22-Swabrun Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat - 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'Anhaa)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)  

 

22- Subira Za Swahaabiyaat – Mama Wa Waumini  ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)

 

 

 

 

Kisa kinachojulikana kwa ‘Ifk’ (kashfa ya uzushi) kimekusanywa katika Al-Bukhaariy Amekielezea mwenyewe Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)

 

“Kila alipotaka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kwenda safari alikuwa akipiga kura ya wake zake. Kisha ambaye kura imemuangukia, huwa ndiye anayechukuliwa safarini pamoja naye.

 

Wakati mmoja alipotaka kwenda vitani, kura ikaniangukia mie kwa hiyo nikasafiri na Rasuli wa Allaah. Wakati huo Shariy’ah ya hijaab kwa wanawake ilikuwa imeshaamrishwa, kwa hiyo nikawa nabebwa katika msafara (juu ya ngamia) na nikiteremshwa nayo.

 

Tukaendelea na safari, na Rasuli wa Allaah alipomaliza vita vyake kisha akarudi, tukakaribia Madiynah. Rasuli wa Allaah akaamrisha kuendelea safari usiku. Jeshi lilipoamrishwa kuendelea safari ya nyumbani, niliinuka (kutaka kufanya haja msalani) nikatembea (kutafuta sehemu ya kufanyia haja) hadi nikaliacha (kambi la) jeshi nyuma. Nilipomaliza kujisaidia (msalani), nililiendea msafara wangu lakini kumbe! (mara nikakumbuka!) Kidani changu kilotengenezwa kutokana na aina ya shanga nyeusi kilivunjika. Nikakitafuta hadi kutafuta huko kukanizuia. Watu waliokuwa wakinibeba (katika msafara) wakafika ili kulibeba msafara juu ya ngamia wangu niliyekuwa nimempanda wakidhania kwamba nimo humo. Wakati huo wanawake walikuwa hafifu kwa uzani na hawakuwa wanene kwani walikuwa wakila (chakula) kidogo, kwa hiyo wale watu hawakuhisi kuwa msafara ni hafifu walipounyanyua. Nami nilikuwa bado mwanamke kijana.

 

Wakamwendesha ngamia, wakaendelea. Nami nikakiona kidani changu baada ya jeshi kuondoka. Nikaenda katika kambi yao lakini sikumwona mtu huko kwa hiyo nikaenda mahali nilipokuwa nimekaa (wakati tulipopumzika) nikidhania kwamba watanikosa na watarudi kunitafuta. Nilipokuwa nimekaa mahali pangu, nilisinzia nikalala. Swafwaan bin Al-Mu’attwil As-Sulamiyy Adh-Dhakwaaniy alikuwa nyuma ya jeshi. (alichelewa kuondoka) Akaanza (safari) nyakati ya mwisho ya usiku akafika kituoni pangu wakati wa asubuhi. Akaona umbo la mtu aliyelala. Akanijia na akanitambua baada ya kuniona kwani alikuwa akiniona kabla ya (Shariy’ah ya) ya hijaab. Nikainuka baada ya kauli yake aliyotamka aliponitambua: “Innaa liLLaahi wa innaa Ilayhi raaji’uwn.” Nikajifunika uso wangu kwa nguo yangu na Wa-Allaahi, hakuniambia hata neno moja isipokuwa istirjaa’ah (Innaa liLLaahi wa innaa Ilayhi raaji’uwn) mpaka alimpomwinamisha ngamia aliyekanyaga (chini) miguu yake ya mbele kisha nikampanda. Kisha Swafwaan akaendelea akimuongoza ngamia aliyekuwa amenibeba mimi hadi tukakutana na jeshi lilokuwa limepumzika wakati wa mchana wa joto. Akaangamia aliyekadiriwa kuangamia kiongozi wa ‘ifk’ ambaye ni ‘Abdullaahi bin Saluwl.  Baada ya hapo tukafika Madiynah nami nikawa naumwa mwezi mzima. (Kumbe) Huku watu wakitumbukia katika kusambaza kauli za wazushi wa kashfa nami sikuwa na habari nazo. Lakini kilichonitia shaka wakati naumwa ni kwamba sikuwa napokea tena kutoka kwa Rasuli wa Allaah huruma ile ile niliyokuwa nikiipata wakati nikiumwa (kabla ya uzushi huu wa ifk). Rasuli wa Allaah alikuwa akija kwangu na kuamkia kisha akiongeza kusema: ((Mnaonaje [vipi hali zenu]?)) kisha akiondoka. Hilo lilinitia shaka lakini sikujua kuhusu uovu uliokuwa ukienea mpaka nilipopata nafuu ya ugonjwa wangu.

