Rafiki Yake Amekiri Kuwa Ametenda Maasi Ya Zinaa Sasa Hamuamini Tena, Je Aachane Naye Au Aendelee Naye

SWALI:

 

Asalam ‘alaykum warahmatullahi wabarkat. 

Nina rafiki yangu tuseme kama mchumba wangu. Tunasoma, mimi nasoma nje ya nchi ila tumeahidiana tukimaliza shule inshaallah tutaoana. Nampenda na naamini nae ananipenda na niko tayari kusubiri ingawa tuna miaka mingi ya kusubiriana. Hivi karibuni, kanambia mwenyewe kwamba ameshiriki na mtu tendo la ndoa. Sikuwa nimemuuliza alisema mwenyewe na akasema kwamba alishatubia kwa M/mungu na akaniahidi hatarudia tena kwani alipitiwa na shetani tu na kwamba anaomba msamaha kwangu pia. Nilikasirika na nilimchukia kwa kitendo alichofanya. Nikamsamehe ingawa kila muda ninapokumbuka huwa inaniuma na najaribu kusahau lakini ikikumbuka huwa nahisi namchukia. Huwa nawaza je vipi kama bado anafanya, nilikuwa namuamini coz ni muumini mzuri wa dini, ananiambia aliteleza, tuna miaka ya kusubiriana je kwa kipindi hiko atateleleza mara ngapi? kwa kifupi nashindwa kumuamini kama zamani nilivyokuwa namuamini na najiamini kwake, imani kwake imepungua  nakuwa na wasiwasi kama kweli tutafika. Na kuwa na hasira nae na ina sababisha mara nyingi twagombana bila sababu.  Je nifanyeje? 

Wabillahi tawfiiq


 

JIBU:

 

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mchumbako aliyeteleza na kuingia katika dhambi kubwa la zinaa. Tufahamu kuwa kila mwanadamu ni mkosa na bora wa mwenye kukosa ni mwenye kutubia na kurudi nyuma na akaweka ahadi ya kutorudia tena.

 

Na kwa kuwa umesema kuwa una muda kabla ya harusi huenda akashawishika tena kwani kitendo cha ndoa kina utamu wake na ushawishi kutoka kwa aliyefanya naye kitendo huenda ukazidi mpaka awe na Imani kubwa ya kutorudia. Bila shaka, una haki ya kukasirika lakini mliingia katika mtengo kuanzia mlipofanya urafiki baina yako na wewe na mkaanza kuzungumza kwani jambo hilo halifai kisheria.

 

Hata hivyo, katika suala lako hilo unaweza kufanya moja kati ya mawili yafuatayo:

 

1.      Kumsamehe, na kuolewa na mwengine  awe ni halali yako kuzungumza naye. Ukichagua kipengele hiki itabidi usahau kabisa yaliyopita na ugange yajao. Ukiwa hutaweza basi, kipengele cha pili ni,

 

2.      Umsahau kabisa na umtoe katika mawazo yako. Tatizo la kuolewa naye ukiwa na mawazo ya yaliyotendeka kila wakati yatakuwa yanajitokeza baada ndoa na kitu kidogo huenda kikakufanya umkumbushe jambo hilo, jambo ambalo litaleta matatizo makubwa katika ndoa yenu.

 

Ushauri wa mwisho ambao tunaweza kukupa ni uswali Swalah ya Istikhaarah kabla ya kuamua lolote lile. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akufanikishe uchague lililo na kheri nawe katika maisha yako na Akhera pia.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

  

 

Share