'Aqiydah Ya Imaam Sufyaan Ath-Thawriy (97H - 161H)

‘Aqiydah Ya Imaam Sufyaan Ath-Thawriy (97H-161H)

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Isnaad  Ya ‘Aqiydah Hii

 

 

1-Muhammad bin ‘Abdir-Rahmaan bin al-’Abbaas bin Abdir-Rahmaan Abu Twahiyr Al-Baghdadiy Al-Mukhallas. Ni Shaykh, na Muhaddith, ni mwandamizi na mkweli. Khatwiyb alisema: ‘Ni mwaminifu.’ Adh-Dhahabiy amesema: ‘Hii (‘Aqiydah) imehakikishwa kutoka kwa Sufyaan na Shaykh al-Mukhallas ni mwaminifu (Allaah Awarehemu wote)’ [Tadhkiratul-Huffaadh, 1/206- 207].

 

 

Alizaliwa Shawwal mwaka wa 305H na alifariki katika Ramadhaan mwaka wa 393H. [Adh-Dhahabiy, Siyar A’laam an-Nubalaa, 16/478-480; Taarikh Baghdaad, 2/322-323; Shadharaatudh-Dhahab, 3/144]

 

 

2-Shu’ayb bin Muhammad bin Rajiyan. Adh-Dhahabiy alimtangaza kuwa ni mtu mwaminifu. [Tadhkirah, 1/207]

 

 

3–‘Aliy bin Harb al-Mawsiliy, Abul-Hasan: Imaam, na Muhaddith, mwenye kuaminika na mjuzi. Alizaliwa katika mwaka wa 175H. Abu Hatiym amesema: ‘Ni mkweli.’ Daraqutniy alisema: ‘Ni mwenye kuaminika’. Alifariki katika mwaka 265H [Adh-Dhahabiy, Siyar A’laam an-Nubalaa, 12/251-253, al-Jarh wat-Ta’diyl, 6/183, Taariykh Baghdaad, 11/418-420; Twabaqaat al-Hanabilah, 1/223; Shadharaatudh-Dhahab, 2/150]

 

 

4-Shu’ayb bin Harb: Imaam, kiigizo bora, mcha Mungu, ni Shaykh wa Uislamu, Abu Swaalih al-Mada’ini. An-Nasaaiy amesema: ‘Muaminifu.’, Na Ibn Ma’iyn na Abu Haatim wamesema: “Mkweli na mwenye kuaminika” Alifariki katika mwaka wa 196H inasemekana pia katika mwaka wa 197H (Allaah Amrehemu). [Adh-Dhahabiy, As-Siyar, 9/188-191; Twabaqaat Ibn Sa’ad, 7/320, al-Jarh, 4/342, Al-Miyzaan, 2/275; Tahdhiyb at-Tahdhiyb, 4/350; Shadharaatudh-Dhahab, 1/349]

 

 

 

Matini (Maandiko) Ya ‘Aqiydah Hii

 

Muhammad bin ‘Abdir-Rahmaan bin al-’Abbaas alitueleza akisema: ‘Abul-Fadhwl bin Muhammad bin Shu’ayb Rajiyaan amesema: ‘Aliy bin Harb al-Mawsiliy alituhadithia - katika mwaka wa 257H- akisema: ‘Mimi nimemsikia Shu’ayb bin Harb akisema:

 

 

Nilimwambia Abu ‘Abdillaah Sufyaan bin Sa’iyd ath-Thawriy: ‘Nisimulie Hadiyth kutoka katika Sunnah ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atanifaidisha nayo, ili wakati nitasimama mbele ya Allaah (Jalla Jalaaluh) na Akaniuliza kuhusiana nayo (hiyo Hadiyth), Akisema: ‘Kutoka wapi umepata hii Hadiyth?

