Mke Anayo Haki Kisheria Kutamka Talaka Kwa Mume? Amefanya Hivyo Kisha Baada Ya Muda Ameolewa Na Mwengine

 

SWALI:

 

Nini hukmu ya mwanamke anaye mtamkia mme wake talaka;tangia leo mimi sio mke wako baada ya muda anaolewa na bwana mwingine.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke kutamka talaka kwa mumewe. Kiislamu haki ya talaka anayo mume, ambaye anapoitoa hata kwa mzaha talaka inakuwa imepita.

 

Mke ikiwa hataki kubakia na mume kwa sababu moja au nyingine ni lazima aende kwa Qadhi ili kuchukua talaka yake. Mke anaweza kupata talaka kupitia kwa Qadhi kwa njia mbili:

 

  1. Mume hana makosa ya aina yoyote yale lakini mke ndie hataki kuishi na mume huyo. Hii ni talaka ya kutoka kwa mwanamke, itambidi mke arudishe mahari na wanandoa hao watenganishwe hali hiyo mke atarudisha mahari. Hii ni kutokana na sheria ya khul’u ambayo inapatikana dalili kutoka usimulizi ufuatao:

 

Mke wa Thaabit bin Qyasi (Radhiya-Allaahu ‘anhu)  alikwenda kushitaki kuwa hamtaki mume ambaye hana kosa lolote isipokuwa kwa maumbile yake.  Akamwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Ewe Mtume wa Allaah; Thaabit bin Qays, simsimangii tabia wala dini, lakini nachukia kukufuru katika Uislamu. Mtume akamwambia utamrejeshea shamba (bustani) yake? Akasema: ndiyo. Mtume akasema kumwambia Thaabit, ‘kubali shamba na umtaliki talaka moja’”. Hadithi hii imepokelewa na Imam Al-Bukhaariy. Na katika Riwaya nyingine ya Hadithi hii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema: “Utamrejeshea shamba lake (ambalo alikupa kama mahari?) akasema: ndiyo, akarejeshewa shamba lake kisha Mtume akamuamrisha atengane naye”.

 

 

  1. Mume ana matatizo makubwa ambayo yanamfanya mke asipate haki zake za kisheria. Katika hali hiyo Qadhi, atamshurutisha mume atomize haki hizo au atoe talaka na kuwatenganisha baina yao wawili bila ya mke kurudisha mahari.

 

Ikiwa mke ndiye aliyemtamkia mumewe kuwa amemtaliki bado talaka haijapita baina yao. Ikiwa mke ameolewa na mume mwingine hakuna ndoa bali watu hao wawili kisheria wanakuwa ni wenye kuzini.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share