 

Nikatoka nje pamoja na Ummu Mistwah kuelekea Al-Manaaswi’ mahali ambako tulikuwa tukienda kujisaidia haja. Na ilikuwa hatwendi huko kwa ajili hiyo ila usiku tu. Na hivyo ilikuwa ni kabla ya kuwa na vyoo karibu na nyumba zetu. Desturi hii ililingana na desturi ya Waarabu wa zamani (jangwani au katika mahema) kuhusu kujisaidia haja kubwa kwani tuliichukulia kuwa ni tatizo na madhara kuweko vyoo katika nyumba. Kwa hiyo nikaenda na Ummu Mistwah ambaye ni bint Ruhm bin ‘Abdil-Manaaf na mama yake ni bint wa Sakhr bin ‘Aamir ambaye ni shangazi yake Abuu Bakr As-Swiddiyq, na mwanawe ni Mistwah bin Uthaathah. Tulipomaliza haja zetu, wakati tunarudi nyumbani kwangu, Ummu Mistwah akajikwaa kwa nguo yake akasema: “Aangamizwe Mistwah!” Nikamwambia: “Maovu yaliyoje uliyoyasema! Unamtukana aliyeshiriki katika vita vya Badr?” Akasema: “Ee wee, hukusikia aliyoyasema?” Nikasema: “Amesema nini?” Hapo ndipo aliponitajia kauli za wazushi wa ifk ambazo zilizidisha maradhi yangu. Niliporudi nyumbani, Rasuli wa Allaah alinijia na baada ya kuniamkia akasema: ((Mnaonaje [vipi hali zenu?)) Nikasema: “Utaniruhusu niende kwa wazazi wangu?” Hapo nilitaka kuhakikisha kuhusu habari (hizo za ifk) kutoka kwao. Rasuli wa Allaah akaniruhusu nikaenda kwa wazazi wangu nikamuuliza mama yangu: “Ee mama! Watu wanaongelea kuhusu nini?” Mama yangu akasema: “Ee mwanangu! Chukulia mepesi, kwani hakuna mwanamke mcheshi anayependwa na mumewe ambaye ana wake wengineo pia ila hao wake watamtafutia kasoro!” Nikasema: “Subhaana Allaah! Hivyo kweli watu wamezungumza hayo?” Usiku ule nikawa nalia mno hadi asubui. Machozi yangu hayakusita, wala sikuweza kulala, na asubuhi kukapambazuka nikiwa bado nalia. Wahyi (kutoka kwa Allaah) ulichelewa na Rasuli wa Allaah alimwita ‘Aliy bin Abi Twaalib na Usaamah bin Zayd  (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa  ili kutaka ushauri kuhusu kumtaliki mkewe. Usaamah bin Zayd alimkumbusha Rasuli wa Allaah kuhusu kutokuwa na hatia mkewe na ambayo Nabiy mwenyewe anayayajua katika nafsi yake ya ahli yake kuhusu mapenzi. Akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Yeye ni mkeo, nasi hatujui lolote kuhusu yeye isipokuwa mazuri.”

