Kiongozi Wetu Anataka Kujua Amali Zetu Za Kheri Tunazofanya Kila Wiki, Je, Ni Sawa Kumjulisha?

SWALI:

 

Kwenye nyumba ninayokaa kiongozi wetu hutugawiya karatasi tujaze amali tulizo wiki nzima halafu tumrudishie yaani amali zenyewe ni kama kusoma quran, tahajjud, kusoma vitabu vya dini na kadhalika. Sasa swali langu ni kwamba hii inaruhusiwa?


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kujaza karatasi za ‘amali kisha kumrudishia kiongozi.

Hakika ‘Ibaadah na mambo yote ya kheri anafanyiwa Allaah Aliyetukuka pekee kwa nia nzuri na ikhlaaswi. Hivyo si haki kwa mwengine yeyote kujua yale unayoyafanya. Kufanya jambo hilo linaweza kumuingiza mtu katika riyaa. Na ukisha ingia katika riyaa ndio ‘amali zalo zote zimekwenda na kuruka patupu.

 

Tunafikiri huenda kiongozi wenu hakuelewa haswa maana ya karatasi hizo. Karatasi hizo zimefanywa ili kumhimiza mtu kufanya ‘amali za kheri na kujaza yeye mwenyewe ili kujiona anaendelea vipi. Hiyo ni kama kujihesabu kabla hujakwenda kuhesabiwa na Allaah Aliyetukuka siku ya Qiyaamah. Hiyo inatakiwa iwe ni baina yako na Allaah Aliyetukuka sio ya mwengine yeyote kuiona. Kiongozi na nyinyi wenyewe mnaweza kuhimizana kufanya ‘amali njema, lakini sio ‘amali kupitiwa na yeye.

 

Lakini ikiwa huyo kiongozi mumfanya ni kama mlezi wenu wa Dini na anafanya hivyo kuwahimiza katika mambo ya kheri, kama vile mwalimu au Ustaadh au Shaykh anavyoweka mikakati na mpangilio wa kuwasomesha wanafunzi wake, lakini anatakiwa abadilishe utaratibu huo wa makaratasi ambao unamfanya mtu kutangaza ‘amali zake kwa mwanaadam, na kisha pia huenda ikawapelekea baadhi yenu kuwa mnafanya kwa ajili yake au kwa kuogopa na si kwa ajili ya Allaah ambaye Pekee Anastahiki kufanyiwa hayo.

Hivyo, badala ya kuwa anafanya utaratibu kama huo, ni vizuri awe anawapa kazi za kufanya kisha awe anawasikiliza kama mumefanya kazi hizo, mfano, anawapa Surah ya kuhifadhi kwa wiki nzima, na mwisho wa wiki anakuja kuwasikiliza mlivyohifadhi. Na mengine mfano wa hayo. Ama kuhusiana na Swalah hilo ni gumu kulihakikisha isipokuwa ima awe yeye anaswali na nynyi Jama’ah hiyo ya Swalah za usiku, ama kinyume na hivyo basi si vizuri kutangaza ‘amali zenu hizo, isitoshe inaweza kupelekea wengine wakawa wanafanya tu kwa ajili yake, au wakaacha kufana na kumdanganya kuwa wamefanya.

 

Njia nyingine ni kuwafundisha umuhimu wa hizo ‘Ibaadah na kuwaelimisha vizuri na kuwahamasisha hadi wenyewe mjue umuhimu wake na kuzipenda na kuzitekeleza wenyewe kwa sababu ya kujua umuhimu wake kwenu na mbele ya Allaah, na si kwa ajili ya kumfanyia yeye.

 

Kwa hali zozote, inaonyesha huyo Kiongozi wenu ana nia nzuri na malengo mema lakini njia zake ndio sio sahihi. Ni kumuelimisha ajue njia sahihi na abadilishe utaratibu huo.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share