 

 

Mimi nitasema: ‘Ee Rabb wangu, Sufyaan ath-Thawriy ndiye aliyenisimulia Hadiyth hii na mimi niliichukua kutoka kwake. Hivyo basi mimi nitaokolewa na (kisha) wewe uulizwe hiyo Hadiyth.

 

Hivyo Sufyaan akasema: ‘‘Ee Shu’ayb, ama kweli hii ni dhamana na dhamana gani kama hii?

 

Andika:

 

 بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Allaah, Mwingi wa Rahmah Mwenye Kurehemu.

 

 

Qur-aan ni maneno ya Allaah. Haikuumbwa. Ni asili kutoka Kwake na Kwake Yeye ndiko itarudi. Yeyote yule asemae zaidi ya haya ni kafiri.

 

 

Na Iymaan (ya Muislamu) inasadikishwa kwa maneno, matendo na Niyyah. Inaongezeka na kupungua. Inaongezeka kwa vitendo vya utiifu na inapungua kwa matendo ya maovu. Hakuna maneno yanayokubaliwa ila mpaka yaambatane na vitendo, na hakuna vitendo vinavyokubaliwa ila mpaka viambatane na Niyyah (nzuri), na hakuna Niyyah ispokuwa ikiwa itaafikiana na Sunnah.

 

 

Shu’ayb akasema: ‘Ee Abu ‘Abdillaah, ni kipi kiafikianacho na Sunnah?

Akasema: ‘Kuwapa kipaumbele Mashaykh wawili: Abu Bakr na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa).

 

 

Ee Shu’ayb uliyoandika hayatokuwa na faida kwako mpaka umuweke ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mbele ya wale waliokuja baada yao.

 

Ee Shu’ayb bin Harb, uliyoandika mwenyewe hayatokuwa na faida kwako mpaka ushuhudie kwa watu wote kwamba wao ni wa Peponi au motoni, wameokolewa watu kumi kutokana na ambavyo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoshuhudia, na wote ni kutoka kabila la Quraysh.

 

 

Ee Shu’ayb bin Harb, uliyoandika mwenyewe hayatokuwa na faida kwako mpaka ushikilie kwamba kupangusa juu ya khuffayn (soksi za ngozi) ni bora kwako kuliko kuzivua wakati unaosha miguu.

 

 

Ee Shu’ayb uliyoandika hayatokuwa na faida kwako mpaka uwe ni mwenye kusema

 

 بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

BismiLlaahi Rahmaaniyr-Rahiym” kimya (kwa sauti hafifu) katika Swalaah, kufanya hivyo ni bora zaidi kwako kuliko kuisema kwa sauti.

 

 

Ee Shu’ayb bin Harb, uliyoandika hayatokuwa na faida kwako mpaka uwe mwenye kuamini Qadar (Matakwa ya Allaah), mema na mabaya, matamu yake na machungu yake. Yote (yatayokukuta) ni kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

 

Ee Shu’ayb bin Harb, Ninaapa kwa Allaah wasemayo Qadariyyah siyo kabisa Asemayo Allaah, au wasemayo Malaika, au wasemayo Rusuli, au wasemayo watu wa Peponi na wa Motoni, au asemayo ndugu yao (Qadariyyah), Ibliys (Allaah Amlaani).

 

Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema:

 

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّـهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَن يَهْدِيهِ مِن بَعْدِ اللَّـهِ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ﴿٢٣﴾

Je, umemuona yule aliyejichukulia hawaa zake kuwa ndio mwabudiwa wake, na Allaah Akampotoa juu ya kuwa na elimu na Akapiga mhuri juu ya masikio yake na moyo wake; na Akaweka kifuniko juu ya macho yake? Basi nani atamuongoa baada ya Allaah? Je, basi hamkumbuki? [Al-Jaathiyah: 23]

 

 

Na (Jalla Jalaaluh) Anasema tena:

 

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٢٩﴾

Na hamtotaka isipokuwa Atake Allaah Rabb wa walimwengu. [At-Takwiyr: 29]

 

 

