Nyumba Ya Shangazi Aliyepotea Inatumiwa Na Baba Ameikodisha Pesa Wanagawana, Inafaa?

SWALI:

 

Asalam aleikum. Hilo hapo chini ndo lilikua swali langu.  Samahani sikujua nilitie swali kwenye subject ya urithi au mchanganyiko. Nimelitia kwenye mchanganyiko. Ahsanteni sana.

 

AA, Naomba kuuliza: Shangazi ambae ni baba mmoja na marehem baba alimwachia baba nyumba yake wakati anasafiri na mumewe na watoto wake wakiume wanne zaidi ya miaka 40 liyopita. Tunavofaham alimwachia baba hiyo nyumba kama muangalizi hakumpa iwe yake. Marehem baba alipangisha upande mmoja na mwingine ikawa wanafikia wageni jamaa/ndugu.Kodi alikua anatumia. Toka aondoke shangazi hakuna taarifa yoyote kama yuhai au amefariki yeye wala watoto na mumewe. Tokea afariki baba, sie watoto wake tumekua tunaendeleza alivokua akifanya; upande mmoja anakaa dada yetu; upande mmoja tunapokea kodi tunagawana sawasawa wanawake na wanaume. Walipofariki ndugu zetu watatu tunagawana ndugu waliobakia. Je, tunavofanya ni sawa kisheria ya dini? Je inabidi pia tuwape na vizazi vya ndugu zetu waliofariki? Kama sio sawa, je inabidi tufanye nini kuhusu hiyo nyumba? Je, vizazi wengine wa ndugu wa baba yetu wanayo haki katika nyumba hiyo japokua baba yetu alikufa mwisho? Shukran. M/Mungu Akupeni kila la kheri.Amin


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu amana aliyoachiwa baba na dada yake alipokuwa anaondoka.

Swali hili limeacha mambo mengi hivyo kuleta utata katika kulijibu moja kwa moja. Labda tukiweza kupata mwangaza wa yafuatayo ndipo tutakapoweza kusaidiana:

 

1.     Je, shangazi yenu alimuachia maagizo gani baba yenu?

2.     Je, hakukuwa na mawasiliano kabisa baina ya hao ndugu wawili kwa muda wote huo wa miaka 40.

3.     Je, baba yenu alitumia pesa za ujira wa nyumba kwa msingi gani ikiwa hakukuwa na maagano yoyote?

 

Ikiwa kulikuwa hakuna maagano yoyote kuhusu hiyo nyumba kuhusiana na pesa inayopatikana katika ijara inakuwa si sawa mzazi wenu kutumia yeye peke yake wala nyinyi. Ni ajabu kuwa kwa muda wa miaka yote hiyo nyinyi au baba yenu hajafanya juhudi ya kuwasiliana na shangazi yenu au dada yake. Inabidi kwa sasa mfanye juhudi kupata habari kuhusu kizazi cha shangazi yenu mbali na kuwa muda umepita mwingi.

 

Endapo mtakuwa na khabari ya nchi au mji aliokwenda basi mnaweza kupata usaidizi kwa njia moja au nyengine ya kuweza kupata nambari zao za simu au e-mail na kisha kuwasiliana nao. Fanyeni haraka na ule muda ambao mtakuwa mnatafuta mawasiliano itakuwa haifai kwenu kutumia mali kwani ni haki ya wengineo wala si haki yenu.

 

Nyinyi na watoto wa ‘ami zenu mnaweza kurithi tu ikiwa shangazi yenu hakuwa na kizazi chochote.

 

Ikiwa wapo katika kizazi chake basi nyumba hiyo itakwenda kwao na sio kwenu.

Na likiwa hakutapatikana mawasiliano ya huyo shangazi yenu, haki ya kupata chochote kutoka kwa ijara ya nyumba itakuwa si yenu peke yenu, bali itakuwa ya wote wanaomhusu katika urithi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share