 

Lakini ‘Aliy bin Abi Twaalib alisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Allaah Hakudhikishi jambo, na kuna wanawake tele kama yeye. Lakni ukimuuliza mjakazi wake atakwambia ukweli.”

 ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akaongezea kusema:

 

Basi Rasuli wa Allaah akamwita Bariyrah akamuuliza: ((Ee Bariyrah! Je, umeona lolote la kukutia shaka [kuhusu ‘Aaishah]?)) Bariyrah akasema: “Naapa kwa Allaah Aliyekutuma kwa haki! Sijapatapo kuona lolote la kumlaumu ‘Aaishah isipokuwa yeye ni msichana asiyepevuka bado ambaye akilala na kuacha unga uliokandwa kwa ajili ya familia yake, bila ya kuuhifadhi, ukaliwa na mbuzi.” 

 

Basi Rasuli wa Allaah akainuka (kuwaelekea) kuwauliza watu nani atakeyelipiza kisasi kwa ‘Abdullaahi bin ‘Ubay bin Saluwl. Rasuli wa Allaah alipokuwa juu ya mimbari akasema: ((Enyi hadhara ya Waislamu! Nani atakayenisaidia kunilipizia dhidi ya mtu aliyenifikishia maudhi ya [kukashifu) ahli yangu? Naapa kwa Allaah, sijui lolote ila mazuri kuhusu ahli yangu, na watu wamemtuhumu mtu (mwanamme) ambaye sijui lolote [baya] isipokuwa mazuri na hajapatapo kuzuru ahli yangu isipokuwa [kunizuru] mimi!))

 

Sa’d bin Mu’aadh al-Answaariy alisimama na kusema: “Ee Rasuli wa Allaah! Naapa nitakulipizia (nitakupumuzisha) naye! Ikiwa ni mtu kutoka kwa (Bani) Al-Aws, basi nitamkatilia mbali kichwa chake; na ikiwa ni kutokana na ndugu zetu Al-Khazraj, basi tupe amri yako nasi tutaitekeleza!”  

 

Hapo Sa’d bin ‘Ubaadah akasimama ambaye ni mkuu wa Khazraj. Na kabla ya tukio hili alikuwa ni mtu mwenye taqwa, lakini alipandwa hamasa (kwa ghera ya kabila lake).

 

Akamwambia Sa’ad (bin Mu’aadh), “Naapa Allaah Aliye hai! Umesema uongo! Hutamuua na wala hutaweza kumuua!”

 

Hapo ‘Usayd bin Hudhwayr, bin ammi wa Sa’d (bin Mu’aadh) alisimama akamwambia Sa’d bin ‘Ubaadah: “Wewe ndiye muongo! Naapa kwa Allaah Aliye hai! Hakika tutamuua, nawe ni mnafiki unayewatetea wanafiki!”

 

Basi makabila mawili ya Al-Aws na Al-Khazraj wakazozana mpaka wakahamasika kupigana huku Rasuli wa Allaah amesimama juu ya mimbari. Rasuli wa Allaah akaendelea kuwanyamazisha mpaka wakawa kimya, naye pia akawa kimya. Siku hiyo niliendelea kulia sana hadi kwamba machozi yangu hayakusita wala sikuweza kulala.

 

Asubuhi yake, wazazi wangu walikuwa pamoja nami na nikalia masiku mawili na mchana mmoja bila ya kulala, machozi ya mfululuzo hadi kulia huko kulikaribia kupasua maini yangu.

 

Walipokuwa nami na huku nikilia, akaja mwanamke wa Answaariy kutaka ruhusa kuniona. Nikamruhusu akaketi na akaanza kulia pamoja nami. Nilipokuwa katika hali ile, Rasuli wa Allaah akatujia na kutuamkia kisha akaketi chini. Hakupata kuketi pamoja nami tokea siku iliyosemwa yaliyosemwa. Alikaa mwezi bila ya kupokea Wahyi kuhusu kesi yangu. Rasuli wa Allaah akatamka shahaadah baada ya kuketi kisha akasema: ((Ee ‘Aaishah! Nimejulishwa kadha na kadhaa kuhusu wewe, na ikiwa wewe ni huna hatia, Allaah Atadhihirisha kutokuwa kwako na hatia. Na ikiwa umetenda dhambi, basi omba maghfirah ya Allaah na utubu Kwake, kwani mja anapokiri madhambi yake akatubia kwa Allaah, basi Allaah Hupokea toba yake)).

