Zingatio: Mja Wa Dirham

 

Zingatio: Mja Wa Dirham

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Watu huamka wakiwa kwenye makundi mawili, kuna wale wanaojaaliwa kuinuka kitandani wakiwa na bendera ya shahaadah, na kuna kundi la pili ambalo wao huinuka kitandani wakiwa na bendera ya Shaytwaan. Hili kundi la pili ndilo lisilojali katu mipaka ya halali na haramu.

 

Hao ndio watu ambao kwao kila kitu ni sawa alimuradi tu kinakidhi matakwa ya nafsi; wala haijamiliki nafsi ya mwanaadamu isipokuwa tu ni yenye kumuamrisha kutenda maovu. Asahau kabisa mwanaadamu kwamba nafsi yake itamuusia kumcha  Rabb kwa kutenganisha baina ya halali na haramu.

 

Kwa masikitiko makubwa, ndugu zetu Waislamu wanawake kwa wanaume, wamekuwa wakiamka vitandani mwao wakiwa na fikra tupu za kutafuta mali tu. Wakisahau kabisa kwamba mali itabaki hapa duniani, na kinachosikitika zaidi ni kwamba, namna utakavyoitafuta mali na utakavyoikusanya, ndivyo uroho, ulafi na uwendawazimu unavyozidi. Mali sio chakula, ya kwamba utakapokula utashiba na ukiendelea kula utakitapika. Mali ipo na uroho wake Muislamu ndio utakaomfanya kuikusanya zaidi na zaidi.

 

Hata hivyo, ni vyema kutofautisha katika makala hii, baina ya yule Muislamu anayeitafuta mali katika njia za halali na yule ambaye hajali mipaka ya halali na haramu. Huyu ndiye yule ambaye sie tu ya kwamba anafakamia mali kwa njia za haramu, bali pia anakosa nidhamu ya kuchunga hata Swalah na Zakaah, na wengine kutovukwa na adabu kwa hata kuzivuruga vuruga haki za wazee, watoto wake, mkewe na wanaadamu wenziwe.

 

Hawa ndio wale ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewazungumzia kuwa ni wenye kupenda ‘mali pendo la kupita kiasi’ hadi inafikia wakati mtu mwenye mali (tajiri) kutowatizama ‘mayatima kwa jicho la huruma’ wala hajihimizi ‘kulisha masikini’. Na baya zaidi ni kwamba mtu huyu hukithiri vitimbi hadi kuwa ni mlaji ‘urithi kwa ulaji wa pupa’. [Al-Fajr: 17-20]

 

Basi kwa yule Muislamu ambaye kwake rushwa ni riziki yake, ribaa ikawa ni tandiko lake, utapeli ndio mazungumzo yake na ulaghai/uongo kuwa nyiradi yake; akumbuke tu kwamba ipo siku pumzi zake zitamuishia wala hiyo mali haitakuwa na uwezo wa kuinunua hata akiwa na nguvu ya kufidia hilo kwa mali za watu wote ulimwenguni.

 

Halikadhalika, na atambuwe Muislamu kwamba kila sumni au senti anayoichuma, itakwenda kuhesabiwa kwa kuulizwa: namna gani ameichuma na namna gani ameitumia. Kadiri mali itakavyokuwa ni nyingi, ndipo hesabu yake Muislamu itakavyochukuwa muda wa hoja za kuzijibia, haswa kwa yule ambaye amechuma kwa njia zisizo halali.

 

Ee Muislamu, ndugu yangu, nakuusia na naiusia nafsi yangu kuacha kabisa kughafilishwa kutafuta wingi wa mali na kujifakharisha nayo. Hata ikafika wakati ambao unaingizwa ndani ya kaburi umekufa kabla ya kufanya khayr yoyote, kwani Rabb Ametuapia kuwa lau kama tungelikuwa ni wenye kuelewa ujuzi wa yakini tusingeliipapia mali kwa pupa. [At-Takaathur: 1-7].

 

Kubwa mno ni kwamba, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ ﴿٨﴾

Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema. [At-Takaathur: 8]

 

 

Share