Amekubali Posa Ya Muislamu Aliyeshika Dini, Lakini Sasa Anataka Kuolewa Na Aliyesilimu Akikhofu Atapotea Asipomkubali

SWALI:

Asalam aleikum, swali langu ni hili. Mimi nimeposwa na nimekubali posa hii kwakuwa huyo kijana anajua dini kuliko huyu niliyempenda. Kijana niliye mpenda amesilimu na kwao si waislamu. Kwa muda sasa naona amebadili tabia yeke nakuwa kijana mwema, amejua dini vizuri na anifuata kwa kadri ya uwezo wake inshaallah.

Swali ni kwamba naweza vunja posa yangu kwa yule kijana wakwanza ili niolewe na huyu kwani nampenda na nnahofu nikimwacha atakua ni mwenye kupotea. Wa aleikum salaam.


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kubadili mawazo na kutaka kuolewa na mwanamme mwengine baada ya kumkubali wa mwanzo.

Ni hakika isiyopingika kuwa mapenzi na huruma ya kikweli baina ya wanandoa yanapatikana tu baada ya kuoana na sio kabla.

Mnaweza kudanganyana kuwa mnapendana lakini uhakika wake unanidhiri tu baada ya kuingia katika uanandoa. Na hilo ndilo Alilotuarifu Allaah Aliyetukuka katika Suratur Ruum (30): Aayah ya 21.

“Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.” (Ar-Ruum (30): 21)

Mwanaadamu kwa ujumla wake na haswa Muislamu ni mtu mwenye kutarajia mema na mazuri kwa kiasi kikubwa. Huwa hana khofu kwa sababu yote yanayotokea yameandikwa na Allaah Aliyetukuka Aliye mjuzi wa yote yaliyotokea, yanayotokea na yatakayotokea. Sasa Muislamu huwa hana wasiwasi wa lolote. Yeye anafanya juhudi kwa atakayo kuyafanya na mengine humuachia Allaah Aliyetukuka kutia tawfiki Yake. Kwa hivyo, usiwe na khofu na aliyesilimu, yeye ikiwa anaitaka Dini hii kweli anaweza kupambana na mitihani mwisho ataivuka, atapata mke ampendaye yeye siye anayependwa naye.

Ama ukija katika shari’ah hakuna wasiwasi kuwa mwanamke anaweza kuivunja posa ya mwanamme aliyemposa kwa sababu moja au nyengine. Na ikiwa mwanamme ametoa mahari kwa ajili ya mke mtarajiwa basi mke anatakiwa ailipe au kurudisha mahari hayo ili yeye ajiondoe na mume asiwe ni mwenye kupata hasara.

Hata hivyo, ikiwa kijana mwema amekuja kukuposa kwa njia ya sawa inayotakiwa na Dini ya Uislamu ni vyema wewe baada ya kukubali uwe utatimiza hiyo ahadi kwani kukataa baada ya kukubali, na sio kukataa kuwa kijana hakushika Dini kunaweza kumvunja moyo asiwe ni mwenye kutaka tena kuoa baada ya kupata hayo.

Nasaha ambayo tunaweza kukupa ni wewe ufikirie sana kuhusu suala hilo na kabla ya kufikia uamuzi wowote, fanya yafuatayo:

 

1.   Swali Swalaah ya Istikhaarah, kwani hatokhasirika mwenye kumshauri Allaah Aliyetukuka.

 

2.   Shauriana na watu wa nyumbani kwako, kama wazazi, dada na marafiki wa karibu wenye kukutakia kheri.

 

Ule uamuzi utakaochukua mtegemee Allaah Aliyetukuka nasi tunakuombea kila la kheri na fanaka katika Dini na dunia yako.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share