 

Rasuli wa Allaah alipomaliza, machozi yangu yalisita moja kwa moja hadi kwamba sikuhisi wala tone moja kutoka. Nikamwambia baba yangu: “Mjibu Rasuli wa Allaah anayoyasema kwa niaba yangu.” Akasema: “Naapa kwa Allaah, sijui la kusema kwa Rasuli wa Allaah!” Kisha nikamwambia mama yangu! “Mjibu Rasuli wa Allaah anayoyasema kwa niaba yangu.” Akasema: “Sijui la kusema kwa Rasuli wa Allaah!” Kwa vile nilikuwa bado mwenye umri mdogo na juu ya kuwa na elimu ndogo ya Qur-aan, nikasema:

 

“Naapa kwa Allaah! Najua mengi uliyoyasikia kuhusu kisa (cha ifk) hadi kwamba imestakiri katika akili zenu na mmeamini. Basi sasa nikikujulisheni kwamba mimi sina hatia, na Allaah Anajua kwamba mimi sina hatia, hamtoniamini. Na nikikiri jambo ambalo Allaah Anajua kwamba mimi sina hatia, mtaniamini. Naapa kwa Allaah! Siwezi kukupatieni mfano isipokuwa wa baba yake Yuwsuf: ((“Basi subira njema, na Allaah ni Mwenye kuombwa msaada juu ya mnayoyavumisha.”)) [Yuwsuf: 18]

 

 

Kisha nikageuka na kulala kitandani mwangu, na wakati huo nilijijua kuwa sina hatia na kwamba Allaah Atadhihirisha kutokuwa kwangu na hatia. Lakini naapa kwa Allaah! Sikufikiria kwamba Allaah Atateremsha Wahyi kwa ajili yangu utakaosomwa (milele), kwani nilijidhania sina thamani hivyo hata nitajwe na Allaah kwa Aayah za kusomwa. Lakini nilitarajia labda Rasuli wa Allaah ataoteshwa ndoto na Allaah kudhihirisha kutokuwa kwangu na hatia. Naapa kwa Allaah! Rasuli wa Allaah hakuwahi kuinuka alipoketi na hakuna aliyeondoka katika nyumba mara Wahyi (kutoka mbinguni) ukamfikia Rasuli wa Allaah. Ukamfikia katika hali ile ile ngumu ya kawaida inayomfikia (anapoletewa Wahyi kutoka mbinguni). Kwa hiyo majasho yakawa yanamwagika chini kama mfano wa lulu, juu ya kwamba ilikuwa siku ya msimu wa baridi, na hivyo ni kwa sababu ya uzito wa kauli (za Wahyi) zilofunuliwa kwake.

 

Baada ya hali hiyo nzito iliyompata Rasuli wa Allaah kumuondokea huku akitabasamu alipokuwa akifunuliwa Wahyi, neno la mwanzo alosema ni:

((‘Aaishah! Allaah Amedhihirisha usafi wako [kutokuwa kwako na hatia])).

 

Mama yangu akaniambia: “Inuka na mwendee.” Nikasema: “Naapa kwa Allaah! Sitomwendea na wala sitomshukuru yeyote isipokuwa Allaah!”