Na Malaika walisema:

 

قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٣٢﴾

Wakasema: Utakasifu ni Wako hatuna elimu isipokuwa Uliyotufunza; hakika Wewe Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Baqarah: 32]

 

 

Na Muwsaa (‘Alayhis-salaam) alisema:

 

تُضِلُّ بِهَا مَن تَشَاءُ وَتَهْدِي مَن تَشَاءُ ۖ 

Unampotoa kwayo Umtakaye, na Unamuongoa Umtakaye. [Al-A’araaf: 155]

 

 

Na Nuwh (‘Alayhis Salaam) alisema:

 

وَلَا يَنفَعُكُمْ نُصْحِي إِنْ أَرَدتُّ أَنْ أَنصَحَ لَكُمْ إِن كَانَ اللَّـهُ يُرِيدُ أَن يُغْوِيَكُمْ ۚ هُوَ رَبُّكُمْ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٣٤﴾

Na wala haitokufaeni nasaha yangu nikitaka kukunasihini ikiwa Allaah Anataka kukuacheni kupotea. Yeye ndio Rabb wenu, na Kwake mtarejeshwa. [Huwd: 34]

 

 

Na Shu’ayb (‘Alayhis-salaam) alisema:

 

  وَمَا يَكُونُ لَنَا أَن نَّعُودَ فِيهَا إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّنَا ۚ وَسِعَ رَبُّنَا كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا ۚ.. ﴿٨٩﴾

Na haiwi kwetu kureja humo isipokuwa Akitaka Allaah Rabb wetu. Rabb wetu Amekienea kila kitu kwa ujuzi. [Al-A’araaf: 89]

 

 

Na watu wa Peponi watasema:

 

 الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي هَدَانَا لِهَـٰذَا وَمَا كُنَّا لِنَهْتَدِيَ لَوْلَا أَنْ هَدَانَا اللَّـهُ ۖ  ﴿٤٣﴾

AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Ametuongoza kwa haya; na hatukuwa wenye kuhidika kama Allaah Asingetuongoza.  [Al-A’raaf: 43]

 

 

Na watu wa Motoni watasema:

 

رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ ﴿١٠٦﴾

Rabb wetu! Imetughilibu ufedhuli wetu, na tulikuwa watu waliopotea. [Muuminuwn: 106]

 

 

Na ndugu yao, Ibliys akasema:

 

رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٣٩﴾

Rabb wangu! Kwa vile Umenihukumia kupotoka basi bila shaka nitawapambia (maasi) katika ardhi na nitawapotoa wote. [Al-Hijr: 39]

 

 

Ee Shu’ayb, uliyoandika hayatokuwa na faida kwako mpaka ushikilie kuwa: Swalaah inaswaliwa nyuma ya kila mtu mwema au mtu mwenye dhambi; ushikilie kuwa Jihaad itakuwepo mpaka siku ya Qiyaamah; ushikilie kuwa uvumilivu ni kitu muhimu sana chini ya bendera ya (yaani chini ya uongozi) wa mtawala sawa akiwa ni mtu dhalimu au mwema.

 

 

Shu’ayb akasema: ‘Kwa hiyo nikamwambia Sufyaan: Ee Abu Abu ‘Abdillaah, ni katika Swalaah zote?

 

 

Akasema:

‘Hapana, ni Swalaah ya Ijumaa na Swalaah ya ‘Iyd mbili. Swali Swalaah hizi nyuma ya mtu yeyote utakayemkuta. Lakini katika Swalaah zingine zote (yaani za faradhi) uko na hiari katika jambo hilo. Usiswali nyuma ya yeyote ila tu yule ambaye unamuamini na ambaye unamjua vizuri ni katika Ahlus-Sunnah Wal Jama’aah.

