Swalah Ya Safari Ya Mtu Anayeishi Katika Nchi Muda Mrefu

SWALI:

Kwajina la mwenyezimungu mwingi wa rehema,

Naomba kuuliza: Jee ni vipi kuhusu swala ya safari? {a} Jee ni usafiri wa umbaligani ndio mtu unafaa kuwa uswali safari? {b}Jee na huko safarini ukishafika pia ni kipindigani ukiwa huko unaweza kuendelea kuswali safari? {c}Kwa sababu kuna baadhi ya watu ambao wanaishi nje ya nchi yao kwa kipindi kirefu yaani zaidi ya miaka miwili au mitatu nao bado huwa wanaendelea kuswali safari jee hili ni sawa?

Inshallah nategemea kujibiwa ili iwe faida kwangu na kwa wote

 


 

JIBU:

AlhamduliLLaah - Sifa njema zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwa vile Uislamu ndio njia pekee kamili na sahihi ya maisha, basi unawafikiria Waumini na hali zao katika mazingira tofauti. Na kwa vile safari zina mashaka, misukosuko na taabu, Uislamu unamsahilishia mambo msafiri upande wa Swalah na hata Funga. Hivyo ukiwa safarini swali Rakaa mbili badala ya Rakaa nne katika Swalah ya Adhuhuri, Alasiri na Ishaa. Ama Alfajiri na Magharibi hazipunguzwi. Allah Ametuambia:

Na mnapo safiri katika nchi si vibaya kwenu kama mkifupisha Swalah”

(4: 101).

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hii (kupunguza Swalah) ni neema ya Allaah kwenu, basi ipokeeni kwa shukrani” (Al-Bukhari).

Mtu akishatoka sehemu anayoishi kwa nia ya kuwa safarini (safari ianyokusudiwa hapa ni safari ya kheri inayoruhusiwa na Uislamu si safari ya maasiya na ufisadi) inakubidi ufupishe Swalah.

((Amehadithia ‘Abdillahi bin ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa alisafiri na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu), ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) na ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu 'anhu) na kamwe hakuwaona kabisa kuswali zaidi ya Rakaa mbili zile Swalah za Rakaa nne ndani ya safari)) (Al-Bukhariy na Muslim).

Hamna umbali maalumu uliowekwa na Qur-aan au Sunnah. Kuna kauli nyingi na rai tofauti kutoka kwa Maulamaa kuhusu masafa, wengine wamesema ni maili 48 au kilomita 85 kutokana kwamba Ibn 'Umar na Ibn 'Abbaas walikuwa wakifupisha katika masafa hayo, na wengine wameonelea mwendo wa siku tatu kutokana na Hadiyth ya kuwa 'asisafiri mwanamke masafa ya siku tatu bila kuwa na Mahram wake', na wengine kutokana na kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuswali Rakaa mbili baada tu ya maili tatu. Ama kauli yenye nguvu ni kuwa pale popote panapojulikana katika ada ya jamii ni safari basi hupunguzwa Swalah, japo ni chini ya masafa yaliyotajwa. Na hapa haiangaliwi jinsi ya kusafiri iwe kwa mguu, mnyama, gari, treni, meli au ndege, kinachoangaliwa ni tendo la safari.

Wanachuoni wana rai tofauti juu ya jambo hili, umbali unatofautiana kati ya maili 3 na 56 na sababu makhsusi ya tofauti hii ni kwamba hamna Hadithi yoyote ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayoweka umbali maalumu. Rai yetu ni kuwa hamna umbali maalumu ambao kwayo sharia inadhamiria kumruhusu msafiri kufupisha Swalah, bali uamuzi umeachiwa akili ya kawaida na busara ya mtu mwenyewe. Kila mtu anajua anapokuwa safarini hasa, na anapokuwa hayupo safarini.

Msafiri atafupisha Swalah kwa muda wote atakaokuwa safarini hadi atakaporejea kwao. Lakini kama ataamua kutua mahala kwa muda wa siku 4 au zaidi, bila kuhisabia siku ya kufika na kuondokea, hapo ataswali Swalah zote kwa ukamilifu. Hii ni rai ya wengi wakiwemo Imaam Shafi‘iy, Ahmad na Maalik.

Ama Imaam Abu Haniyfah, Ath-Thawriy na Al-Muzniy wanaonelea ni siku 15 kutokana na kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) vilevile.

Ama wengine rai yao ni kuwa kama mtu amesafiri kwenda pahali ambapo anatarajia kutekeleza au kupata jambo Fulani, basi ataendelea kufupisha Swalah katika kipindi chote cha kungojea kwake, hata kama itamchukua miaka, na wanajitegemeza kwa Hadithi zifuatazo:

1.     Amehadithia Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kuiteka Makkah alikaa hapo siku 18 naye alikuwa anafupisha Swalah (Ahmad).

2.    Amesema Ibn Qayyim kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa Taabuuk siku 20 naye alikuwa akifupisha Swalah (Ahmad).

3.    Amehadithia Hasan bin ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu 'anhuma) kuwa: “Tulikaa pamoja na ‘Abdur-Rahmaan bin Samurah (Radhiya Allaahu 'anhu) Kabul, Afghanistan miaka miwili nasi tulikuwa tunafupisha Swalah”.

Tumetoa dalili chache tu hapo juu kwa sababu huu ni mlango mpana sana na una dalili nyingi hatuwezi kuziorodhesha zote hapa kwenye jibu.

Hivyo kwa muhtasari ya yote ni kuwa katika safari hakuna umbali maalumu bali kila mmoja wetu anajua safari ni nini na mara kadhaa Mtume wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatoka nje ya Madinah kidogo na akawa anaswali Swalah ya safari. Ama kuhusu muda ni kuwa ukiweka nia ya kukaa sehemu kwa muda wa chini ya siku kumi 18, 19, au 20 kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) unaweza kuswali Swalah ya safari ama ikiwa una nia ya kukaa zaidi ya siku hizo basi unakuwa ni Muqiym (mkazi wa huo mji). Ama ikiwa umekwenda safari na ukatarajia ya kwamba utafanya kazi yako na utamaliza kwa muda mfupi lakini ukachelewa kumaliza au ukachelewshwa lakini una tamaa ya kuwa utamaliza kesho au kesho kutwa utakuwa ni mwenye kuruhusiwa kuswali Swalah ya safari mpaka umalize kazi yako. Hiyo ni kuwa kwa hakika huna umakini wala utulivu na ndivyo Maswahaba walivyofanya kama tulivyonukuu hapo juu.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share