 

Hapo Allaah Akateremsha Wahyi:

 

إِنَّ الَّذِينَ جَاءُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ ۚ لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم ۖ بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۚ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ ۚ وَالَّذِي تَوَلَّىٰ كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١١﴾

Hakika wale walioleta singizo la kashfa; (kumzulia ‘Aaishah  رضي الله عنها) ni kundi miongoni mwenu. Msiichukulie kuwa ni shari kwenu, bali ni kheri kwenu.  Kila mtu katika wao atapata yale aliyochuma katika dhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kuu.

 

لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ ﴿١٢﴾

Kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa), Waumini wanaume na Waumini wanawake wasiwadhanie wenzao kheri, na wakasema: “Hii ni kashfa ya kusingizwa iliyo dhahiri?”

 

لَّوْلَا جَاءُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ ۚ فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاءِ فَأُولَـٰئِكَ عِندَ اللَّـهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٣﴾

Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Na kwa vile hawakuleta mashahidi, basi hao mbele ya Allaah ndio waongo.

 

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٤﴾

Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmah Yake duniani na Aakhirah, bila shaka ingekuguseni adhabu kuu kwa yale mliyojishughulisha nayo kuyaropoka,

 

إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾

Mlipoipokea (kashfa ya uzushi) kwa ndimi zenu, na mkasema kwa midomo yenu, yale ambayo hamkuwa na elimu nayo; na mnalidhania ni jambo jepesi; na hali hili mbele ya Allaah ni kubwa mno.

 

وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ ﴿١٦﴾

Na kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa) msiseme: “Haitupasi sisi tuzungumze haya; Subhaanak! Utakasifu ni Wako huu ni usingiziaji wa dhulma mkubwa mno!”

 

يَعِظُكُمُ اللَّـهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَدًا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧﴾

Allaah Anakuwaidhini msirudie abadani mfano wa haya, mkiwa ni Waumini wa kweli.

 

وَيُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿١٨﴾

 

Na Allaah Anakubainishieni Aayaat. Na Allaah Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.

 

إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾

Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini; watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui.

 

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّـهَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٠﴾

Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmah Yake, na kwamba Allaah ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu. [An-Nuwr: 11-20]

 

Aayah kumi zote. Alipoteremsha hizo Aayah Allaah, kuthibitisha usafi wangu, Abuu Bakr As-Swiddiyq ambaye alikuwa akimpa swadaqah Mistwah bin Uthaathah kwa vile ni jamaa yake wa uhusiano wa damu na kwa vile alikuwa ni maskini alisema: “Naapa kwa Allaah! Sitompa tena Mistwah chochote baada ya aliyoyasema kuhusu ‘Aaishah” Hapo Allaah Akateremsha Wahyi:

 

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾

Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.  [An-Nuwr: 22]

 

 

Abuu Bakr akasema: “Naapa kwa Allaah! Nataka Allaah Anighufurie.” Basi akarudia kumpa Mistwah swadaqah aliyokuwa akimpa kisha akasema: “Naapa kwa Allaah! Sitoacha kabisa kumpa!”

 

‘Aaishah akaendelea kusema: Rasuli wa Allaah alimuuliza Zaynab bin Jahsh pia kuhusu kesi yangu: ((Ee Zaynab! Unajua nini au umeonaje?))

 

Akajibu: “Ee Rasuli wa Allaah! Mimi nahifadhi masikio yangu na macho yangu (kujiepusha kusema uongo). Sijui lolote (baya kuhusu ‘Aaishah) isipokuwa mazuri.” Naye (Zaynab) ndiye miongoni mwa wake za Rasuli wa Allaah, aliyekuwa anayetamani kupokea kutoka kwake fadhila kama nilizokuwa nikizipokea (aliyekuwa na wivu nami).

 

 

Lakini Allaah Alimhifadhi (na uongo) kwa sababu ya huruma yake.

 

Lakini dada yake Hamnah (aliyekuwa akishiriki kwenye hizo tuhuma), aliendelea kugombana naye akaangamizwa kama kama wale waliotunga na kueneza kashfa.”  [Al-Bukhaariy]

Share