 

 

Ee Shu’ayb bin Harb, wakati utakaposimama mbele ya Allaah (‘Azza wa Jalla) na Akakuuliza juu ya hii Hadiyth, basi sema:

 

 

‘Rabb wangu, Sufyaan bin Sa’iyd ath-Thawriy ndiye aliyenihadithia hii Hadiyth, kisha mimi nitajenga urafiki kati yangu mimi na Rabb wangu. [al-Lalika’iy, Sharh Uswuulil-I’tiqaad Ahlis-Sunnah Wal Jama’ah, 1/151-154. Adh-Dhahabiy, Tadhkiratul-Huffaadh, 1/206-207]

 

 

 

Tanbihi

 

1-Imaam Atw-Twabariy alisema:

 

“Qur-aan ni maneno ya Allaah na Tanziyl yake (yaani Wahyi Wake), haikuumbwa katika hali yoyote; inaweza kuwa imeandikwa au wakati ilipokuwa ikisomwa, katika mahali popote inaposomwa, kama jinsi ilivyopatikana katika mbingu au juu ya ardhi, hata hivyo inaweza kuwa imehifadhiwa kama ilivyoandikwa katika Lawhul-Mahfuwdhw au katika nakala za watoto wa shule za Qur-aan, au ilipoandikwa juu ya jiwe na kuandikwa juu ya karatasi au majani, kama kuihifadhi katika moyo, au kusemwa na ulimi. Yeyote yule atakayesema kinyume na haya, au akadai kuwa Qur-aan ambayo tunaisoma na ndimi zetu, na ambayo tumeandika katika Mswahafu, au ambaye ataamini katika moyo wake au ambaye ataficha aina ya iymaan  kama hiyo katika moyo wake, au ambaye atakiri kwa ulimi wake, basi yeye ni kafiri ambaye damu na mali yake ni halali na ambaye atakuwa mbali na Allaah na Allaah yuko mbali naye.” [Atw-Twabariy, Sarihus-Sunnah, 24-25].

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kasema (kuhusiana na Aayah):

 

قُرْآنًا عَرَبِيًّا غَيْرَ ذِي عِوَجٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿٢٨﴾

Qur-aan ya Kiarabu isiyokuwa kombo ili wapate kuwa na taqwa. [Az-Zumar: 28]: “Haikuumbwa”. (Sharh Uswuulil-I’tiqaad, 2/217)

 

 

Al-Laalikaiy alisema:

‘Sa’iyd bin Naswiyr alisema: “Nilimsikia Ibn Uyaynah akisema: Nini ambacho huyu dawih (Bishr al-Marisi) anachosema ‘Ee Abu Muhammad bin Abu Imraan, (anasema) Qur-aan imeumbwa?: Akajibu: amedanganya. Allaah (‘Azza Wa Jalla) Anasema:

 

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ 

Tanabahi! Uumbaji ni Wake Pekee na kupitisha amri.  [Al-A’raaf:54)

 

Kwa hiyo “viumbe” ni uumbaji wa Allaah, na amri ndiyo Qur-aan.

 

 

Na Imaam Ahmad bin Hanbal na Nu’aym bin Hammaad, Muhammad bin Yahyaa ad-Dihli, ‘Abdus-Salaam ‘Aaswim bin ar-Raaziy, Ahmad bin Sin’aan al-Waasitwiy na Abu Haatim ar-Raaziy wamesema vivyo hivyo.” [Sharh Uswuulil-I’tiqaad 2/219]

 

 

‘Aliy bin al-Hasan al-Haashimiy alisema:

“Mjomba wangu alinihadithia: Nilimsikia Waki bin al-Jarrah akisema: Mtu yeyote atakaedai kuwa Qur-aan imeumbwa basi atakuwa amedai kuwa kitu kutoka kwa Allaah kimeumbwa. Hivyo nikamwambia:

 

 

Ee Abu Sufyaan, unasemaje hili? Akasema: “Kwa sababu Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema:

 

وَلَـٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي

Lakini imethibiti kauli kutoka Kwangu.. [As-Sajdah: 13].

