16-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Swabrun Jamily (Subira njema)

 

16- Subira Za Maswahaba – Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu)

 

 

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa mtumwa kabla ya Uislamu. Bwana wake aliyemtumikia alikuwa ni Umayyah bin Khalaf anayetokana na kabila la Al-Jumhiy. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoanza kulingania watu katika Dini ya Kiislamu, Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alifurahishwa na habari alizokuwa akizisikia kutoka kwa Abuu Bakr Asw-Swiddiyq  (Radhwiya Allaahu 'anhu)   ambaye alikuwa akiwalingania waliokuwa huru na watumwa. Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) hakukawia kuingia Usilamu mikononi mwa Abuu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye alimpeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na kuzitamka shahada mbili mbele yake. Akawa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika Uislamu.

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  naye alipata sehemu kubwa ya adhabu, kwani bwana wake Umayyah bin Khalaf alikuwa mtu khabithi sana. Alikuwa akimtoa nje wakati wa jua kali linalounguza mwili akimvua nguo zake kisha akimlaza juu ya mchanga wa jangwani unaounguza. Kisha akimwekea jiwe kubwa sana juu ya kifua chake huku akimwambia: “Utabaki hivyo hivyo mpaka ufe isipokuwa kama utamkanusha Muhammad na kumtukana kisha urudi tena kuiabudu miungu yako Laata na ‘Uzza." Lakini Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)   alikuwa akimjibu kwa kusema: “Ahadun Ahad." (Mmoja tu, mmoja tu) akikusudia Allaah. Alipoulizwa: “Kwa nini unaendelea kusema hivyo ‘Ahadun Ahadun’ na hali unajua kuwa maneno hayo yanawaghadhibisha na kwa ajili hiyo wao wataendelea kukuadhibu?" Akajibu: ”Wa-Allaahi kama ningekuwa nalijua neno jingine linaloweza kuwakasirisha zaidi kuliko hilo, basi ningelilitamka." Na neno hilo ‘Ahadun Ahadun’, lilikuwa likimkera sana Umayyah, na kila alipolisikia alipandwa na ghadahbu akawa anampiga Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kama vile mtu aliyepandwa na kichaa! Lakini juu ya hivyo, Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  aliendelea kuvuta subira huku akitamka neno lake hilo “Ahadun Ahadun” mpaka Umayyah akashindwa.

 

Ikawa kila siku baada ya kumtesa juani, alikuwa akimfunga kamba shingoni kisha akiwakabidhi watoto wadogo na wendawazimu wamburure Bilaal  (Radhwiya Allaahu 'anhu)  na wazunguke naye mjini Makkah, huku wakimzomea na kumpiga. Lakini alikuwa akiendelea kusema: “Ahadun Ahadun.”

 

Hali iliendelea hivyo hadi siku moja Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alimuona Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  katika hali ya mateso hayo, akamwambia Umayyah: "Je, humuogopi Allaah unamtesa namna hii huyu maskini, mpaka lini utaendelea hivi?” Umayyah akamwambia: "Wewe ndiye uliyemharibu huyu, kwa hivyo sasa muokoe wewe kama unaweza." Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)   akamnunua kwa wakia tano kisha akamuacha huru. Kabla ya hapo, Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)   alikuwa keshawanunua watumwa sita na kuwaacha huru, na Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alikuwa wa saba.

 

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)   akaepukana na adhabu, na Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) bila shaka akapata ujira mkubwa kutoka kwa Rabb wake (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)   aliendelea na kazi hiyo ya kuwanunua watumwa na kuwaacha huru. ‘Ulamaa wa tafsiri wamekubaliana kuwa Allaah Alimsifia Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) katika Aayah 17 Suwratul-Layl:  

 

وَسَيُجَنَّبُهَا الْأَتْقَى ﴿١٧﴾

Na ataepushwa nao mwenye taqwa kabisa.

