Malezi Ya Mama, Mama Yangu Ana Upendeleo Ananitumia

 

SWALI:

Assalam alaikum,

Mimi ni mwanamke nishaolewa na mume wangu yuko nje anafanya kazi so naishi na familia yake ingawa ni kwa mvutano sana. But niko na familia ya mamangu ambayo iko kando nami huiangalia kwa hali na mali coz mama kaashwa na baba na hakuna wakumwamgalia, nina ndugu watatu mmoja mwanamke na wawili waume.hawa waume mmoja yuko four 3 na mmoja amemaliza four four but yuko nyumbani sina uwezo wa kumpeleka college.

Huyu wa kike ni dadangu mkubwa but alikimbia nyumbani akaenda kwa mwanamume ambaye ni mkristo,sasa mimi huiangalia familia ya mama kwa hali na mali ingawa naishi kando. 

Mama alikuwa na wasiwasi sana kuhusu msichana wake aliyekimbia na alikuwa na mimba na jamaa walisema yule kijana waliamchukuwa kwa unganga na huyu dada kila siku alikuwa akiambia jamaa kuwa atarudi nyumbani lakini hakurudi mpaka siku alipojifungua na kurudi nyumbani na mama akampokea kwa mikono miwili akisema ni mwanangu na yeye sie wa kwanza kuzaa haramu. Na mama anamuhudumia kwa kila kinachohitajoka kwa aliye zaa.Na huyo mwanamume wake anakuja nyumbani akaingia chumba cha dadangu wakazungumza bila kuwa na mtu.Hili liliniuma sana nikamwelezea mamangu akasema afanye nini na yeye ni babake mtoto na angonje amalize damu awaoze.nikamwambia kuwa si katai but pia dada alikuwa akilalamika hamtaki kisha imekuwaje amekubali kumwoza akasema shauri yake!kwani mwanae akizini pia yeye atapata dhambi.Kila nikijaribu kumweleza mamangu hivyo afanyavyo si sawa coz huyu kijana asingemkubalia aingie home ovyo ovyo but mama huwa mkali anasema nataka yeye afe!Na mimi ni mja mzito nataka kwenda kwake kujifungua.

mamangu anataka nikienda kuzaa nibebe kifurushi cha pesa,na mimi kila siku husimamamia gharama za nyumbani!hili liliniuma sana ambapo dadangu hampi hata ndururu but anamwangalia kwa hali na mali!na kumbe siku zote tuko kwa nyumba mamangu hapawi pesa na dadangu but mimi anataka kila mwezi nimpe pesa za matumizi na pia niwasomeshe kaka zangu.Yeye husema dadangu hajapokea but yuko kazini kila siku napia ananifisha kuhusu dadangu kipesa

Hivi dadangu hasaidii kitu na mama hataki kuambiwa ukweli.ukisema anasema atajiuwa coz hatumsikizi mimi nimeumia sana tena hali hii ni mja mzito nimeona dhiki zaidi.Nimeshindwa nimridhshe vipi naogopa sije akaniapiza!mimi ndie naumia kwa kumtizama yeye mwengine akisherekea jasho langu

Sasa nimeamua nisiende kwa mamangu tena nikizaa nikae kwangu coz mimi pia sina pesa nyingi za kuangalia nyumba mbili but najitahidi but mamangu kila kukisha anaitisha pesa JE NIFANYE NINI? I am confused

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani dada yetu kwa maelezo yako marefu na ni masikitiko kwetu kuhusu yanayokukumba. Haya ni mitihani na misukosuko ambayo mja mwema wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) hukumbana nayo kwa njia moja au nyengine. Mitihani hutofautiana baina ya Muislamu na mwengine kulingana na Imani zao. Kila Imani ikipanda juu ndio mitihani inakuwa mingi zaidi. Miongoni mwa mitihani mikubwa ni mtu kuwa anasumbuliwa na mtu aliye jamaa yake ya karibu. Hakika ni kuwa ndiye aliye karibu zaidi na mtoto wake.

Katika hayo yote yanayokukumba mwanzo tunakunasihi sana ushikamane na Taqwa, 'Ibaadah, subira na uzidi kumtendea wema mama yako. Hakika ni kuwa Uislamu kutoka nyenzo zake za msingi, Qur-aan na Sunnah za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimewapatia wazazi daraja kubwa. Inatakiwa uwatendee wema na kuwasaidia kwa kadiri ya uwezo wako. Allaah Aliyetukuka hatakuadhibu kwa jambo ambalo lipo juu ya uwezo wako. Anasema Aliyetukuka: "Allaah haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo" (2: 286).

