Zingatio: Simu Misikitini

 

Zingatio: Simu Msikitini

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Miongoni mwa mambo muhimu mno siku ya Qiyaamah ni Swalah, inapotengenea basi matendo yote ya Muislamu yametengenea, na inapokuwa na kasoro basi matendo yote huwa na kasoro. Hivyo, kwa kila Muislamu anayeelewa hili, hutilia maanani sana kuichunga Swalaah yake isije kuharibika.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewataja miongoni mwa wenye kufaulu Muflihuun kuwa ni wale ambao wanakuwa na unyenyekevu khushuu katika Swalaah zao: 

 

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾

Kwa yakini wamefaulu Waumini. Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea. [Al-Muuminuwn: 1-2]

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Swalini kama mulivyoniona mimi nikiswali.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

 

Sasa mbali ya kuwa Waislamu wenyewe haswa wa siku hizi kuacha mafunzo ya hapo juu, yaani kukosa unyenyekevu na kutokufuata maagizo ya kumuiga Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) namna alivyoswali, tunaletewa uzushi na ukiritimba mkubwa ndani ya misikiti na Swalah zetu kupitia matumizi ya simu.

 

 

Hakuna shaka yoyote kwamba matumizi ya simu yameenea kwa kiwango kikubwa, wala hukuna wasiwasi wowote kwamba simu zimekuwa na manufaa makubwa miongoni mwa Waislamu. Lakini, kitendo cha kuweka miziki ndani ya simu na kuifanya simu kulia miziki hiyo hadi kipindi cha Swalah ni haramu iliyo wazi kabisa. (Rudia fatwa iliyopo katika Alhidaaya.com)

 

Iwapo Swalah yako umeiona haina muhimu, basi ni afadhali ukaswali chumbani mwako, sio kuwaletea Waislamu vituko vya miziki ya simu ndani ya Swalaah zao. Tena la kustaajabisha ni kwa juhudi waliyoichukua misikiti kuweka matangazo ya kuzima simu kabla ya kuingia Misikitini. Kinachojitokeza badala yake ni kwamba hizo simu zimekuwa ni muhimu zaidi kuliko Swalaah. Hivyo, inaachwa wazi na kupelekea bughudha ndani ya misikiti.

 

Muislamu leo hii anafikia kiwango cha kujisifu kwamba simu yake imelia Msikitini na kuwafanya Waislamu kucheka. Wengine wana milio ya majibwa, wengine vicheko/vilio vya watoto. Je, Waislamu tumechukua dhamana gani ya hizi Swalaah za Waislamu wenzetu? Tumekaa kulifikiria hilo, ama twatumbukia tu Misikitini bila ya kuzingatia heshima na hadhi ya Swalaah?

 

Na tunawatahadharisha wale wenye kutia miziki ndani ya simu, waache kufanya hivyo mara moja. Iwapo simu italia miziki ndani au nje ya Swalaah, uharamu wake upo sehemu zote mbili, isipokuwa tu dhambi zake za kulia ndani ya Swalaah haswa katika Jama’ah inakuwa ni mara dufu.

 

Kwa kumalizia, kama Muislamu anahisi ni mgumu wa kuizima simu yake, ni afadhali zaidi akaiacha simu nyumbani kwake au sehemu yake ya kazi. Hilo litakuwa ni bora zaidi.

 

Twamuomba Rabb Atujaalie haki tuione tuweze kuifuata na baatwil kuielewa tuweze kuicha – Aamiyn.

 

 

Share