Toba Ya Mkimbizi Mwenye Kuishi Nchi Za Nje Kama Msomali Akiwa Ni Mtanzania

SWALI:

 

Assalam alakum warahmatullah waislamu wenzangu

Naomba kuuliza jee toba yangu itasihi ikiwa mimi sitoacha kabisa kabisa mpaka nitakufa kuiishi kisomali wakati mimi ni mtanzania ndani ya nchi ya uk yaani England.

  


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

La msingi ni kuelewa na kuwa na imani na uhakika bali kuwa na yakini kuwa mwenye kuomba tawbah kikweli kweli na kwa ikhlaas awe amefanya dhambi kubwa kabisa ambalo ni shirk au kuua nafsi bila ya haki; hutakiwa awe na yakini kuwa Allaah humkubalia; na hii ina maana kuwa mja hatakiwi awe na wasiwasi wala shaka katika maombi yake kwa Allaah yawe ya tawbah au mengineyo, kwani ni Allaah pekee Ndie mwenye uwezo wa kusamehe na kukubali maombi ya waja Wake; Allaah Anasema:

Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Allaah na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na nani anayefuta dhambi isipokuwa Allaah? - na wala hawaendelei na waliyoyafanya na hali wanajua.” Aal-‘Imraan: 135.

 

Pia ni vyema kuelewa kuwa miongoni mwa yenye kuonyesha kuwa umetubia ni hii hali ya kuona kuwa umefanya kosa, unajuta unachukia kama hali hii inayosimulia Qur-aan kwa kusema:

“Na pia wale watatu walioachwa nyuma hata dunia wakaiona dhiki juu ya ukunjufu wake, na nafsi zao zikabanika, na wakayakinika kuwa hapana pa kumkimbia Allaah isipokuwa kwake Yeye. Kisha Akawaelekea kwa rehema Yake ili nao waendelee kutubu. Hakika Allaah ndiye Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.” At-Tawbah: 118.

 

Pia ni vyema kama unavyoelewa kuwa tawbah ina masharti yake ambayo yanakwenda sambamba na hiyo tawbah na ukweli wako katika huko kutubia kwenyewe, jambo linalopelekea kusihi kwa tawbah ya mja.

 

Suala muhimu la kuelewa hapa ni kuwa Usomali au Utanzania sio jambo la msingi wala sio muhimu katika tawbah yako, kwani unachotakiwa kuomba tawbah ni kule kusema uongo na hili ndio la kulizingatia; sio Usomali wala Utanzania kwani wengi wanaitwa kuwa ni Watanzania lakini ndani ya nyoyo zao hawakubali hilo isipokuwa ni mazingara yaliyowakuta na hili ni wazi kwa kila mtu.

 

Cha kusisitiza ni kuwa unatakiwa ujute kwa kule kusema uongo na ujaribu kadiri ya uwezo wako kuacha kurejea kusema tena uongo, na kama ikiwezekana kuachana na yote hayo bila ya kujiingiza katika yatayopelekea kujihilikisha; hivyo basi kama unaona kuwa hakuna njia ya kusamehewa na kukubaliwa tawbah yako isipokuwa kwenda serikalini na kuwaeleza kuwa mimi sikuwa Msomali basi fanya hivyo.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

 

Nasaha Kwa Wakimbizi Wanaoishi Kusema Hawajaoana Ili Wapate Ruzuku Ya Serikali

 

Inafaa Kwenda London Kujiripua?

Pesa Alizozichuma Kusema Uongo Azifanye Nini?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share