Kuzini Kabla Ya Ndoa Ni Dhambi? Baada Ya Kuolewa Amegundua Mume Hana Nguvu Za Kiume, Aachike Asiingie Katika Maasi?

 

Asaalaaam Aleykum

Nina swali linanitatiza kuzini kabla ya ndoa ni dhambi na ikitokea ukampenda mtu na kufunga ndoa bila kukutana kimwili halafu baada ya ndoa unagundua mwenzio ana mapungufu ya nguvu za kiume na tayari mna watoto, na kuzini nje ya ndoa ni dhambi kumuacha mume kwa ajili ya tatizo hilo sidhani kama ni haki, na kujisaidia mwenyewe kujipunguzia tamaa ya mwili ni dhambi je unashaurije hapa. Mume nampenda na sitaki kuwanyima watoto mapenzi ya baba na mama.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuzini kabla ya ndoa na matatizo ya ukosefu wa nguvu za kiume.

 

Hakika ni kuwa ni dhambi kubwa kwa mwanamme na mwanamke kuzini kabla au baada ya ndoa. Japokuwa madhambi ya kuzini ndani ya ndoa ni makubwa zaidi hata adhabu yake hapa duniani ni kubwa zaidi kuliko zinaa kwa wale wasioa au kuolewa.

 

Allaah Aliyetukuka Ametuonya juu ya zinaa pale Alipotuambia:

Wala msikaribie zinaa kwani huo ni uchafu na ni njia mbaya kabisa” (al-Israa’ [17]: 32).

 

Ama adhabu hapa duniani kwa mwenye kuzini kabla ya kuoa au kuolewa ni kupigwa mijeledi mia moja bila huruma (an-Nuur [24]: 2).

 

Mapenzi ni kawaida baina wanaadamu kwa jinsi moja au nyingine. Na huenda mwanamke akavutiwa na mwanamme na akatamani kuwa mwanamme huyo awe mumewe kama vile alivyompenda Khadiyjah binti Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘anha) Mtume wa Allaah, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata hivyo, mapenzi hasa ya jinsia mbili tofauti ni baada ya kufungamana kwa uhusiano unaokwenda sambamba na shari’ah ya Kiislamu.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Kufanya Mapenzi Bila Ya Kitendo Cha Ndoa Kwa Ambaye Hajaolewa?

 

Kulala Pamoja Bila Ya Kufunga Ndoa

 

 

 

Ni hakika kuwa baada ya kuoana ndio hujitokeza mambo mengi sana baina ya wanandoa. Na huja wakagundua mambo ambayo walikuwa hawayajui hivyo kuwa ni changamoto kubwa sana baina ya wanandoa ambayo inaweza kutishia uhusiano wao wa kuishi pamoja. Matatizo hayo hutokea kwa mume au mke kwa namna moja au nyingine. Ukosefu wa nguvu kwa mume katika ndoa ni sababu moja ambayo shari’ah imempatia haki mwanamke aende kwa Qaadhi ili aombe talaka. Shari’ah imeliangalia hilo katika madhara ambayo anaweza kuyapata. Kwa hiyo, inabidi mke achague dhara dogo katika madhara mawili. Na katika kesi yako, kuna madhara mawili, moja kubwa la kubaki na mume na huku unazini ambayo kishari’ah mzinifu aliyeoa au kuolewa anahukumiwa kupigwa mawe mpaka kufa au dhara dogo la kuomba talaka ili upate nafasi ya kuolewa na mwanamme mwingine. Hivyo, utaona kuchagua dhara dogo hapo ni nafuu zaidi kwako na kwa dini yako ikiwa unahisi hutoweza kuvumilia kabisa kubaki katika ndoa bila tendo la ndoa.

 

Hata hivyo, ushauri wetu kwako ni kuwa jaribu kuzungumza na mumeo aende kwa wataalamu wa magonjwa ya uume ili aweze kutibiwa kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufahamisha kuwa hakuna ugonjwa usiokuwa na dawa yake. Kwa kutafuta matibabu huenda ndoto yako ya kubakia na mume unayempenda ikatimia. Wala usikate tamaa kwani Muislamu hafai kukata tamaa na rehema ya Allaah Aliyetukuka. Hata ikiwa hamkufanikiwa na matibabu ya hospitali basi nenda kwa wataalamu wa tiba ya kitwabibu kutumia miti shamba na madawa mengine ya Ki-Sunnah. Pia musisahau nyote wawili kumuomba Allaah Aliyetukuka ili amuondolee mume wako tatizo hilo na Allaah Aliyetukuka ni Mwenye kujibu du’aa zetu. Kwa hivyo, ikiwa umeshindwa kukaa na mumeo na ugonjwa huo kubakia hata baada ya kutafuta matibabu basi unaweza kuomba talaka kutoka kwake au kwa Qaadhi na hiyo ni haki yako.

 

Ama kujipunguzia matamanio ya kimwili kwa njia moja au nyingine kama kutumia vidude vya kiume vya kutengeneza, kujisaga na njia nyingine zozote ni haramu katika shari’ah ya Kiislamu. Ikiwa unataka kupungunza matamanio basi chukua agizo la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kufunga. Na pia unaweza kujishughulisha kwa kufanya mazoezi na kuutumia muda wako kwa harakati tofauti ili uweze kuzitumia nguvu za ziada katika mambo hayo ya faida kwako kwa mwili.

 

Ikiwa unampenda kweli mumeo basi utamsaidia katika kupata dawa na matibabu ili muendelee kubakia pamoja. Na pia unaweza kumsaidia kwa kutofanya haraka wakati wa tendo la ndoa. Kwa sababu ya udhaifu anatakiwa yeye aende taratibu na wewe pia umuendeshe mumeo taratibu wakati mnastarehe. Mnaweza kuanza na maneno matamu yanayohusiana na tendo hilo la ndoa, busu, kushikana shikana na mwisho kabisa tendo lenyewe. Kufanya hivyo kunaweza kumweka yeye katika hali nzuri na yale mapungufu yakafunikika.

 

Twawaombea kila la kheri katika uanandoa wenu pamoja na kutatulika kwa udhaifu huo wa mumeo inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share