Nguzo Za Swalaah Na Yaliyo Waajib Katika Swalaah

 

Nguzo Za Swalaah Na Yaliyo Waajib Katika Swalaah

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

Ni vitendo gani katika Swalaah ni Sunnah na vipi ni Fardhi? Nitashukuru mkinieleza kwa Salaa za rakaa mbili, tatu na nne.
 
Jazzakallahu Khayr

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa swali lako zuri. Nasi tutakuongezea jibu la nguzo ‘Rukn’ za Swalaah kwa faida yako na wengi wengine. Na tutajibu kuhusu Sunnah za Swalaah kwenye jibu jengine  kwa sababu ni mengi ambayo yamegawanywa katika Sunnah za maneno ‘As-Sunnan Al-Qawliyyah’ na Sunnah za vitendo ‘As-Sunnan Al-Fi’iliyyah’ hadi baadhi ya ‘Ulamaa  wanasema hizo Sunnah zinazidi 50. Hivyo pokea majibu kuhusu yaliyo Nguzo na Waajib katika Swalaah kwa leo.

 

Nguzo za Swalaah ni 14: Nguzo ni zile ambazo ukiswali na ukaziacha kwa makusudi Swalaah yako inabatilika, na ikiwa umeacha kwa kusahau, Swalaah yako pia itakuwa haikukamilika hadi urejee kitendo chenyewe au urejee rakaa na kisha mwishoni utoe Sajdatus-Sahw. Lakini ukiwa umesahau nguzo ya Takbiyratul-Ihraam, basi Swalaah yako basi itakubidi uiswali Swalaah upya tokea mwanzo.

 

Nguzo hizo 14 ni hizi zifuatazo:

 

 1. Kusimama katika Swalaah za fardh kwa yule mwenye uwezo.
 2. Takbiyratul-Ihraam.
 3. Kusoma Suwratul-Faatihah katika kila rakaa.
 4. Rukuu.
 5. Atw-Twumaaninah (utulivu) katika Rukuu
 6. I’itidaal (hapa inaingia na kunyanyuka kutoka katika Rukuu hadi anaponyooka mtu).
 7.  Atw-Twumaaninah (utulivu)  katika  I’Itidaal.
 8. Kusujudu.
 9. Atw-Twumaaninah (utulivu)  katika kusujudu.
 10. Kikao baina ya Sijda mbili.
 11. Atw-Twumaaninah (utulivu)  katika kikao baina ya Sijda mbili.
 12. Tashahhud ya mwisho.
 13. Kikao katika Tashahhud ya mwisho.
 14. Salaam (Kutoa Salaam).

 

Wametofautiana sana wanachuoni kuhusiana mambo yaliyo waajib.

 

Ama hapa tutaweka yale yaliyotajwa ambayo yanaelekea kuwa na nguvu zaidi.

Kwanza kabla hatujataja mambo yenyewe, tunapaswa kujua kuwa mambo ya Waajib ni yale ambayo vilevile atakapoacha mtu kwa makusudi hubatilika Swalaah yake, na atakapoacha kwa kusahau inamtosheleza yeye kusujudu Sijda mbili za kusahau ‘Sujuudus-Sahw’.

 

Na hayo mambo ya Waajib ni 8 kama yafuatayo:

 

 1. Takbiyrah nyingine zote isiyo ile ya Ihraam.
 2. Kusema “Sami’a-Allaahu liman hamidah” kwa Imaam na mwenye kuswali peke.
 3. Kusema “Rabbana Lakal Hamdu”.
 4. Kusema “Subhaana Rabbiyal-‘Adhwiym” mara moja kwenye kurukuu.
 5. Kusema “Subhaana Rabbiyal-A’alaa” kwenye kusujudu.
 6. Kusema “Rabbi-Ghfir-liy” kwenye kikao baina ta Sijda mbili.
 7. Tashahhud ya mwanzo.
 8. Kikao katika Tashahhud ya mwanzo.

Hizi ndizo maarufu zaidi kwa wanachuuoni.

 

Ama mambo ya Waajib ambayo yametajwa katika kitabu cha ‘Swahiyhu Fiqhis-Sunnah’ kwa dalili mbalimbali za Aayah na Hadiyth ni 9 kama yafuatayo:

 

 1. Du’aa ya ufunguzi wa Swalaah ‘Du’aa al-Istiftaah’.
 2. Kusema “A’uwdhu biLlaahi minash-dhaytwaanir-rajiym” kabla ya kusoma “BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym” na ‘Suwratul-Faatihah’.
 3. Kusema “Aamiyn” baada ya Suwratul-Faatihah.
 4. Takbiyrah za kuhama baina ya kitendo na kitendo.
 5. Kusema “Sami’a-Allaahu liman hamidah”
 6. Kusema “Rabbana Lakal Hamdu” katika I’itidaal.
 7. Kusema “Subhaana Rabbiyal-‘Adhwiym” wakati wa kurukuu na kusema “Subhaana Rabbiyal-A’ala” wakati wa kusujudu.
 8. Tashahhud ya kwanza.
 9. Kikao cha Tashahhud ya kwanza.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share