Msichana Niliyekuwa Simpendi Ameachwa Sasa Nampenda Na Huku Nimeposa Kwengine – Naogopa Kuwajulisha Wazazi Nifanyeje?

SWALI:

 

Assalam alekum, suali langu ni hili nilikuwa na msichana amenipenda sana kisha akamua kuolewa ili anisahau kwani nilikuwa simpendi lakini baada ya miaka miwili tukaonana tena alikuwa amewachwa na ana mtoto mmoja sasa amenigusa moyo wangu nanimeposa naniliye mposa ananipenda kweli lakini mahaba yake yamenitoka kuanzia nimuone huyo mwengine na naogopa kuwaambia wazee wangu naogopa kutukanwa je nifanyeje? Nataka msaada wenu masheikh 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumpenda uliyekuwa humpendi na huku umeposa kwingine. Ndugu yetu mpendwa inaonekana unajichang’anya bila ya kuwepo na haja. Huu ni wasiwasi ambao mwanadamu anatiwa na shetani ili kuvunja aliyoyadhamiria mwanadamu kufanya.

 

Kwa hali hiyo unatakiwa ufikirie sana kwani huenda ukajiwa na mushkeli mkubwa kwa muda mfupi. Hiyo ni kuwa huenda ukakutana na mwingine akakuingia katika roho ukataka kumuoa huyo. Haya ndio maumbile ya mwanadamu kwani jana huyu msichana aliyekuwa akikupenda nawe humpendi sasa amekuingia rohoni wakati tayari umeposa ili kujenga familia yako mpya. Mahaba yanaingia na kutoka wakati mmoja au mwingine na kwa sababu moja au nyingine kwa sababu ya kushawishiwa kiakili jambo ambalo halifai kwani ukiendelea hivyo utajikuta pabaya sana.

 

Hutajutueleza huyu mwanamke aliyekuwa akikupenda nawe humpendi amekugusa kwa kuwa ameachwa au kwa kuwa ana mtoto. Inatakiwa utizame usije ukamgusa mwingine kwa kuwa tayari umemposa ukawa unataka kujenga sehemu moja na kubomoa kwingine.

 

Jambo ambalo tunaweza kukushauri ni ujitulize na uanze kuangalia kila upande ili chochote utakachoamua kitakuwa ni chenye maslahi kwako, wazazi wako, mke wako utakaye mchagua na jamii kwa jumla. Kabla ya kutoa maamuzi ya aina yoyote yale tungekushauri uswali Swalaah ya Istikhaarah ili umtake ushauri Allaah Aliyetukuka, na hakuna ushauri baada ya ushauri wake.

 

Na Allaah anajua zaidi.

 

 

Share