Mdaiwa Anafaa Atoe Zakaah?

SWALI:

 

Assalam aleikum warahamtullahi wabarakatu.  Mimi nimfanya kazi nalipwa mshahara kila mwezi, pato langu kwa sasa haliniwezeshi kuweka akiba lakini niko na pesa benki na nimekopesha watu pesa kitambo ambao bado hawajanilipa. Mwaka jana nilipatwa na mkasa ambao ulinitia katika deni kubwa na hospital, ambalo deni hilo ni kubwa hata kama ni wakulilipa kutokamana na mshahara wangu wa mwaka mzima na hizo pesa ninanzo dai watu haziwezi kulilipa deni hilo nililo nalo.

 

Swali langu ni nimewajibika kutowa zakatul maal ama la? Nakama nimewajibika hesabu yangu nafaa niifanye vipi ikiwa kwa mfano mshahara ni $320 kwa mwezi, deni nalo dai ni $1,500 na deni nalo daiwa ni $ 13,000. Kumbuka sina njia nyengine ya income ispokuwa huo mshahara tu.

 

Natarajia jawabu yenu nzuri inshallah.

 

Wabilahi Taufiq

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako kuhusu kudaiwa deni la hospitali na kutaka kujua kiwango chako cha kutoa Zakaah.

Mwanzo inafaa tuelewe kuwa Zakaah kama ‘Ibaadah ina masharti yake ya kutimizwa kabla ya mtu kupaswa kutoa Zakaah. Na mojawapo ya sharti ni kuwa na Nisaab (kiwango cha chini cha akiba uliyonayo), ambacho ni sawa na kununua gramu 82 za dhahabu.

 

Kulingana na hesabu zako ni kuwa kwa sasa wewe wadaiwa takriban $ 11,500. Hivyo huna akiba ya aina yoyote ile kwa ajili hiyo wewe kishari’ah hupaswi kutoa Zakaah bali unatakiwa upewe Zakaah za kukusaidia kulipa deni hilo lako.

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Allaah, na wasafiri. Huu ni waajibu uliofaridhiwa na Allaah” (at-Tawbah [9]: 60).

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akufanyie sahali kulilipa deni hilo kwa haraka iwezekanavyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share