Kurithi Nyumba Iliyojengwa Na Pesa Za Ribaa Inajuzu?

SWALI:

 

Asalaam aleikum.

Kuna mama alofiwa na mumewe, ana watoto wawili wote wafanya kazi benki, naye hataki kutumia pesa zao kwa sababu asema mishahara yao yatokana na riba. Ategemea kodi ya nyumba alorithi kwa mumewe. Mumewe alikua pia akifanya kazi benki, sasa auliza kama pesa ile ya kodi pia ni haramu kwa sababu capital ilotumika kujenga nyumba ile pia imetokana na mshahara wa benki?


 

JIBU: 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu utumiaji wa pesa za ribaa.

 

Hakika ni kuwa haifai kwa Muislamu kutumia pesa za ribaa kujinufaisha yeye mwenyewe kwa njia moja au nyingine. Ama kuhusu nyumba aliyoirithi kutoka kwa mumewe kwake itakuwa halali kwa msingi kuwa yule aliyeinunua ndiye mwenye madhambi lakini mwenye kurithi yeye si makosa yake na maadam kitu chenyewe kilivyo –nayo ni nyumba- ni halali.

 

Madhambi yatakuwa ni yenye kumuangukia aliyenunua si aliyerithi kwa mumewe ambaye ni wajibu wake.

 

Kisichofaa kurithiwa ni kile ambacho chenyewe ni haramu kama vile pombe, nguruwe, mali iliyoibiwa n.k.

 

Hayo ni maoni ya Maulamaa kama Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) kwenye Fatawa zake za Liqa’aat al-Baab il-Maftuuh (1/304).  

 

Hata hivyo, mke huyo ikiwa atakuwa na wasiwasi na hilo na ikiwa atakuwa na njia nyingine ya kuweza kujikimu kimaisha basi itakuwa bora kwani kuacha lenye shaka nao ni msingi mkubwa wa Iymaan. 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Ampatie njia mbadala ya kuweza kuendesha maisha yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share