Ziara Ya Madiynah

 

Ziara Ya Madiynah: Hajj

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Ziara ya Madiynah ni jambo linalopendeza sana. Kwa kawaida Mahujaji na wafanyao ‘Umrah huuzuru mji huu mtukufu wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kabla au baada ya kwenda Makkah.

 

Hata hivyo kuna baadhi ya watu wanaojaribu kupunguza umuhimu wa ziara ya mji huu mtukufu kwa kuwaambia watu kwa mfano:

 

“Ukihiji bila ya kwenda Madiynah Hijjah yako inakubaliwa", au

 “Ziara ya Madiynah haihusiki na Hijjah", au

“Haina lazima kwa mwenye kuhiji kwenda Madiynah", n.k.

 

Ingawaje maneno kama hayo ni ya kweli, na kwamba mtu akienda Makkah na kutimiza shughuli za Hijjah bila ya kwenda Madiynah, Hijjah yake huwa imekamilika na haina shaka yoyote na inakubaliwa, lakini maneno hayo yanaleta maana ya kuwakimbiza watu mbali na mji huo mtukufu ambao Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiupenda sana na kuutukuza.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Madiynah ni mji mtukufu kuanzia (jabali) Ayrin mpaka (jabali) Thawr.”

 

Haya ni majabali mawili, mojawapo lipo mwanzo wa Madiynah na la pili lipo mwisho wa Madiynah.

 

Na akasema:

 

“Hakika Ibraahiym ameutukuza mji wa Makkah na akauombea du’aa, na mimi nautukuza mji wa Madiynah kama alivyoutukuza Ibraahiym mji wa Makkah. Rabb wangu mimi naitukuza ardhi (yote ya Madiynah) iliyo baina ya majabali yake (Ayrin na Thawr), usikatwe mti wake na pasitendeke maasi. Atakayetenda maasi katika mji huu, atapata laana ya Allaah na ya Malaika wake na ya watu wote kwa ujumla.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Wakati fulani palikuwa na shida kubwa sana hapo Madiynah na vitu vikapanda bei na kuwa ghali kupita kiasi. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema kuwaambia watu wa Madiynah:

 

“Nakupeni bishara njema. Mimi nimekubarikieni katika vibaba vyenu na katika magao yenu, chakula cha (mtu) mmoja kitawatosha wawili, na cha wawili kitawatosha wanne, watano au sita. Kwa hivyo jikusanyeni katika chakula kwa sababu baraka imo katika mkusanyiko wa jamii. Atakayesubiri katika shida za mji huu (Madiynah) nitamuombea shifaa siku ya Qiyaamah, na atakayeweza kufa katika mji huu, basi afe, kwani mimi nitakuwa mwenye kumuombea shafa’ah siku ya Qiyaamah.” [Imepokewa na Atw-Twabaraaniy]

 

Hii ndiyo sababu iliyomfanya ‘Umar bin al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) apende kuomba du’aa ifuatayo:

 

“Rabb wangu, mimi nakuomba nife shahidi katika njia yako na katika mji wa Nabiy wako (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)”. [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

 

Du’aa zote mbili hizo za ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) zimekubaliwa, maana aliuliwa shahidi akiwa anaswalisha Swalah ya Alfajiri ndani ya Msikiti wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na akazikwa Madiynah tena karibu na kaburi la Sahibu yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Hizi ni baadhi tu ya sifa mbali mbali za mji huu mtukufu ambao Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiupenda sana.

 

Pana kundi jengine ambalo hupindukia mipaka katika kuitukuza ziara ya mji huu mtukufu. Kundi hili huwatuhumu wasiouzuru mji huu mtukufu kuwa wamemuasi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakitegemea Hadiyth zisizo sahihi (Hadiyth Maudhu’i).

 

(Hadiyth Maudhu’i - ni zile ambazo ‘Ulamaa wa fani hii wamezigunduwa kuwa ni Hadiyth zilizopachikwa, zisizo za kweli na hazina asili wala msingi wowote.)

 

Mfano wa Hadiyth wanazozitegemea ni hizi zufuatazo:

 

Wanasema kwamba eti Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Atakayehiji na asinizuru ameshaniasi.” au

“Atakayehiji na akalizuru kaburi langu baada ya kufa kwangu anakuwa mfano wa aliyenizuru nilipokuwa hai”.