 

 

Hakuna kitu cha Allaah ambacho kimeumbwa” [Sharh Uswuulil-I’tiqaad 2/219] Habari zaidi kuhusu mada hii inaweza kupatikana kutoka katika vitabu hivi:

 

 

As-Sunnah cha Imaam ‘Abdullaah, 2/18; Sharh Uswuulil-I’tiqaad, 2/216, 3/378-385; Sarihus-Sunnah cha Imaam Atw-Twabariy,, 24-29; Al-Hujjah cha Asbahaaniy,, 1/334-359, 2/198; Ash-Shari’ah cha Al-Ajuwriy, 75-96, al-Asmaa was-Swifaat cha Al-Bayhaqiy, 1/299- 422; Sharhu Atw-Twahaawiyyah, 107-127.
 

 

 

2-Iymaan inajumuishwa na maneno na vitendo na kupungua na kuongezeka kwake ni moja ya mambo ambayo ummah umekubaliana kwalo. [Atw-Twabariy, Sarihus-Sunnah, 42-45; Al-Ajuwriy, Ash-Shariy’ah, 103-118; Ibn Abi ‘Aaswim, As-Sunnah, 449-451; Al-Laalikaiy, Sharh Uswuwlil-I’tiqaad, 4/830, 5/890-964, Al-Bayhaqiy, al-I’tiqaad, 174-185)

 

 

3-Ummah umekubaliana kuwa mbora zaidi katika Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni Asw-Swiyddiyq, Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kisha Al-Faaruwq, ‘Umar bin al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kisha Dhun-Nuwrayn (mwenye nuru mbili); ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kisha Amiyrul Mu-uminiyn, na Imaamul Muttaqiyn, ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu). [Atw-Twabariy, Sarihus-Sunnah, 38-39).

 

 

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Kwa kuendelea, Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kisha ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kisha ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) haya ni mashauri walikubaliana Wanavyuoni wote wa Waislamu na miongoni mwa wale viongozi katika elimu na Dini miongoni mwa Swahaba, Taabi’iyn, kisha waliokuja baada yao... na Imaam Maalik amenukuliwa na Ijmaa’ (makubaliano) ya watu wa Madiynah juu ya suala hili akisema: “Sijakutana na mtu yeyote miongoni mwa wale wengine ambao wanaongoza wenyewe wakiwa na mashaka juu ya uongozi wa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu).” [Majmuu’ al-Fataawaa, / 421-428), Ibn Hajar, Fat-hul-Baariy, 7/16; Al-Laalikaiy, Sharh Uswuulil-I’tiqaad, 7/1363-1372)

 

 

4-Ibn Abil-‘Izz (Aliyefariki 792H) amesema:

“Hatusemi juu ya mtu yeyote maalum miongoni mwa watu wa Qiblah kuwa yeye ni mtu wa Peponi au wa Motoni, isipokuwa yule ambaye mkweli mwaminifu (wa Allaah) katueleza juu yao, kwamba ni miongoni mwa watu wa Peponi, kama vile wale kumi waliobashiriwa Jannah (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Na kama tutasema: Yeyote ambaye Allaah Atamuingiza Motoni miongoni mwa watu ambao walitenda madhambi makubwa atakuwa anastahiki kuingia huo Moto, na kwamba atatolewa nje ya Moto ikiwa atakuwa miongoni mwa wale ambao wanastahiki kuombewa Shafaa’h, basi tunasimamia kwa kutosema ni mtu maalum. Hivyo hatuna ushahidi wa yeye kama ataingia Peponi, wala kama ataingia Motoni ila tu kutokana na dalili kwa sababu ukweli wa mambo umefichikana na anachofia mtu hakijulikani na yeyote kati yetu.

