Du’aa Za Masjidul-Haraam Kuwaombea Maiti Ni Tafauti Na Kukusanyika Na Kumuombea Du’aa Maiti?

SWALI:

 

ASSALAAMU ALAYKUM WARAHMATULLAHI WABARAKAATUH.

 

Nimesoma katika category ya bid'ah - uzushi kuhusiana na suala la kukusanyika kumuombea marhum dua. Kuna mambo mengi bado yananipa utata wa hali ya juu. Je tunavyosikiliza Dua za Masjidil Haram (Makkah), dua mbalimbali zinasomwa ikiwemo kuwaombea dua aliyefariki. Je suala hilo liko tofauti na kukusanyika na kumuombea dua marhum?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu uombaji wa du’aa katika Msikiti Mtukufu wa Makkah na wakajumlishwa ndani yake walioaga dunia.

Hakika ni kuwa hayo ni masuala mawili tofauti kabisa yasiyolingana kabisa. Mikusanyiko yoyote inayofanyika ni lazima iende sambamba na shari’ah ya Kiislamu. Hakujapatikana kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) wala watangu wema waliokusanyika katika sehemu moja ili kumuombea maiti aliyekufa.

Kwanza ifahamike kuwa katika Masjidul Haraam, du’aa huombwa ndani ya Swalaah, katika Qunuut ya Witr na si baada ya Swalaah au nje ya nyakati za Swalaah.

 

Du’aa ndani ya Swalaah ni suala tofauti kwani maana ya Swalaah yenyewe ni du’aa. Sasa katika du’aa ambayo inayopatikana katika Swalaah kwenye Qunuut unatakiwa uombe mambo yote yaliyo mema na mazuri miongoni mwayo ni kuwaombea wale ndugu zetu katika Imani walioaga dunia wawekwe mahali pema na Allaah Aliyetukuka. Kwa hiyo, du’aa hazina tatizo kwani hamkujumuika kwa ajili ya kuombea kitu kimoja tu – maiti.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share