Hampendi Mumewe, Hawana Masikilizano, Hawalali Pamoja Miaka Anadai Talaka Lakini Mume Hataki Kutoa – Je Ndoa Inasihi Bado?

 

SWALI:

 

Assalam alaykum, Naomba kujua hukumu ya Mwanamke ambae hampendi mume na wala hawasikilizani na wameasiana hawalali pamoja kwa mnyaka, Mwanamke anaomba talaka kila siku na Mwanamme hataki kutoa talaka. Jee hiyo ndoa bado ipo? Natanguliza shukran na kuwaombea kila la kheri duniani na Akhera Amiin.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke kutompenda mume na hata kwa sasa wameasiana. Mwanzo ni kukujulisha kuwa ndoa bado ipo baina ya wanandoa hao wawili, kwani mwenye kumiliki talaka ni mume hajatoa talaka hiyo.

 

Suala la mwanamke kutompenda mwanamme kwa sababu moja au nyingine lilitokea wakati wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam).  Na sheria hii inaitwa khul’u (kujivua mwanamke katika ndoa). Hadiyth ifautayo inathibitisha:

 

Mke wa Thaabit bin Qyasi (Radhiya-Allaahu ‘anhu)  alikwenda kushitaki kuwa hamtaki mume ambaye hana kosa lolote isipokuwa kwa maumbile yake.  Akamwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Ewe Mtume wa Allaah; Thaabit bin Qays, simsimangii tabia wala dini, lakini nachukia kukufuru katika Uislamu. Mtume akamwambia utamrejeshea shamba (bustani) yake? Akasema: ndiyo. Mtume akasema kumwambia Thaabit, ‘kubali shamba na umtaliki talaka moja’”. Hadithi hii imepokelewa na Imam Al-Bukhaariy. Na katika Riwaya nyingine ya Hadithi hii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema: “Utamrejeshea shamba lake (ambalo alikupa kama mahari?) akasema: ndiyo, akarejeshewa shamba lake kisha Mtume akamuamrisha atengane naye”.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Kujivua Mwanamke Katika Ndoa (Khul'u) Na Hukumu Zake

 

Sababu Gani Zinamruhusu Mke Kuomba Talaka?

 

Sababu Gani Zinamruhusu Mke Kuomba Talaka?

 

 

 

Kwa hiyo, kwa kesi hii inabidi mwanamke aende akashitaki kwa Qadhi au shaykh ambaye anaaminika kwa elimu yake, uchaji Mungu wake na uadilifu. Kwa kujikomboa na kujivua katika ndoa (Khul’u), mwanamke atarudisha mahari na atakuwa ametalikika. Hii ikiwa mume hana makosa ya aina yoyote ile.

 

Ikiwa mume ndiye mwenye makosa kwa kutotimiza mambo ambayo ni wajibu wake kama kumlisha mke, kmvisha na mengineo, Qadhi atawaatisha lakini mke hatolazimika kurudisha mahari aliyopewa wakati wa nikaha.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share