Kutumia Miswaak Na Faida Zake

Kutumia Miswaak Na Faida Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum warahmatullahi wabarakatu.

 

Mimi naomba mutuletee darsa inayohussu sunna ya miswaak (msuaki wa jiti aliokua akitumia Nabii Salla-Allaahu  wasalam,  jinsi gani ya kutumia kama na dawa au mtupu, unaweza kupiga chooni au la, ni wakati gani na wakati gani, jinsi ya faida  ziliomo katika miswaki hiyo ili tufaidike na sunna hiyo kwani katika waislam ni wachache wanaoidumisha sunna hii na wengine hata misuaki yakawaida hawatumii katika sala zao au wakati wa kulala huchukulia kupiga ukiamka inatosha kutokana na kukosa elimu hii.

 

Mimi ninaishi ulaya na nina chumba kimoja sina ukumbi jiko nashea na watu wa dini tofauti kwa hivyo miswaki hupiga chooni kwani chumbani nahofia mtoto wangu asinione kwa sababu yeye nimemfundiha asitembee na msuaki kila pahala apige chooni amalize atoke msafi na ana miaka

 

 

Jee niko sawa?.  Allaah akuzidishieni elimu, awazidishieni moyo wa kuipeleka mbele dini yetu na allah atusamehe madhambi yetu tunayo yajua na tusiyojua. amin

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Msuwaki ni miongoni mwa Sunnah nzuri ambazo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   ametuachia:

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه- عن النبي صلى الله عليه وسلم  قال: " لو لا أن أشق على أمتي لأمرتهم بالسواك عند كل صلاة".  رواه البخاري

 

Abuu Hurayrah (Radhwiya-Allaahu 'anhu) amehadithia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Lau si ugumu ambao Ummah wangu ungepata ningeliwaamrisha kupiga msuwaki (kabla ya) kila Swalaah” [Al-Bukhaariy]

 

Msuwaki unaweza piga katika sehemu nyingi kwa mfano chooni, Msikitini wakati unatawadha, unapoingia nyumbani, pia chumbani. Hata hivyo, ukipiga chumbani mtu ahakikishe kuwa hajachafua kwa kutema mate au vinavyotoka mdomoni ovyo ovyo:

 

عن عائشةَ رَضِيَ اللهُ عنها  أنَّ النبيَّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم كان إذا دخَلَ بَيتَه بدأ بالسِّواكِ

 

 ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: Kitu cha kwanza ambacho Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akifanya anapoingia nyumbani ilikuwa ni kupiga msuwaki [Muslim].

 

Kwa kawaida, msuwaki wenyewe huwa na dawa lakini ukitaka kutia dawa kwa juu hakuna shida yoyote ile. Utumiaji huwa ni kwa utumiaji wa kijiti au kitu chengine chochote kusafisha meno yake. Kitu bora cha kusafishia meno ya mmoja wetu ni kijiti cha mti wa arak ambao unapatikana Hijaaz.

 

Ada hii ya utumiaji wa msuwaki huimarisha ufizi, hulinda meno kuoza na magonjwa ya meno, inasaidia usagaji wa chakula na kusahilisha utokaji wa mkojo:

 

عن عائشةَ رَضِيَ اللهُ عنها، عن النبيِّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم أنَّه قال:  السِّواكُ مَطهَرةٌ للفَمِ، مَرْضاةٌ للرَّبِّ

‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Msuwaki unasafisha mdomo na unamridhisha Rabb” [Ahmad, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy].

 

Utumiaji wa msuwaki unapendeza kila wakati, lakini zipo nyakati nyingine ambazo inapendeza zaidi haswa nyakati zifuatazo:

 

1.      Wudhuu,

2.      Swalaah,

3.      Usomaji wa Qur-aan,

4.      Unapoamka, na

5.      Pindi ladha yam domo inapobadilika.

 

Wasiofunga au waliofunga wanaweza kutumia bila ya tatizo lolote. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatumia msuwaki na huku akiwa katika Swawm [Ahmad, Abuu Daawuwd na at-Tirmidhiy].

 

Ni Sunnah kuuosha msuwaki baada ya kupiga, amesema hilo ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

alipomaliza kutumia msuwaki, alikuwa ananipatia mimi. Nilikuwa nauosha, nautumia, nauosha tena, kisha namrudishia” [Abu Daawuwd na al-Bayhaqiy].

 

Na pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutuonyesha umuhimu wa msuwaki amesema: “Mambo kumi ni katika fitrah: … kupiga msuwaki…” [Muslim na Abuu Daawuwd].

 

Ni muhimu umfundishe mtoto wako kuwa mtu anaweza kupiga msuwaki mahali popote bora tu achunge usafi la sivyo, basi mtoto atakuwa anapiga chooni peke yake na akifika Msikitini hatakuwa na hamu wala motisha ya kupiga.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share