17-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Subira njema

 

17- Subira Za Maswahaba – Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

 

 

Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa ni mtengenezaji panga alizokuwa akiwauzia watu wa Makkah. Alikuwa ni miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia Uislamu na akapata mateso kwa ajili ya Dini hii tukufu.

 

Makafiri walipotambua kwamba ameingia katika Dini ya Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  wakaanza kumtesa kwa kumvisha nguo ya chuma na kumlaza katika jua kali. Mara nyingi alilazwa katika mchanga wa moto uliombabua mgongo wake. Alichomwa pia kichwa chake kwa chuma cha moto. Makafiri walichukua vyuma walivyovikuta nyumbani kwake, alivyokuwa akitengenezea mapanga, kisha walivitia   katika moto viwake kisha wakamfunga navyo mwilini, miguuni na mikononi kama minyororo. Lakini alivumilia na mateso yalipomzidi, alimuomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amwombee pamoja na Waislamu wengineo waliokuwa matesoni. Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwanasihi wathibitishe iymaan zao katika Dini ya haki na akiwakumbusha fadhila za kusubiri mitihani. 

 

‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipokuwa Khalifa wa Waumini, aliwahi kumuuliza Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kuhusu mateso aliyoyapata kwa ajili ya kuingia Uislamu. Alipomuonyesha mgongo wake, ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu)   alishtuka na kusema: “Sijapatapo kuona kama hivi kabla!” Khabbaab akasema: “Mwili wangu uliburuzwa katika mrundo wa makaa ya moto hadi damu na mafuta yaliokuwa yakitoka mgongoni mwangu yalikuwa yakizima moto wa makaa.”

 

Alikuwa ni miongoni mwa Waumini dhaifu na masikini kama Bilaal na Suhayl  (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ambao makafiri Quraysh walimtaka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  atengane nao. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimteremshia Rasuli Wake Aayah za Qur-aan kumkataza asiwafuate makafiri. Aayah za Qur-aan zikawanyanyua na kuwapa heshima na utukufu na badala yake ikawa ni kuwadhalilisha makafiri:

 

وَلَا تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ مَا عَلَيْكَ مِنْ حِسَابِهِم مِّن شَيْءٍ وَمَا مِنْ حِسَابِكَ عَلَيْهِم مِّن شَيْءٍ فَتَطْرُدَهُمْ فَتَكُونَ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٢﴾

Na wala usiwafukuze wale wanaomwomba Rabb wao asubuhi na jioni wanataka Wajihi Wake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, na wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, hata ukawafukuza; utakuja kuwa miongoni mwa madhalimu.

   

وَكَذَٰلِكَ فَتَنَّا بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لِّيَقُولُوا أَهَـٰؤُلَاءِ مَنَّ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّن بَيْنِنَا ۗ أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِالشَّاكِرِينَ ﴿٥٣﴾

Na hivyo ndivyo Tulivyowafanyia mtihani baadhi yao kwa baadhi ili waseme: “Je, hawa ndio wale Aliowafadhilisha Allaah baina yetu?” Je, kwani Allaah Hajui zaidi wanaoshukuru?

   

وَإِذَا جَاءَكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِنَا فَقُلْ سَلَامٌ عَلَيْكُمْ ۖ كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ۖ أَنَّهُ مَنْ عَمِلَ مِنكُمْ سُوءًا بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابَ مِن بَعْدِهِ وَأَصْلَحَ فَأَنَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥٤﴾

Na wanapokujia wale wanaoamini Aayaat Zetu basi sema: “Salaamun ‘alaykum! Rabb wenu Ameandika juu ya Nafsi Yake rahmah; kwamba yeyote miongoni mwenu atakayetenda ovu kwa ujahili, kisha akatubia baada yake na akatengenea, basi hakika Yeye ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Al-An’aam: 52-54]

 

Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alithibitisha iymaan yake juu ya mateso na adhabu kali. Alishiriki vita vyote pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hadi kufariki kwake. 

 

Hao ni Waislamu wa mwanzo waliotupa mafunzo muhimu ya kuvumilia tabu na mateso kwa ajili ya mapenzi ya Dini yao tukufu. 

 

 

Share