021-Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Mapambo

 

Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Mapambo

 

Alhidaaya.com

 

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana katika kuzitolea Zakaah dhahabu na fedha za mapambo.

 

Wapo waliosema kuwa dhahabu au fedha ya kujipamba inapofikia Niswaab yake lazima itolewe Zakaah yake, na hawa wameegemeza Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema kumwambia mwanamke mmoja aliyemvisha mwanawe mkufu wa dhahabu akamwambia:

 

"Unailipia Zakaah yake?"

Akasema:

"La, hatuilipii"

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

"Huogopi Allaah akakuvalisheni mikufu ya Moto? Zilipie Zakaah yake". [Ahmad]

 

Na pia Hadiyth iliyosimuliwa na Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) aliposema:

 

"Aliingia chumbani kwangu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniona nimevaa pete za fedha. Akaniuliza:

"Nini hiki Ee ‘Aaishah?"

Nikamwambia:

"Nimezitengeneza ili nijipambe kwa ajili yako ee Rasuli wa Allaah".

Akasema:

"Unazilipia Zakaah yake?"

Nikasema:

"Hapana."

Akasema:

"Hiyo inatosha kwa (kukupatia adhabu ya) Moto". [Abuu Daawuwd – Ad-Daaraqutniy na Al-Bayhaqiy]

 

Ama wale wanaosema kuwa Dhahabu ya mapambo hailipiwi Zakaah, wao wameegemeza hoja zao katika Hadiyth iliyosimuliwa na Al-Bayhaqiy inayosema:

 

"Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliulizwa juu ya mapambo:

"Yanatolewa Zakaah?

Akasema:

"La, hayatolewi"

Akaulizwa:

"Hata kama thamani yake itafikia Dinari elfu moja?'

Akasema:

"Zaidi" (hata kama zaidi ya thamani hiyo)

 

Na pia Hadiyth iliyomo katika Muwataa, kitabu cha Imaam Maalik inayosema:

 

"Bibi ‘Aaishah alikuwa akiwalea wana wa kaka yake mayatima na walikuwa na mapambo na hakuwa akiyatolea Zakaah.”

 

Atakayezichunguza Hadiyth hizi na zile, ataona kuwa zile zinazolazimisha kuitolea Zakaah dhahabu au fedha ya mapambo ndizo zenye nguvu zaidi na zenye uhakika zaidi kuliko zisizolazimisha - Wa-Allaahu A'lam.

 

Share