 

الَّذِي يُؤْتِي مَالَهُ يَتَزَكَّىٰ ﴿١٨﴾

Ambaye anatoa mali yake kujitakasa.

 

وَمَا لِأَحَدٍ عِندَهُ مِن نِّعْمَةٍ تُجْزَىٰ ﴿١٩﴾

Na hali hakuna mmoja yeyote aliyemfanyia fadhila yoyote hata amlipe.

 

 

إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٠﴾

Isipokuwa kutaka Wajihi wa Rabb wake Aliyetukuka.

 

 

وَلَسَوْفَ يَرْضَىٰ ﴿٢١﴾

Na bila shaka atakuja kuridhika. [Al-Layl: 17-21]

 

 

 

Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) akaondoka pamoja na Bilaal  (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).  Alipokuwa akiondoka naye, Umayyah akamwambia: "Ondoka naye hapa, Naapa kwa Laata na ‘Uzza, kuwa ungekataa kumnunua kwa wakia tano, basi hata kwa wakia moja tu ningekuuzia!" Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)   akamjibu: “Lau kama ungelitaka nimnunue kwa wakia mia, basi ningelikupa.”

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifurahi kupita kiasi alipomuona Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kawa huru, akawabashiria Waislam juu yake na akamfanya baadaye kuwa ni Muadhini wa mwanzo katika Uislam, kwani Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa na sauti nzuri sana na Allaah Akaijaalia sauti hiyo iwe yenye kuleta taathira ndani ya nyoyo za kila mwenye kuisikia.

 

 

Iymaan ya Bilaal na subira yake imempatia fadhila zifuatazo:

 

1. Kupendwa mno na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  pamoja na Maswahaba zake.

 

2. Kuwa ni Muadhini wa kwanza wa Waislamu na hivyo thawabu za Swalaah za Maswahaba alizibeba yeye pia.

 

3. Alikuwa wa kwanza kuadhini juu Ka’bah, pale baada ya kuukomboa mji wa Makkah, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaka Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) apande juu ya Al-Ka’bah na kuadhini.

 

4. Amebashiriwa Jannah na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kwa kuwa alisikia sauti ya viatu vyake vikiwa mbele yake Peponi. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipomuuliza ((Nielezee juu ya ‘amali njema kabisa unayoitenda, kwani nimesikia sauti ya viatu vyako vikiwa mbele yangu Peponi?)) Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  akajibu: “Ee Rasuli wa Allaah, sijafanya ‘amali yoyote niliyoiona kuwa ni bora kwangu isipokuwa kawaida yangu mimi kila nikitawadha huswali kadiri ninavyojaaliwa kuswali)) Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Hilo ndilo lililokufikisha)) [Al-Bukhaariy]

 

5. Alishiriki katika vita vingi vikiwemo vya Badr na akaweza kumuua aliyekuwa bwana mmiliki wake, Umayyah bin Khalaf ambaye alikuwa akimtesa.

 

6. Alipata heshima kubwa kutoka kwa Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kwani juu ya kuwa daraja yake ilikuwa ni kubwa mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  lakini hakuwa mwenye kiburi wala kujiona wala kutakabari, bali alikuwa mnyenyekevu kwa Waislam wenzake, huku akiichunga nafsi yake.

 

Alifikwa na majonzi makubwa mno alipofariki Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  mpaka akashindwa  kuadhini.

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) alifariki akiwa shahidi kwani alifanya jihaad kwenda Shaam kupigana vita na akakumbwa na maradhi ya tauni yaliyowaua watu wengi sana huko Shaam. Inasemekana kuwa roho yake ilipokuwa ikimtoka, mkewe alikuwa akimwambia: "Huzuni iliyoje, huzuni iliyoje!” Lakini Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa akiyafumbua macho yake akasema: "Bali furaha iliyoje, kesho nitaonana na wapenzi, Muhammad na Maswahaba."

 

 

Share