 

 

Hata hivyo tuna matumaini mazuri kwa wale waliofanya matendo mazuri na tunakuwa na hofu kwa wale waliofanya maovu. Na Salaf (Wema waliotangulia) walikuwa na kauli tatu katika suala la kushuhudia Jannah kwa mtu fulani: Kauli ya kwanza ni kwamba Jannah haishuhudiwi na mtu yeyote isipokuwa Rusuli, na imenukuliwa kutoka kwa Muhammad bin al-Hanafiyyah na al-Awzaa’iy.

 

 

Kauli ya pili ni kwamba Jannah inashuhudiwa kwa kila Muumini ambaye maandiko yametajwa juu yake, na hii ni kauli ya Wanavyuoni wengi na Ahlul Hadiyth (watu wa Hadiyth).

 

 

Kauli ya tatu ni kwamba Jannah inashuhudiwa juu ya (wote) na ambaye waumini wameshuhudia juu yake kwa hilo (Sharh ‘Aqiydatit-Twahaawiyyah, 378)

 

 

5-Nao ni: Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Twalhah bin ‘UbaydiLlaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu),  Az-Zubayr bin Al-Awwaam (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Sa’ad bin Abi Waqqaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Zayd bin Sa’iyd bin ‘Amr bin Nufayl (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Abu ‘Ubaydah bin al-Jarraah (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

6-Sunnah ya kufuta juu ya khufu (soksi za ngozi) wakati wa kuosha miguu imekuja kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mapokezi mengi (mutawaatir).

 

 

Raafidhah (Mashia) wanapinga hii Sunnah iliyo Mutawaatir. Kwa hiyo tunawaambia: ‘Wale ambao walisimulia Wudhuu kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maneno na matendo na wale ambao wamejifunza Wudhuu kutoka kwake, wakafanya Wudhuu kipindi cha maisha yake na akawaona wafanyavyo na kuwasadikisha kwa hilo. Kisha wakasimulia hili kwa wale waliokuja baada yao, kwa idadi kubwa zaidi kuliko wale waliosimulia mapokezi haya, kwa sababu Waislamu wote walifanya Wudhuu wakati wa maisha yake na hawakujifunza Wudhuu isipokuwa kutoka kwake (Nabiy) na kitendo hichi hakikufungamana nao wakati wa zama za Ujahiliya - na walimuona akifanya Wudhuu mara kadhaa ambayo hakuna yeyote ila Allaah (Jalla Jalaaluh) ndiye anaweza kuhesabia.

 

 

Na pia walisimulia kutoka kwake uoshaji wa miguu miwili katika kila kitu ambacho Allaah Anapenda miongoni mwa Hadiyth” [Sharhu At-Twahaawiyyah, 386-387]
 

 

 

7-Hili ni moja ya masuala madogo ya utekelezaji na tofauti imetokea kwa heshima na ni miongoni mwa Wanavyuoni wa Ummah. Hili latokana na ripoti za yanayokinzana ambazo zipo kuhusiana nayo. Na hata kama Isnaad ya kusema

 

 بِسْمِ اللَّـهِ  

BismiLlaah...’ kimya ni sahihi zaidi, bado ni kunabaki moja ya matatizo ambayo hayashikamani na ‘Aqiydah. [Sharhus-Sunnah, 3/54; Fathul-Baariy, 2/226-229]
 

 

 

 

8-Al-Qadar ni elimu (ujuzi) wa Allaah wa tangu hapo kabla ya ambayo yatayotokea kutoka miongoni mwa matendo ya waja Wake, nini watachochuma, na kuibuka kwa vitendo hivyo kutokana na Alichoamrisha, ametakasika yeye kutokana na kutokamilika, na viumbe Wake ndiyo hawakukamilika, mema na mabaya yao. Hivyo, Qadar ni kitu ambacho kwa ajili ya mambo manne kimethibitishwa: Jambo la kwanza ni kutokana na elimu ya Allaah juu ya mambo kabla ya hayajatokea. Jambo la pili ni kutokana na maandiko ya (elimu hio). Jambo la tatu ni kuwa hakuna jambo laweza kutokea au laweza kuja katika kuwepo ila ni kutokana na matakwa Yake, hivyo basi chochote akitakacho hutokea na chochote Asichokitaka hakitokei. Jambo lanne ni kuwa uumbaji wa Allaah – mkamilifu ni Yeye kutokana na upungufu wa matendo na kuwaleta kwake katika kuwepo.

