Talaka Kwa Kuasi Amri Ya Mume

 SWALI: 

 

 

 

Assalam alaykum ama baada ya kukutakieni kila la kheri na mafanikio mema napenda kutoa shukuruni zangu kwa juhudi zenu zote mnazochukua katika Alhidaaya haswa katika kujibu masuali.

Napenda kwa leo niulize juu ya suali la talaka: Jee ikiwa Mke amemwambia mumewe anatoka nje ya nyumba ama kwenda kwa jirani, kwa shoga au kusafiri, kisha mumewe akamkataza na akamwambia kama ukitoka (ikiwa nipo au sipo nyumbani), basi ujue ndio talaka yako (nimekuwacha).

 Jee ndoa namna hii inasihi ikiwa mke yule ameasi amri ya mumewe na kutafuta safari? Ahsanteni sana Alhidaaya. Allah akutakabalieni dua zenu zote AMIN. 


 

 JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Mola Mlezi wa viumbe vyote, Swalah na salamu zimshukie hashimu kipenzi chetu, Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم  na Masahaba zake  رضي الله عنهما na waliowafuatia kwa wema mpaka Siku ya Kiyama.

Ni shukrani kwa dada yetu ambaye ametuuliza swali hili kuhusu talaqa. Na pia ni shukrani kwake kutuamini katika hilo.

Mwanzo tunatakiwa tuelewe kuwa talaqa kisheria ni kujiondoa katika mafungamano ya kindoa au ni kumaliza uhusiano wa kindoa.

Lengo kubwa la ndoa ni kuwaweka watu wawili (mume na mke) katika mahusiano ya kukaa pamoja mpaka kufa kuzikana. Na ndio kwa ajili hiyo Allah akayaita mahusiano hayo kuwa ni ahadi nzito (Miithaaqan Ghalidhwa). Allaah سبحانه وتعالى  anasema kuhusiana na hilo:

}}وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَى بَعْضُكُمْ إِلَى بَعْضٍ وَأَخَذْنَ مِنكُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا{{

{{{Na mtachukuaje, na hali nyinyi kwa nyinyi mmeingiliana? Nao (wanawake) wamepokea kwenu ahadi thabiti (kuwa mtakaa nao kwa uzuri )}}  An-Nisaa 4: 21

Hii ni kama ile ahadi ambayo Mayahudi waliyopatiwa na Allaah سبحانه وتعالى kuwa wasiruke mipaka kwa kuvunja taadhima ya siku ya Jumamosi nao wakatoa ahadi iliyo madhubuti lakini wakaivunja kwa kutotekeleza hilo.

}}وَقُلْنَا لَهُمْ لاَ تَعْدُواْ فِي السَّبْتِ وَأَخَذْنَا مِنْهُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا{{

{{ ….Na tukawaambia: Msiivunje Siku ya Sabato (Jumaa mosi). Na tukachukua kwao ahadi iliyo madhubuti}}

An-Nisaa 4: 154

Na hii ni halali pekee ambayo inachukiwa sana na Allaah سبحانه وتعالى. Na kuna hadiyth ambayo inaonyesha ni jambo linalomuudhi Mwenyeezi Mungu ila hadiyth hiyo kwa mujibu wa wanachuoni wa hadiyth wamesema ni dhaifu, nayo ni hii:

((Imepokewa kwa Ibn ‘Umar رضي الله عنه   kwamba Mtume wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم   amesema: “Halali inayochukiwa sana na Allah Aliyetukuka ni talaqa”)) (Abu Dawud na Ibn Maajah)

Hivyo wanandoa wanatakiwa wavumiliane na mmoja akiwa mkali mwengine awe baridi kwani ukali unampatia nguvu shetani kuweza kuivunja nyumba. Lakini mbali na hayo kuna wakati talaqa inakuwa ni bora yakiangaliwa mahusiano ya wanandoa, kwani msingi wa Uislamu ni: “Haifai kujidhuru wala kudhuriana (kudhuru mwengine)” (Ibn Maajah na Daraqutniy kutoka kwa Abu Sa‘iid al-Khudriy رضي الله عنه  

 Kuna baadhi ya wakati ambapo mume akitoa talaqa huwa haichukuliwi; Ya kwanza ni talaqa ya anayelazimishwa kwa dalili ya Hadithi iliyopokewa kutoka kwa:

((Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema: “Kila talaqa inakubaliwa ila talaqa ya aliyelazimishwa juu ya akili (matashi) yake”)) (at-Tirmidhy).

Na Allaah سبحانه وتعالى anatufahamisha juu ya mtu anayelazimishwa kutamka kufuru bila ya kuamini basi hiyo haiathiri Imani yake:

{{Anayemkufuru Allah baada ya Uislamu wake isipokuwa yule aliyeshurutishwa, hali ya kuwa moyo wake umetuwa juu ya Imani}} An-Nahl :106).

 Hivyo yule mwenye kushurutishwa kutoa talaqa, talaqa yake haichukuliwi. Mtume wa Allaah  صلى الله عليه وآله وسلمamesema: ((Ummah wangu umenyanyuliwa makosa na kusahau na wanayo shurutishwa)) (Ibn Maajah, Ibn Hibbaan, ad-Daraqutniy, at-Tabarani na al-Haakim).

Talaqa ya mwenye kufanya mzaha au dhihaka inakuwa imetuka (imehesabika), kwani ndoa yake pia ni sahihi. Hii ni kwa Hadithi iliyopokewa kwa ((Abu Hurayrah رضي الله عنه  kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    amesema: “Mambo matatu ambayo ni ya dhati ni ya dhati (kweli) na dhihaka kwayo pia ni dhati: Ndoa, talaqa na kumrudia mke”)) (Ahmad, Abu Dawud, at-Tirmidhy na Ibn Maajah).

Baada ya hayo tukirudi katika swali ni kuwa mume akimwambia mkewe kuwa nimekutaliki kesho au baada ya mwaka au ukitoka nje ya nyumba basi talaqa itakuwa imepita. Sasa kusihi ndoa na kuwa ndoa haisihi inategemea talaqa aina hiyo imetokea mara ngapi. Ikiwa mume ametoa sharti hilo na mke akatoka nyumbani mara ya kwanza, hiyo itakuwa ni talaqa ya kwanza ambayo ni rejea (yaani wanaweza kurudiana) ima kabla ya eda kumalizika au ikiwa eda limemalizika itabidi mume apeleke posa mpya na mahari mapya na mke akubali kurudiwa. Lakini ikitokea mara ya tatu hiyo inakuwa ni talaqa wasioweza kurudiana mpaka mke aolewe na mume mwengine wafanye tendo  ndoa  kisha aachwe. Ikiwa ataachwa anaweza kurudiwa na mume wa kwanza bila ya matatizo yoyote.

Na Allaah Anajua zaidi

  

 

Share