 

Zipo Hadiyth nyingi za mfano huu.

 

Ni haramu kumsingizia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uongo, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametoa onyo kali kwa kila anayemsingizia uwongo aliposema:

 

“Atakayenisingizia uongo makusudi, basi keshajitayarishia makazi yake Motoni.”

 

Hapana sababu yoyote ya mtu kutumia hoja kama hizo katika kuithibitisha Ibada ya aina yoyote ile. Isitoshe zipo hoja zenye nguvu kuliko hizo zinazotegemea Hadiyth zilizo sahihi zinazotilia nguvu ziara ya mji huu mtukufu wa Madiynah.

 

Ziara Ya Msikiti:

 

Kwanza kabisa itabidi tusahihishe itikadi yetu kuhusu ziara ya mji huu mtukufu katika kutia niyyah ya Ziara.

 

Nia ya ziara ya Mji wa Madiynah, inatakiwa iwe ni kuuzuru Msikiti wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na isiwe kulizuru kaburi lake, kama wanavyotia nia hiyo baadhi ya watu. Ingawaje kuzuru makaburi kwa niyyah ya kuwaombea maiti na kujikumbusha Aakhirah ni jambo jema, lakini kufunga safari ndefu kwa ajili hiyo haijuzu.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Isifungwe safari ndefu (kwa ajili ya ibada) isipokuwa kwenda katika Misikiti mitatu; Al-Masjidul Haraam (Makkah), na Msikiti wangu huu (Madiynah), na Msikiti wa Ilyaa (Baytul Maqdis).” [Imepokewa na Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na wengineo]

 

Na akasema:

 

“Swalah katika Msikiti wangu ni bora kuliko Swalah elfu katika Misikiti mingine, na Swalah katika Msikiti wa Makkah (Masjidul Haraam) ni bora mara elfu mia kuliko Misikiti mingine.” [Imam Ahmad bin Hanbal]

 

Allaah huumba na kuchagua atakavyo. Ametuchagulia sayari ya ardhi miongoni mwa sayari zote kuwa ni mahali petu pa kuishi, na Akamchagua mwanadamu miongoni mwa viumbe vyote Akamtukuza, kisha Akawachagua Rusuli (‘Alayhim-salaam) miongoni mwa binadamu wote na kuwatukuza, na Akamchagua Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni Imaam wa Rusuli yote, na Akaichagua Misikiti katika ardhi kuwa ni mahali patukufu kupita sehemu zote, kisha Akaichagua Misikiti hii mitatu kuwa ni mitukufu zaidi miongoni mwa Misikiti yote, na Yeye ndiye Anayeumba na kuchagua na sisi jukumu letu ni kufuata tu. Kwa sababu Anayeumba ndiye Mwenye kujua na si aliyeumbwa.

 

Allaah Anasema:

وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَيَخْتَارُ ۗ مَا كَانَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٦٨﴾

Na Rabb wako Anaumba na Anachagua Atakavyo. Haikuwa wao wana khiari yoyote. Subhaana-Allaah Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa kutokana na yale yote wanayomshirikisha. [Al-Qasas: 68]

 

Bustani Katika Bustani Za Jannah:

 

Hapana Hadiyth sahihi isemayo; "Baina ya Kaburi langu na mimbari yangu bustani katika bustani za Jannah." Bali Hadiyth iliyo sahihi ni ile iliyopokelewa na Imam Al-Bukhaariy na Muslim na At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy na Imaam Ahmad inayosema kuwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema, kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Baina ya NYUMBA yangu na Mimbari yangu, bustani katika bustani za Jannah”

 

(Bayna BAYTIY wa mimbariyna sio Bayna Qabriy wa Mimbary).

