Sina Utulivu Katika Ndoa Yangu Baada Ya Kudanganywa na Mume Wangu Pamoja na Mama Mkwe

SWALI:

 

MIMI NIMEOLEWA MIAKA MIWILI. SINA UTULIVU KABISA KATIKA NDOA YANGU. BAADA YA SIKU MBILI YA HARUSI MUME WANGU ALIKUWA NA KAMA WASIWASI, HASA WAKATI WA 'KULALA' ALINISIMULIA KUWA KUNA MSICHANA WA UKOO WAO AMBAE WATU WAKE HUYO MKE WALIMTAKA AMUOE, LAKINI YEYE HAKUMTAKA WALA MAMAKE PIA. AKAHOFIA PENGINE WAMEMFANYIA KITU. NILIGUNDUA JAMAA ZAKE HAWANA FURAHA WANAPONIONA MIMI MPAKA SASA. ALIAMBIWA MAMANGU NA MWANAMKE AMBAE NI JAMAA YA MUME WANGU KINYUME YA MANENO AMBAYO YALINICHOMA SANA. TANGU SIKU HIYO SIJAKUWA NA FURAHA. NAHISI KAMA NIMEDANGANYWA NA KUDHULUMIWA. NILIMWELEZA MUME WANGU YALE NILOYASIKIA. ALIKANA NA KUAPA MUNGU KUWA NI MANENO YA UONGO. SIKURIDHISHWA NA JAWABU LAKE. NIKAWA KILA NIKIGHADHIBIKA HUMKUMBUSHA MANENO HAYO. MAMAKE PIA ALIAPA NA KUKANA KUWA SI MANENO YA KWELI. SIJARIDHIKA BADO. MARA HULIA PEKE YANGU NIKAKOSA USINGIZI KWA MAFIKRA CHUNGU NZIMA. NIMECHUKIA MAISHA. HASA WATU WA MUME WANGU. NAOMBA USHAURI KWENU.


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mahusiano yako na mumeo. Mwanzo dada yetu tunakushauri sana tena sana uyathamnini maisha yako wala usifanye jambo ambalo linaweza kukupelekea kujidhulumu pamoja na kuidhulumu nafsi yako ambayo ni ghali na yenye thamani mbele ya Allaah Aliyetukuka. Utulivu mara zote hupatikana katika kujali maagizo ya Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam). Hayo hupatikana kwa kusoma Qur-aan kwa kufuata maagizo yaliyomo ndani, kumtaja Allaah kwa wingi, kuleta istighfaar, kufanya Ibaadah kama ya Swalaah za faradhi na Sunnah, funga na Ibaadah zote aina nyinginezo. Fanya bidii ujikurubishe kwa Allaah Aliyetukuka kwa kufuata yaliyo amrishwa na kuacha makatazo Yake.

 

Utulivu hauji tu hivi hivi. Bali watu wengine wasio wapendelea wenziwao mema hujaribu kila njia kuleta bughudha na kutosikilizana baina ya watu wawili wapendao au wenye mafungamano ya kama wanandoa. Kuna watu maumbile yao ni hasadi na chuki kwa wengineo, hawapendi wenziwao wapate kheri ya aina yoyote ile. Kwa hiyo, inatakiwa wewe uwe ni usaidizi kwa mumeo ambao anapigwa vita nje na watu wake na wewe ambaye ni wapili wake badala ya kumsaidia unasaidia maadui zake katika kuvunja nyumba yenu changa.

 

Mume wako kukusimulia yaliyopita ni jambo zuri kwani ungekuja jua hayo baadaye ungehisi kuwa mumeo amekuficha na hivyo hakukutakia kheri. Mumeo aliona kuwa ana   pili wake ambaye angeweza kumtegemea katika matatizo ya kimaisha anayo kumbana nayo ili muweze kusaidiana. Na lengo la ndoa ni hivyo muweze kusaidiana ili kukabiliana na changa moto zozote zile na matatizo. Dunia ni mitihani na kila mmoja wetu atafikiwa na mitihani ya aina yake yaliyo tofauti na mwenziwe. Leo ni mumeo ana dhiki na shida kesho inaweza kuwa ni wewe au mmoja wa familia yako. Wakati huo utahitajia mumeo asimame na wewe kwa kukushauri, kukuliwaza na kukupatia moyo au akwambie shauri yako, hayo niko sio yangu.

 

Hakika ni kuwa jamaa zake hawawezi kuwa na furaha na mumeo kwani waliona atamuoa binti yao kwa kule yeye kuja kukuoa wao ndoto zao zote zimeanguka. Kwa hiyo, wanaona njia ya pekee ni kuwasha moto wa fitina baina yenu ili muachane pengine huenda akamuoa huyo binti yao. Muislamu ni yule mwenye kuzingatia na kufikiria vyema pamoja na kuona mbali, nawe unatakiwa uwe na busara ya aina hiyo kuilinda ndoa yenu, haswa ndoa yako.

 

Tunakupongeza kuwa nawe ulikuwa mkweli kwa mume wako kwa kumwambia uliyoyasikia kwa lengo la kutaka kujua ukweli na kutatua tatizo kama lipo baina yenu. Lakini unatakiwa uwe mwangalifu sana katika kuchukua maneno ya watu bila ya kuyachunguza. Mara zote mtu anapokuletea maneno inatakiwa uwe jasiri na mkakamavu wa kuweza kumwambia mwenye kuleta maneno ngoja nimuite yule ambaye unataka kumsema. Ikiwa ni mwongo ataruka kuwa hilo halina haja na hatakuletea tena maneno ya mumeo wala ya mtu mwengine. Wewe na mumeo mnatakiwa muaminiane mmoja anapomueleza jambo mwenziwe kwani bila ya hivyo itakuwa ni balaa baina yenu ambazo hazimaliziki kabisa maisha na mwisho itawapelekea kuachana. Ikwia mumeo amekueleza na kisha akaapa kuwa hivyo ni hivyo inatakiwa umuamini na usahau suala hilo wala isiwe kuwa mnapokosana unarudia jambo hilo tena tena. Hiyo itakuwa ni kutonesha kidonda ambacho bado ni kibichi na si njia nzuri ya kuweka uhusiano mwema baina yenu.

 

Isitoshe mama mkwe wako amekuelezea pamoja na kuapa kuwa hayo uliyoelezwa sio ya kweli, hata hivyo wewe bado hujatosheka, hujaridhika wala kuamini. Huu ni mtihani kwako na pia kwa mumeo hivyo unatakiwa kuwa na subira na uongoze Ibaadah na bila shaka Allaah Aliyetukuka Atakusaidia kwa njia muruwa kabisa. Usichukie nafsi yako bali jitahidi kufanya mema na jirekebishe na njia yako itakuwa nzuri hapa duniani na Kesho Akhera.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share