Nini Hukumu Ya Mwanamke Kumkimbia Mumewe Na Hali Mumewe Anamtaka?

 

SWALI:

 Ndugu wana “Alhidaaya.com"
Assalam Aleykum!
Alhamdulillahi kuniwezesha tena kuwasiliana nanyi baada ya kuridhika pia kwa maswali yangu jinsi mlivyonijibu. Allahu Akbar, mmenielimisha kweli na ni fursa vile vile kwa waislamu wengine kunufaika kwa kupata sabuni ya roho.
Allah awafunguliye elimu zaidi tuendeleye kukosha mioyo yetu. Kwa hiyo ndugu zangu, maswali yangu mengine, nahitaji uvumbuvi kwenu Inshallah ni:  

1. Ikiwa mke kamtoroka mumewe na akajirudi kwa kumuomba msamaha mumewe kwa kisa chake cha kuukimbiya tu ujumba wake wa ndoa na sio tena kurudi kuendeleza maisha na mumewe, itakuwa vipi hapa na mume anataka mkewe arudi ili kuinusuru ndoa yao, na ndio shuruti la kumtakabilia msamaha? Naomba ufafanuzi zaidi?
  2. Na mwanamke
kama huyo nini hatma yake duniani na akhera kwa kumfanya mumewe ajikute kalazimika kuivunja ndoa yao na angalau mume bado anapenda aendeleye kuishi na mkewe?
  3. Naomba mnielimishe zaidi na waislamu wote, ni shuruti gani ambazo dini yetu ya ISLAM, inaruhusu mke muolewaji kuukimbiya ujumba wake ao mume kuukimbiya vile vile ujumba wake?
  Nitashukuru saaana kwa kupata jawabu kwa haya maswali ambayo unidadisi kila siku. Assalam Aleykum?

 


 
JIBU:

 

 Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum)   na walio wafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 Shukran kwa swali lako zuri kuhusu mas-ala ya unyumba ambayo ni matatizo makubwa sana katika jamii yetu ya Kiislamu katika nchi tofauti za Waislamu. Tukija katika maswali yako tunasema: -
 

Mas-ala ya Kwanza

Kwa mke kumtoroka mumewe kwa sababu yoyote ile au bila ya sababu ni makosa ambayo mwanamke wa Kiislamu hafai kufanya kabisa. Ikiwa mume amemkosea mke zipo njia ambazo zinaweza kufuatwa ili kutatua tatizo ambalo limetokea. Inatakiwa tuelewe kuwa kosa halitatuliwa na kosa.

Uislamu umeweka nidhamu ya kila jambo na kutoa suluhisho kwa matatizo yetu yote hata katika mas-ala ya ndoa, talaka na mengineyo. Kutoroka kutoka nyumba ya mume huwa bado hujatatua tatizo ambalo lipo. Ikiwa mume amemkosea mke inatakiwa mke amueke chini na kumueleza anavyofikiri kwa lile jambo. Ikiwa hakuweza kutatua, anaweza kuwatumia wazazi wake na wale wa mumewe au masheikh wazoefu katika mas-ala ya suluhu za kindoa. Mke kafanya vizuri kujirudi kwa makosa yakutoroka kwani makosa hayasamehewi na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) mpaka mtu aombe msamaha kwa aliyemkosea akiwa ni mwanadamu mbali na kujuta, kuwa na azma ya kutorudia kosa na pia kutolifanya kosa hilo. Sasa mke hajaomba msamaha kwani huu unakuwa ni kama mfano wa gazeti la Denmark, Jyllands-Posten, pale meneja aliposema tunaomba msamaha kuwaudhi Waislamu lakini sio kuchapisha vikaragosi vya Mtume (Swalla Allahu  'alayhi wa aalihi wa sallam). Na hapa tunaona hivyo hivyo kuwa mke amejirudi kwa kumuomba mumewe msamaha lakini hataki kubaki naye na mas-ala makubwa ya mtu anapofanya kosa na kusamehewa ni ajiondoe katika lile kosa na kurudi kama awali.

 

Ili kosa hilo kuondoka ni mke arudi baada ya kusamehewa katika nyumba yake ili waweze kuishi pamoja na mumewe na wawalee watoto wao ikiwa wanao. Na lau amekimbia kwa sababu ya tatizo baina yake na mumewe wanaweza kukaa chini na wakaangalia ni njia gani wanaweza kutumia ili kusuluhisha tatizo hilo.