 

Kwa hivyo itikadi iliyo sahihi ni kutia niyyah ya kuuzuru Msikiti wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na sio kaburi lake, na hii ni kwa sababu unapofika pale kaburini na kumswalia na kumsalimia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wewe na aliyepo popote duniani thawabu zenu ni sawa sawa, maana aliye mbali pia Swalah na Salaam zake zinafikishwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Lakini ulichofaidika wewe ni kule kusali kwako ndani ya Msikiti wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na hasa katika Ar-Rawdhah Ash-Shariyf, na pia unafaidika na ziara yako katika sehemu nyingine takatifu za Madiynah.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Niswalieni, kwani popote mlipo Swalah zenu ninafikishiwa.” [Imepokewa na Abu Daawud, Imam Ahmad na Atw-Twabarani]

 

Na akasema:

 

“Allaah Ana Malaika wanaotembea ardhini, wananifikishia salaam kutoka kwa ummah wangu.” [Imepokewa na An-Nasai, Ad-Daramiy na Ibni Habban]

 

Ziara Ya Msikiti:

 

Inapendeza mtu aoge na kuvaa nguo nadhifu, kisha aende Msikitini na kuingia kwa mguu wa kulia kwa utulivu na unyenyekevu na kusema pale anapoingia:

 

“A’udhu biLlaahi mina Shaytwaani rajiym, BismiLlaahir Rahmanir Rahiym Allaahumma Swaliy ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa sallim Allaahumma gh-firliy dhunuubiy wa ftah liy abwaaba rahmatik.”

 

Na maana yake ni:  Baada ya kusema A’udhu biLLaah na BismiLLaah, kisha unamswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ‘Aali zake na unamuomba Allaah maghfirah na Akufungulie milango yake ya Rahma.

 

Ni vizuri unapoingia Msikitini kwanza uelekee Ar-Rawdhah (sehemu iliyopo baina ya nyumba yake na mimbari yake ndani ya Msikiti), na kuswali hapo Tahiyyatul Masjid raka’ah mbili, ukishindwa kwa sababu ya zahma, basi swali sehemu yoyote ile ndani ya Msikiti, na ukishaswali elekea penye kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa utulivu na kwa moyo mkunjufu, na unapofika penye kaburi lake sema:

 

“Assalamu ‘Alayka ya RasuulaLLaah wa RahmatuLLaah wa Barakaatuh!

 

Na anaweza kuzidisha kwa kusema:

 

“Swalla Allaahu wa aalihi wa sallam ‘alayka wa ‘alaa asw-haabika, wa jazaaka Allaahu ‘an ummatika khayra, Allaahumma Aatihi al-wasiylata wal fadhwiylata wa b’ath-hul maqaamal mahmuudal lladhiy wa’adtah”

 

Na maana yake ni:

 

“Amani iwe juu yako ee Rasuli wa Allaah, na rahma za Allaah na barakah zake.”

“Rahma za Allaah na amani ziwe juu yako na juu ya Swahaba zako, na akulipe Allaah kheri wewe na ummah wako, Ee Allaah mpe wasiylah na fadhila na mnyanyue katika makazi matukufu ambayo umemuahidi”

 

Kisha unasogea mbele kidogo na unamsalimia Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), aliyezikwa umbali wa dhiraa moja na kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kisha hatua moja nyingine unamsalimia ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Kwa sababu Swahaba wawili hawa (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) wamezikwa karibu na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kisha unaelekea Qiblah na kujiombea mwenyewe Du’aa na kila unayempenda na unawaombea ndugu zako Waislamu, kisha unaondoka.

 

Si vizuri kunyanyua sauti na kuomba kwa sauti kubwa, unatakiwa uombe kwa sauti ndogo na kwa moyo mkunjufu, kiasi cha kuweza kujisikia mwenyewe tu. Iwapo utasoma juu ya ukuta wa nyumba yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambayo sasa ni kaburi lake, utaona kuwa imeandikwa Aayah isemayo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ

Enyi walioamini! Msipandishe sauti zenu juu ya sauti ya Nabiy.. [Al-Hujuraat: 2]

 

‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwahi kuwasikia watu wawili wakipaza sauti zao mahali hapo, akawaambia:

 

“Mungelikuwa nyinyi ni watu wa hapa hapa Madiynah, basi ningelikupigeni bakora.”

 

Haijuzu mtu kupangusa mikono yake kwenye kuta za kaburi kisha akajipangusia mwilini pake au kubusu yale mapambo ya kaburi, kama wanavyofanya baadhi ya watu kwa kutegemea eti wanapata baraka za mahali hapo.

