzinzi.

 

Inaonekana kuwa wazazi wameshindwa kuona tatizo hilo na watoto nao wameshindwa kuweza kukaa na wazazi wao na kulizungumzia suala hilo kwa kina. Lako mwanzo ni kuwa na subira huku ukingoja jawabu la babako mzazi. Kuna tatizo pia kuwa watoto wanashindwa kuelewa hekima na busara ya wazazi kwa kukataa posa. Hii ni kuwa lipendalo roho ni dawa, na kwa sababu ya msichana kumpenda mvulana huwa haoni kasoro zake, hata akiwa mume ni chongo msichana husema ni makengeza lakini mzazi hutizama maslahi ya msichana wake ili asiingie katika shida wala matatizo.

 

Mbali na ksuema hayo, mwanamke katika mas-ala ya ndoa ana haki ya kuulizwa na kukubali kuhusu mume atakaye kuwa wake wa mustakbali. Kwa hapa sisi tunaweza kukushauri yafuatayo:

 

1.                  Awali ya yote swali Swalah ya Istikhaarah, kumuomba Allaah Aliyetukuka Akubainishie kheri au shari ya huyu mume aliyekuja. Kisha naona umekosea sana ukisema kuwa huyu bwana ni Muislamu anayenipenda sana. Mapenzi hujitokeza na kuonekana mnapooana kwani wanaume wengi huwa wana mchezo wanaocheza kujionyesha kuwa ni wacha Mungu na wenye kupenda kubadilika tu baada ya kupata atakalo na baadaye kutokujali tena. Kwa hiyo, tahadhani sana na ufanye uchunguzi wa kina kwa wanaomjua kujua uhakika wake.

 

 

2.                  Ikiwa Istikhaarah imekuonyesha kheri ya huyo mume, jaribu kukaa na babako kwa njia muruwa ya heshima na uzungume naye kwa upole na hekima kuhusu suala la ndoa yako.

 

 

3.                  Ikiwa ni vigumu kwako kufanya hivyo zungumza na mamako ambaye atakuwakilisha kwa babako. Ikiwa si mamako mzazi basi watumie watu wengine ambao watazungumza na babako kama vile shangazi au ami au jamaa mwengine wa karibu ambaye anaweza kuzungumza na babako kuhusu suala hilo la ndoa yako.

 

 

4.                  Waweza pia kumtumia Shaykh au mwalimu wa Madrasah amabaye anaaminiwa na babako ili kumzungumizia kuhusu hilo.

 

 

Hatuna shaka, ufumbuzi wa tatizo lako utapatikana kwa pia kuzidi kumuomba Allaah Aliyetukuka wakati unapofunga funga ya Sunnah, kuamka usiku na kuswali Tahajjud kisha kumuomba Yeye kwa unyekevu na wakati mwingine ambao du’aa zinakubaliwa kwa haraka.

 

Pia tungependa kukushauri utilie maanani sana hukmu za Kiislamu pamoja na kuchunga mipaka yake. Kwa hiyo, inatakiwa musiwe mnakutana na huyo aliyekuja kukuposa wala kuzungumza naye, kwani hizo ni njia za kumfungulia milango shetani ya kuweza kuingia na kuwashawishi. Na kufanya hivyo ni njia moja ya zinaa na mnakuwa na madhambi mbele ya Allaah Aliyetukuka.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

  

 

Share