 

Inafaa tutanabahi ya kwamba talaka ni jambo ambalo linachukiza sana na kutoroka kwa mke kutoka kwa mumewe au kwa mume kumtesa mkewe ni miongoni mwa matatizo sugu ambayo yanatakiwa yazungumzwe na tupate ufumbuzi wa mas-ala hayo. Nasaha yetu ni kuwa kunafaa kuwe na madada ambao wako karibu na dada yetu ili waweze kumnasihi na kumshauri na kumuuliza tatizo liko wapi ili waweze kutatua mzozo huo wa kifamilia na hivyo hivyo wanaume ambao watamshauri ndugu yetu ili kuweza kurekebisha matatizo ya unyumba baina ya hawa wanandoa na hata wengine ambao wana matatizo mfano wa huo. Hakika Misikiti na Maimamu wanafaa wawe na dauru muhimu katika kutatua matatizo na kindoa nyeti na hivyo kuweza kuzihifadhi ndoa za ndugu zetu. Inafaa pia wanandoa wapate ushauri nasaha kabla ya ndoa, wakiwa katika ndoa na kunapotokea matatizo kama hayo.

 

Mas-ala ya pili

 

 Mwanamke kama huyu hatima yake ni mbaya hapa ulimwenguni na Kesho Akhera, kwani Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ikiwa mwanamke yeyote atamuomba mumewe talaka bila ya kuwa na sababu nzito (yenye nguvu), harufu ya Pepo itakuwa ni haramu kwake” (Abu Dawuud kutoka kwa Thawbaan [Radhiya Allahu 'anhu] )

 Hii itakuwa ni hasara ambayo mke atapata Kesho Akhera. Tufahamu kuwa hapa duniani pia atapigwa muhuri wa unafiki. Mtume (Swalla Allahu  'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Wanawake ambao watajiachisha kutoka kwa waume zao na wanawake wenye kuwashawishi waume zao wawapatie talaka kwa malipo ni wanafiki” (at-Tirmidhiy na an-Nasa’iy kutoka kwa Abu Hurayrah [Radhiya Allahu 'Anhu]  

 

 Na hakika ni kuwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewazungumzia wanawake ambao wana sifa ya kubaki na waume zao hata kama waume wanataka kuwaacha kwa kuwa na maagano na ahadi kati yao. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

Na mwanamke akichelea kutupwa au kutojaliwa na mumewe, basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa machoni mwake tamaa na choyo. Na mkifanya wema na mkamchamngu basi hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayoyatenda” (4: 128).

‘Aishah (Radhiya Allahu 'anha) amesema yafuatayo kuhusu aya hii kuwa,  

“Ikiwa mwanamke akichelea kutupwa au kutojaliwa na mumewe” (yaani mume ameona kitu asichopenda kwa mkewe, kama uzee au mfano wake, na akataka kumpatia talaka, lakini mke akamtaka mume akae na ampatie anachopenda mwenyewe. Ndio Allah Akasema: ‘basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu’” (Al-Bukhaariy).  

Mas-ala ya Tatu

 Hapana sharti yoyote ambayo ipo katika Uislamu ambayo itamfanya mume au mke aukimbie unyumba. Kitu ambacho kipo si kukimbia ni kuachana na kuepukana kwa wema. Taizama jinsi Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Alivyowahutubia waume kwa kuwaambia kwamba:

  “Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu Ametia kheri nyingi ndani yake” (). T

 

Tuiangalie aya hii namna ambayo Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anavyo wahimiza wanaume wakae na wake zao kwa wema na hata ikiwa wana baadhi ya makosa huenda wakawa na mazuri mengine ambayo yatawavutia.

  Na kuhusu wanawake wema ni wale ambao wanafanya juhudi kubaki na waume zao na hata wakiwa wanaume wanataka kuwaacha basi wafanye juhudi ili wasiwe ni wenye kupatiwa talaka. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

  “Na mwanamke akichelea kutupwa au kutojaliwa na mumewe, basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa machoni mwake tamaa na choyo. Na mkifanya wema na mkamchamngu basi hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayoyatenda” (4: 128).

  Talaka inatolewa ikiwa imekuwa haiwezekani kwa ndoa kuendelea ima kwa sababu ya ugomvi au uasherati au sababu nyengine yoyote. Hii talaka inatakiwa itolewe kwa wema kwani wakati wa nikaha mume ameahidi ya kwamba atakaa na mkewe kwa wema na ikiwa imebidi kuachana basi wataachana kwa wema. Na ni muhimu tuelewe ya kwamba mke anayeachika anafaa katika eda yake ima tohara tatu au mpaka azae ikiwa ana mimba basi ni wajibu wa mume ampatie mtalaka wake sehemu ya kulala, chakula, nguo, matibabu na vitu vingine vyote alivyokuwa akimpatia kabla ya talaka. Yote haya ni kutoa nafasi ya watu hawa wawili kurudiana katika ndoa katika muda huu wa eda. na haifai kabisa kwa mume kuwatoa wake zao katika nyumba zao isipokuwa wanapofanya uasherati wa wazi. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

  “Ewe Nabii! Mtakapo wapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Mwenyezi Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya” (65: 1).

 Hivyo, ikiwa talaka inatolewa inatakiwa itolewe kwa wakati unaofaa na kila mmoja apatiwe haki yake na iwe ni katika wema. Kwa hiyo, haifai kwa mtu au mke kuukimbia unyumba bali wanafaa kuachana kwa njia nzuri.


  Na Allah Anajua zaidi.

 

Share