 

Haya ni katika mambo aliyokataza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema:

 

“Musigeuze kaburi langu kuwa mahala pa Ibada, na mniswalie popote mlipo, kwa sababu Swalah zenu ninafikishiwa.”

 

Kumbuka - Tulivyoamrishwa ni kumswalia na kumsalimia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na sio kumuomba yeye akuondolee shida zako. Du’aa ni Ibada, na ibada zote zinaelekezwa kwa Allaah peke Yake.

 

Unapomaliza kulizuru kaburi, omba Du’aa ukiwa umeelekea Qiblah na umelipa mgongo kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) - Usielekee kaburini huku ukiomba Du’aa.

 

Makaburi Ya Baqiy’:

 

Hakuna ulazima ila akipenda mtu vizuri kwa wanaume tu, kuyazuru makaburi ya Baqiy’, mahala walipozikwa Swahaba wengi sana (Radhwiya Allaahu ‘anhum), pamoja na wake za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wajukuu zake (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na wengi katika waliofuata baada yao, kama vile Imaam Maalik na Naafiy’ na wengi wengineo (Allaah Awarehemu).

 

Kumbuka kuwa waliozikwa hapo wote ni ndugu zako Waislam, kwa ajili hiyo unatakiwa unapoyafikia makaburi hayo, ufanye kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani Nabiy wenu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mara anapoyafikia makaburi hayo akiwasalimia na kuwaombea Du’aa wote waliozikwa humo bila ya kubagua. Alikuwa akisema:

 

“Assalaamu ‘Alaykum ahl ddiyaari minal muuminin wal muslimiyn, wainnaa in shaa Allaahu bikum laahiquwn. Yarhamu Allaahul mustaqdimina minna wa min-kum wal-muta-akhiriyn. Nas-alu Allaaha lanaa walakum al ‘aafiyah. Allaahumma laa tuh-rimnaa ajrahum walaa tuftinnaa ba’adahum, waghfir lanaa walahum”

 

 Ziara Ya Msikiti Wa Qubaa:

 

Hakuna ulazima mtu anapokuwa Madiynah kwenda Msikiti wa Qubaa (Masjid Qubaa), lakini akiwa na nafasi baada ya 'ibaadah zake, akitaka anaweza kuzuru Msikiti wa mwanzo ulojengwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), ambao Allaah Amesema juu yake:

 

 ۚ لَّمَسْجِدٌ أُسِّسَ عَلَى التَّقْوَىٰ مِنْ أَوَّلِ يَوْمٍ أَحَقُّ أَن تَقُومَ فِيهِ ۚ فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُوا ۚ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ﴾

Msikiti ulioasisiwa juu ya taqwa tokea siku ya kwanza unastahiki zaidi usimame humo. Humo mna watu wanaopenda kujitwaharisha. Na Allaah Anapenda wanaojitwaharisha. [At-Tawbah: 108]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipenda kwenda hapo kila Jumamosi, akiwa amepanda mnyama, na kuswali raka’a mbili. Na alikuwa akisema:

 

“Mtu akijitwaharisha nyumbani kwake, kisha akaenda Msikiti Qubaa na akaswali hapo raka’a mbili, huandikiwa thawabu za aliyefanya ‘Umrah.” [Imepokewa na Imam Ahmad, An-Nasai, Ibni Maajah na Al-Haakim[

 

Mashahidi Wa Uhud:

 

Hakuna ulazima japo mtu anaweza kuzuru mashahidi wa Uhud na kuwaombea, na hapo lipo kaburi la ‘ammi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Hamzah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ‘Sayyidu Shuhadaa’, pamoja na Swahaba wengine (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliokufa mashahidi. ‘Ammi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliwa hapo alipopigwa mkuki katika vita vya Uhud na kuzikwa pale pale alipouliwa.

 

Kwa vile mahali hapo pana makaburi mengine, kwa hivyo ni vizuri mtu kuwatolea salaam waliozikwa hapo kwa kutamka yale yale uliyotamka pale ulipoyazuru makaburi ya Baqiy’.

 

Share