[Sharh Uswuulil-I’tiqaad, 3/534, Al-Bayhaqiy, Al-I’tiqaad, 132; Ajuwriy, Ash-Shariy’ah, 149-168; Atw-Twabariy, Sarihus-Sunnah, 34-36; Al-Bukhaariy, Ar-Radd ‘Alal-Jahmiyyah, 39-42; Majmuu’ Al-Fataawaa, 2/152, 8/484-488; Sharhut-Twahaawiyyah,383-399].

 

 

9-Imaam Atw-Twahaawiy alisema:

“Tunashikilia ya kuwa Swalaah nyuma kila mtu mwenye mwema na hata mwenye dhambi kutoka katika watu wa Qiblah (Waislamu), na pia kuwaswalia miongoni mwao wanaokufa.”

 

 

Kisha mfafanuzi wa hii ‘Aqiydah, Ibn Abi Al-‘Izz kasema: “Jua - (Allaah Akurehemu), kwamba inaruhusiwa kwa mtu kuswali nyuma ya mtu ambaye ana uzushi wa ufasiki (fisq) inayojulikana kwa makubaliano ya Wanavyuoni. Na si miongoni mwa masharti ya kumfuata Imaam, na haifai mtu kumchunguza Imaam na kumuuliza haswa:

 

 

“Nini unachoamini? Badala yake, ataswali nyuma ya mtu ambaye msimamo wake haujulikani. Na hili (inatumika) hata kama atabidi kuswali nyuma ya mtu wa Bid’ah ambaye analingania na kuita watu katika hizo Bid’ah zake au faasiq anayetenda madhambi yake wazi na ambaye ni Imaam kateuliwa hapo haitokuwa rukhsa kuswali nyuma yake, ispokuwa tu kama atakuwa ni Imaam wa Swalaah ya Ijumaa, Swalaah ya ‘Iyd mbili na Swalaah wakati wa Hajj katika ‘Arafah na Swalaah mfano wake. Maamuma wataswali nyuma yake na hii ndiyo mtazamo wa jumla wa Salaf na wa Makhalaf (Wanavyuoni waliotangulia na waliofuatia). Na mtu yeyote atakayeacha kuswali Swalaah ya Ijumaa nyuma ya Imaam ambaye ni mfanya madhambi huyu ni mzushi katika mtazamo wa Wanavyuoni wengi. Na ni sahihi kuwa ataswali pamoja na Imaam na kwamba hatokuwa na haja ya kuzirudia, kwa sababu Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakiswali Swalaah ya Ijumaa na mara kwa mara wakiswali nyuma ya kiongozi mwenye madhambi na walikuwa hawazirudii Swalaah zao.” [Sharhut-Twahaawiyyah, 373-377]

 

 

10–Akizungumzia kuwarudi Maraafidhah (Mashia) kwa kusema kwao:

‘Hakuna Jihaad katika njia ya Allaah mpaka aliyechaguliwa kutoka katika kizazi cha Muhammad atokeze na mlinganiaji kutoka mbinguni anadi: ‘Mfuateni’. Uongo wa maneno haya yako wazi kabisa zaidi na dhahiri yasiyohitaji hata kuelezwa kwa Dalili. [Sharhut-Twahaawiyyah, 387-388]

 

 

11-Habari zaidi kuhusiana na mada hii inaweza kupatikana katika: Sharh Uswuulil-I’tiqaad, 7/1229-1233, Al-Bayhaqiy, Al-I’tiqaad, 242-246; Ibn Abi ‘Aaswim, As-Sunnah, 508-511

 

 

 

 

 

Share