Sababu Za Kukhitilifiana ‘Aliy na Mu’aawiyah (رضي الله عنهما)

SWALI:

 

ASSALAM ALYKUM.

 

bismi llah rahman rahiim

 

Mimi napenda nipate ufafanuzi wa kutosha kuhusu hatua ya Ally kuamua kumpiga vita Mu'awiyah. Kwani invoonekana Ally ndio aliondoka madina kumfata muawiah. Kwani hiki kitu kinanisumbua sana na kwenye kisa kile mme weka kwa kifupi sana. Assalam alykum.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kutofautiana baina ya ‘Aliy bin Abi Twaalib na Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu ‘anhuma).

Hakika ni kuwa katika kisa hiko cha kutofautiana kwa Maswahaba wawili hao yameongezwa mengi yasiyo ya sawa kwa sababu ya ushabiki.

Na haswa upande wa Mashia wameweka na kuongeza mengi juu suala hilo ili kuonyesha ubaya na uovu wa Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Kabla ya kuingia katika suala hilo tunapenda kurekebisha ibara yako uliyoandika kuwa, “Kwani invoonekana Ally ndio aliondoka madina kumfata muawiah”. Haya maneno si ya sawa kwani ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakutoka kumfuatia Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) bali alitoka kuwazuilia kikundi kilichotoka Makkah baada ya kuuliwa kwa ‘Khalifah ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kilichokuwa kikiongozwa na Mama wa Waumini ‘Aaishah, az-Zubayr na Twalhah (Radhiya Allaahu ‘anhum). Waliotoka Makkah walikuwa wana lengo la kuelekea ‘Iraaq kwenda kulipiza kisasi cha wale waliomuua ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu). Kwa hiyo, ikambidi ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aende kuwazuilia ila shari’ah iwe itachukua mkondo wake kwa vile yeye kama kiongozi awahukumu waliotekeleza tendo hilo.

 

Makundi hayo mawili yalikutana ana kwa ana, na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamtuma mwakilishi wake, Qa‘qaa’ bin ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwenda kuzungumza na uongozi wa upande wa pili. Mazungumzo hayo yalileta natija nzuri na hivyo maharamia ambao walimuua ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) wakaona wachukue fursa ya kuleta vurugu usiku ili watu wa makundi hayo mawili wapigane. Na bila shaka waliweza kufanikiwa na kuleta hasara kubwa katika ummah wa Kiislamu.

 

Tatizo lililotokea baina ya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye ndiye aliyekuwa Khalifah na Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alikuwa liwali wa Shaam kuanzia wakati wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni tatizo la ijtihadi. Kwa muono wa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ilikuwa waliotekeleza uhalifu wachukuliwe hatua kwa taratibu ilhali Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alikuwa na uhusiano wa kidamu na ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa anataka kisasi kichukuliwe mara moja.

Tatizo hilo ndilo lililosababisha makundi hayo mawili kupambana katika uwanja wa Swiffiyn. Hata hivyo, kuogopea kumwaga damu kila mmoja akajizuilia kutoanza mashambulizi na kukawa na mazungumzo ya muda mrefu baina ya wawakilishi wao.

 

Kwa hiyo, tofauti iliyokuwepo baina ya ‘Aliy na Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) niya kiijtihadi na kisiasa na wala sio ya kimadhehebu kama wanavyosema wengine.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share