Mume Alimfanyia Maudhi Hadi Alimlazimisha Amuache – Akampa Talaka Tatu – Moja Alkuwa Mja Mzito - Mbili Alizitoa Haikupita Mwezi

 

SWALI:

 

Assalam aleykum.

 

Mimi nina swali la kuhusu ndoa yangu, tulioana wenyewe mahakamani bila ya mafunzo yoyote, mume wangu aliniahidi atanipeleka kwao lakini ilichukua mda mpaka nimejifungua mtoto mmoja.

 

Alikua na matatizo yake na mchumba wake wa zamani ambaye alitaka kumuoa, alikua akipelekeshwa kama mtu alorogwa kwani hakua anajielewa kile anachofanya, ikiwemo bangi pia alikua anavuta na pombe pia anatumia, kwa kweli alinifanyia maudhi mpaka nikawa naomba talaka mwenyewe kwa kuhisi labda atatulia lakin skufanikiwa.

 

Alikua hataki kabisa kuniacha ila nilikua namlazimisha mpaka anaandika, katika talaka hizo tatu moja nilikua ni mja mzito je ilisihi. Alafu hizo mbili nyengine likua namlazimisha akaandika ila hakuna hata moja haikupita mwezi alikua ananirudia,pia skumbuki kama nlikua twahara au la alipokua ananiacha.

 

Naomba msaada wenu kwani bado mume wangu tunapendana ila sote tulikua hatujielewi kiakili hatufahamu kama zimepita zote au la, jee tufanyeje????

 

 

Aassalam aleikum warahma tuwallah wabaratatu. Nawashkuru watu wa alhidaaya kuwa na site hii kwa kupata kutuelimisha.

 
Swali langu:  Tulikua na ugomvi na mume wangu, na kila ninapokua na hasira nakua na jazba kubwa sana, ulipokua tunagombana nilikua namlazimisha aniache mara zote nalimtia hasira mpaka akawa anajiandikia kwa mihasira bila kunitamkia na kuondoka zak, ila katika talaka zote hizi iliwemo moja nliku na mimba, haikuweza kufika hata miez miwili alikua ananirejea.
 

Tatizo ni kwamba yeye anavosema hakua na lengo wala nia ya kuniacha ilikua anajiandikia bila kujielewa kwani alikua tayari yeye ana hasira na jazba, na kuhusu mimi kua twahara kusema kweli hatukua na elimu hiyo hakua ananisubiria kupata ada ya mwezi na kua twahara wala kutoniingilia, ilikua tunapeana tu vikaratasi bila kuelewa tunafanyaje kati yangu na yeye.

 
Naomba jibu la haraka, kwani familia yake tayari wana wasiwasi kwamba mimi si mke tena nimeachika talaka tatu. Na sisi kwa vile hatukua na elimu ya kutosha kuhusu ndoa, sasa hivi tunaogopa kwani hatujielewi kama hizo talaka zilipita au la na tuna mtoto tayari mmoja.   

 

SUKRAN JAZILA.


 

JIBU:

 

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu talaka baina ya wanandoa. Kuna msemo unaosema asiyefundishwa na wazazi hufundishwa na ulimwengu.

 

Sisi tuko katika enzi ambayo elimu imepanuka kwa kiasi kikubwa na imekuwa sahali kuipata au kuulizia. Mmekaa kwa muda mrefu na tatizo bila kuulizia mpaka sasa maji yamemwagika yamekuwa hayawezi kuzoleka tena.

 

Tufahamu kuwa talaka ni kitu kizito sana katika Dini yetu ya Uislamu. Talaka ni kitu ambacho mzaha wake ni kweli na kweli yake ni kweli. Kuna wakati mume anapotoa talaka anakuwa ni mwenye kupata madhambi lakini talaka inakuwa imepita bila ya shida wala tatizo lolote. Mifano ni:

 

  1. Wakati mke yuko katika ada yake ya mwezi au nifasi.

  2. Katika twahara ambayo mke ameingiliwa na mume.

 

Mume akitoa talaka akiwa katika hali ya hasira, talaka inapita bila ya tatizo. Mume mzuri na Muislamu mwema ni yule mwenye kumiliki hasira zake wakati akiwa na ghadhabu. Talaka ambazo zinapotolewa hazipiti ni:

 

  1. Mwendawazimu anapotoa talaka.

  2. Mtoto mdogo mpaka abaleghe.

  3. Aliyelala mpaka anapoamka, na

  4. Aliyelazimishwa lakini sio na mke. Mume ndiye kiongozi wa nyumba hafai kukubali kutenzwa nguvu na mkewe aliye chini katika mamlaka.

 

Ikiwa mke amepatiwa talaka tatu moja baada ya nyingine anakuwa ameachika hawezi kurudiwa na mume huyo wake mpaka mke aolewe na mume mwingine aonjwe katika kustarehe naye. Baada ya hapo mume huyo wa pili akimuacha kwa njia ya kawaida kabisa, ndipo itakapokuwa halali kwa mume wa kwanza kumrudia.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share