Kuvaa Mkanda Wenye Ngozi Ya Mnyama Katika Swalaah: Hukmu Yake

 

 

SWALI:

 

Asalaam Aleikum, Kwanza namshukuru Allah Subhaanahu Wa Taala kwa kuniruzuku hi nafasi ya kuuliza swali hili. Pili mi niko kikazi Oman, Juzi wakati tupo kwenye msikiti wetu wa hapa kazini, nilimuona kijana mmoja wa kutoka Bangladesh akivua mkanda wake wakati anaingia na kuuweka pembeni, alipomaliza kuswali, ilibidi nimuulize haswa kisa cha kuvua mkanda, akaniambia kuwa ni haraam kuswali huku umevaa mkanda ambao ni wa ngozi ya mnyama! kwa kweli sikuwezi kuelewa na ndo maana nikaone niwaulize nyie wenye elimu zaidi yangu ili nipate ukweli.

Allah awajaalie ujuzi na hekima zaidi.

Asalaam aleikum


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kufaa au kutofaa kwa ngozi ya mnyama.

Hakika suala hili halina utata katika Dini yetu ya Uislamu kwani lipo wazi kabisa. Ngozi ya mnyama inapotengenezwa kwa kutiwa madawa kiwandani au sehemu yoyote ile huwa ni halali kutumika kwani huko ndiko kuitwaharisha. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Inapodibaghiwa (kutengenezwa/kutiwa rangi madawa) ngozi ya mnyama, hutwaharika” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Amesema Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma), “Mtumwa wa Maymunah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipatiwa kondoo kamaa Swadaqah, akafa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpita kondoo huyo na kusema: ‘Kwa nini hamuitoi ngozi yake, mkaitengeneza na kuitumia?’ Akasema Maymunah (Radhiya Allaahu ‘anha), ‘Amekufa (bila kuchinjwa)’. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ‘Ameharamishwa kuliwa tu” (al-Jama’ah).

 

Imenukuliwa kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa alisoma:

Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharimishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe…” (al-An'aam (6): 145).

Kisha akasema: “Kilichoharamishwa ni nyama yake. Ama ngozi yake, ngozi kutumiwa kwa maji, meno, mifupa, manyoya na sufi, zinaruhusiwa” (Ibn Mundhir na Ibn Haatim).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share