Kwa jinsi ulivyotueleza kuhusu usaidizi unaompatia mamako, hakika ni kuwa umefanya jambo kubwa katika hilo na Insha Allaah, Allaah Atakujazi na kukuondolea matatizo na misukosuko.

Mbali na kusema kuwa ni wajibu wa mtoto kuwatii wazazi wake wawili (mama na baba) kwa mambo ambayo hayaendi kinyume na maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini pindi anapokuamuru ufanye yanayo kwenda kinyume na Uislamu basi hufai kabisa kuwatii. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:  

((Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio))

 ((Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anayeelekea kwangu)) [Luqmaan: 14-15]

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hapana utii kwa kiumbe kwa kumuasi Muumba))

Dada yetu kaika Imani una jukumu kubwa kwa dada yako ya kumtoa katika aliyo nayo ya madhambi. Inabidi ukae kitako na kuzungumza naye kuhusu hayo anayoyafanya hayafai katika Uislamu. ikiwa hakukusikiliza katika hilo, wewe utakuwa jukumu lako umelitekeleza na hutakuwa na lawama mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Kutofanikiwa huko kusikurudishe wewe nyuma katika juhudi zako kwani hutapenda wewe uende Peponi naye aingie Motoni siku ya Qiyaamah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: "Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahli zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allaah kwa anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa" (66: 6).

Inabidi pia ukae na mamako chini ukiona ni wakati mzuri kwake wa kuzungumza naye, na zungumza naye kwa utaratibu na kumuekea heshima yake. Ukiona hakusikilizi basi angalia watu wa karibu naye katika jamaa kama dadake au kakake ili wazungumze naye. Kwa kufanya hayo huenda akaona haki na akabadilika. Hilo ndilo lengo la kila Muislamu ambaye anataka kuona kuwa watu wake wa karibu wamekuwa Waislamu wema na wazuri. Na kwa mama kusema atajiua kwa kutaka kumrekebisha ni uwongo wala hawezi. Jambo hilo lilitokea katika maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pindi alipopatiwa utume, mama wa Swahaba mmoja alimwambia akibakia katika Uislamu basi yeye atabakia katika jua, hatokula mpaka afe. Swahaba huyo alipokataa kuacha Uislamu yule mama hakufanya hayo yote aliyonuia kuyatenda.

Inabidi tuwe makini na imara katika mas-ala ya Uislamu na wala tusiyumbeyumbe katika haki. Katika hali ya uja uzito ambayo huwa ni hali ngumu wakati ambapo kunakuwa na mabadiliko ya kisaikolojia, fiziolojia na homoni ni vyema sana usiwe na harara. Inatakiwa uwe na utulivu wa moyo na nafsi katika kufanikisha hilo, na jitahidi ujiondoe katika migogoro yoyote. Hivyo, nasaha yetu kwako ni afadhali uzalie kwako ili mawazo na dhiki zote zikuondokee kwani inaweza kusababisha uzito katika shughuli nzima ya uzazi. Ikiwa uko katika haki na hujamkosea heshima, unamtendea wema, unamkirimu, unazungumza naye kwa njia nzuri basi kuapiza kwake hakutafika kokote. Allaah Aliyetukuka Atakuwa nawe katika dhiki zako. Tufahamu kuwa hapana dhiki juu ya dhiki, kwani baada ya dhiki ni faraja. Ni matumaini yetu kuwa faraja ipo karibu kwako insha Allaah.

Zidi kumvumilia, kumsaidia kwa kiasi cha uwezo wako, mtendee wema, zidi kumuomba Allaah Amuongoe, zungumza naye kwa njia iliyo nzuri kabisa pamoja na kufanya 'Ibaadah kama inavyotakiwa. Nasi tutakuwa nawe katika du’aa wakati huu mgumu ingawa tuna imani kuwa utapata afueni kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

Tunakutakia kila la kheri, subira na fanaka hapa ulimwenguni na kesho Akhera. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ambadilishe mamako na dadako wawe ni Waislamu wema na wazuri na waache yote ya maasi insha Allaah, Aamiyn.

Na Allaah Anajua zaidi  

 

Share