Afanye Ibada Zipi Ili Aombe Kuondoa Matatizo?

SWALI:

 

Aslaam aleykum

Mimi ni kijana ambaye kwa hakika Allah [S.A] amenijali afya njema pamoja na familia yangu na namshukuru Allah [S.A] kwahilo na hakika hakuna mwanadamu ambaye hana matatizo sasa swali langu ni kwamba kuna tatizo kubwa sana linanisumbua katika maisha yangu na nimeshafanya ibada nyingi za sunna katika kuomba hili kwa Allah [S.A] kama kufunga siku saba pamoja na kuswahili swalatul hajj kwa rakaa nne na ya kwanza kusoma suratul fatiha na kulhulwahu 10 na rakaa ya pili suratul fatiha na kulhulwahu 20 na rakaa ya tatu suratul fatiha na kulhulwahu 30 na rakaa ya nne suratul fatiha na kulhulwahu 40. Je naweza kufanya kisimamo gani cha Sunna ili Allah [S.A] anajalie ninachoomba kwa wepesi na haraka zaidi

 

 

Wabillah tawfiq

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako kuhusu matatizo yanayokumbuka na kuomba kwako kwa Allaah Aliyetukuka kwa ajili ya kukuondolea matatizo hayo.

Ulimwenguni tumeletwa na Allaah Aliyetukuka ili kujaribiwa na kupatiwa mitihani. Kila mmoja miongoni mwetu anapata mtihani aina yake ulio tofauti na mwengine. Hiyo ndio ada ya Allaah Aliyetukuka kwa viumbe vyake.

 

Kuondoa matatizo na kujibiwa du’aa zetu kuna masharti yake bila kuyatimiza hatutakuwa ni wenye kujibiwa. Miongoni mwa masharti ni:

 

1.     Kula, kunywa na kuvaa vya halali.

2.     Kutofanya haraka kujibiwa kama kusema nataka Ee Allaah unijibu leo leo.

3.     Kufanya ‘Ibaadah inavyotakiwa.

4.     Kuacha ada na desturi mbaya na maasiya.

 

Allaah Aliyetukuka Ameahidi kila anayemuomba Atamjibu. Hata hivyo, du’aa zetu zinajibiwa kwa njia gani? Mwanachuoni mkubwa Ibn al-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema kuwa tunajibiwa du’aa zetu kwa njia zifuatazo:

 

1.     Kujibiwa uliloomba.

2.     Kubadilishiwa jambo lenye kheri zaidi nawe.

3.     Kucheleweshewa na kupatiwa Pepo Siku ya Qiyaamah.

 

Kisha katika kuomba huhitajiki kufunga siku saba au kuswali Swalatul Haajah na kusoma surah ulizoziandika. Njia hizo hazikupatikana kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye tunahitajika kumfuata.

 

Swalaah Ya Haja haikuthibiti usahihi wake kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na maelezo yake yanapatikana katika kiungo kifuatacho:

 

Je, Swalatul-Haajah Ni Sahiyh Na Ipi Duaa Yake?

 

 

Unachotakiwa kufanya ni pindi unapofunga Sunnah kama Jumatatu au Alkhamiys au siku nyeupe uwe ni mwenye kumuomba Allaah Aliyetukuka kwa utakacho. Na pia uinuke usiku kuswali Swalaah za usiku wa manane na hapo umuombe Allaah Aliyetukuka. Au uwe ni mwenye kuswali Swalaah ya Istikhaarah.  Na hapo bila shaka utajibiwa kwa jinsi ambayo anataka Yeye mwenyewe Allaah Aliyetukuka.

 

 

 

Tafadhali bonyeza viungo vifautavyo upate maelezo zaidi:

 

 

Nisome Duaa Gani Ili Nipate Kibali Cha Kuishi Nchi Ya Kigeni?

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share