Kuweka Mikono Kifuani Au Kuachilia Baada Ya Kutoka Kwenye Rukuu

SWALI:

 

 

ssalamu alaykum.

 

Kwanza nawapongeza sana alhidaaya kwa juhudi yenu kubwa mnayo ifanya.Allah awalipe kheri nyinyi na sisi duniani na akhera Amin.

 

Najua mumesitisha kujibu maswali ila nahitaji kupata ufafanuzi juu ya KUWEKA MIKONO KIFUANI BAADA YA KUTOKA KWENYE RUKUU. Mimi binafsi nilipitia kitabu cha sheikh Nassordin Albany cha Swifat swalaat.... Nikaona katka sherhe yake kalipinga jambo hili kwavile halina dalili ya hadith. Nimesikia baadhi ya masheikh wakilitilia mkazo jambo la kuweka mikono kifuani kwani ndio sunnah. Wanasema kuwa sheikh Fauzan na Ibn Baaz (kama sijakosea). Wameliruhusu kuwa ni sunnah. Naomba ufafanuzi zaidi juu ya suala hili. Lipi liko sahihi zaidi kuweka mikono au kuacha?

 

Naomba jibu haraka kadri ambavyo Allah atakuwezesheni ili nitowe shaka juu ya jambo hili. Maassalam

 



 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Tunashukuru kwa swali lako zuri.

 

Kwa kifupi kuhusu mas-alah haya Wanachuoni wametofautiana juu yake.
 
Tunavyoona baada ya kupitia hoja za pande mbili, ni kuwa, mas-alah haya si mas-alah ya kusema anayefanya kadhaa ni uzushi bali kutokana na ufahamu wa Hadiyth ambayo kwayo Wanachuoni hao kama kina Shaykh Al-Albaaniy na Shaykh Ibn Baaz na wengine (Rahimahum Allaah) wametofautiana ufahamu wake, msimamo ulio mzuri ni ule uliopokea kutoka kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) kuwa mtu anapotoka katika kurukuu,
"Akipenda mtu, anaweza kuacha mikono yake pembeni, au akipenda anaweza kuweka kifuani mwake".
 
Kwa hiyo, tunaona mas-alah haya si ya wana-Sunnah au Waislamu kwa ujumla kuzozana kwayo au kuvutana. Anayerejesha mikono kifuani baada ya kutoka katika rukuu ana hoja zake na anayeachia ana hoja zake kutokana na ufahamu wa dalili na ijtihaad za Wanachuoni. Kadhaalika ni kama suala la kushuka wakati wa kusujudu; anayetanguliza magoti hakuna mvutano na anayetanguliza mikono, kwani kwa ufahamu wa Hadiyth ya ngamia ilivyokuja, Wanachuoni wamekhitalifiana vilevile kuhusu ufahamu sahihi wa makusudio ya Hadiyth.


Mtu anayekinaikiwa na hoja na ufahamu wa Wanachuoni wanaounga mkono mojawapo ya rai hizo, basi hakuna kulauminiana wala kuzozana.


 
Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share