013-Kutoa Zakaah: Aliyefariki

 

Kutoa Zakaah: Aliyefariki

 

Alhidaaya.com

 

 

Anasema Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah kuwa, katika madhehebu ya Maimaam Ash-Shaafi’iy na Ahmad na Abuu Thawr, ni kuwa mtu akifarki na akaacha deni la Zakaah, basi inawajibika katika mali yake kwanza kutolewa deni la Zakaah, tena iwe kabla ya kutimizwa wasia alioacha na kabla ya urithi kugawiwa.

 

Allaah Anasema:

 مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ

"Baada ya kutoa wasia aliousia (maiti) au kulipa deni". [An-Nisaa: 11]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa". Na Zakaah ni deni la Allaah.

 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

 

“Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Mama yangu amefariki na anadaiwa saumu ya mwezi mzima, je nimlipie?"

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:

"Mama yako angelikuwa na deni ungemlipia?"

Akasema:

"Ndiyo, ningemlipia".

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

"Basi deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa". [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Share