Mke Na Mume Wakigombana, Mke Akiondoka Bila Ruhusa Ya Mume Atakuwa Ameasi?

 

SWALI:

 

Ikiwa mume na mke wamegombana, mke akataka kuondoka, na mume anamkataza. Je mke akiondoka bila ruhusa atapata dhambi?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke kuondoka nyumbani baada ya ugomvi bila ruhusa ya mume.

Tuelewe kuwa ruhusa ya kutoka nyumbani pindi mwanamke anapoolewa iko kwa mume. Mume anapomtaka mke asitoke, pindi anapotoka basi mke atakuwa amefanya makosa, na kwayo anapata dhambi. Hivyo, inafaa kwa wanawake wasiwe ni wenye kuchukua idhini mikononi mwao kwani hilo litawafikisha mahali pabaya.

 

Mke anaweza kutoka tu bila ya ruhusa ikiwa mume amemtisha ima ya kumpiga au kumuua au kumfanya jambo jengine lolote baya. Hapo inafaa atoke ili aende akatafute usaidizi. Lakini ikiwa kumekuwa na ugomvi, mke anawajibika kutatua ugomvi huo uliotokea na mumewe kwa njia nzuri ya kutaka suluhu na wala sio utesi. Ikiwa mke amezungumza na mumewe lakini mume hasikii, anatakiwa awasiliane na watu wake kuhusu tatizo hilo ili waje watatue pamoja na watu wake. Ikiwa pia hatua hiyo imeshindikana kupata ufumbuzi basi atakuwa hana budi kwenda kwa Qaadhi au Shaykh mwenye elimu, mwadilifu ili atatue tatizo hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share