Kuswali Swalah Ya Safari Kwa Sababu Ya Umbali Wa Anapofanyia Kazi

SWALI:

 

Asalam Aleykum;


Sheikh, mimi nafanya kazi katika company iliyokuwa umbali wa kilo 38 kutoka nyumbani. mara nyingi huswali sala ya safar kwa sababu time narejea nyumbani Alaasir imekwisha adhiniwa. kuna siku nilitingwa sana na kazi na sikupata wasaa wa kusali kazini na niliporejea nyumbani nikajiaandaa kukidhi salaa, alikuwepo kijana alietoka chuoni akanambia kuwa inawezekana nikasali kama sala ya safari lakini ninuie kuwa nasali jamaan wa kasrani (yaani nijumuishe adhuhuri na asir kwa kufupisha) kila ninaemuuliza jambo hili anakuwa hana maalumat yoyote. Naomba kujua swala hii inaswihi??


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza tungependa kuziusia na kuziwaidhi nafsi zetu na yako kwamba Swalah tano tunatakiwa na tunatarajiwa tuwe tunaziswali msikitini tena jama’ah kama ni wanaume; huo ndio mwendo wa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndio mafundisho yake. Ila kwa dharura tu ndipo inapokubalika kuswali nyumbani au safari.

 

 

Tunashukuru kuona kwamba umejitahidi kuuuliza huku na kule ila umeshindwa kupata mashekhe wanaohusika kukupa jibu ipasavyo. Mara nyingine jitahidi kutafuta jibu la swali lako kutoka kwa Mashekhe wanaostahiki kutoa majibu ili uweze kupata jibu na uweze kutimiza ibada yako ipasavyo. 

 

Kama ulivyothibitisha kwa kusema kuwa: mara nyingi unaswali Swalah ya safari na kijana wa chuoni alikushauri kuongeza kuchanganya pahala ambapo huna uhakika napo.

 

Asli katika kupunguza Swalah ni kauli yake Allaah Aliposema:

“Na mnaposafiri katika nchi si vibaya kwenu kama mkifupisha Swalah, iwapo mnachelea wasije wale waliokufuru wakakuleteeni maudhi. Hakika makafiri ni maadui zenu walio wazi wazi.” An-Nisaa: 101.

 

Na Hadiyth ya Mama wa Wamini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliposema:

“Allaah Amefaradhisha Swalah Alipofaradhisha rakaa mbili mbili; rakaa mbili katika hadhar-nyumbani- na mbili katika safari.  Swalah ya safari ikabaki vile vile na ikaongezwa Swalah ya hadhar” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swalah ya Wasafiri na namna ya kuipunguza, mlango wa Swalah ya Wasafiri na namna ya kuipunguza.

 

Swali linalojitokeza ni; umbali gani unaruhusiwa kupunguza Swalah?

 

Aayah kama ilivyo wazi haikuweka kiwango cha umbali anaotakiwa mja kupunguza Swalah bali ilibainisha ruhusa –uhalali- wa kupunguza

“…mnaposafiri katika nchi si vibaya kwenu kama mkifupisha Swalah…”

 

Hivyo basi Qur-aan na Hadiyth za Mtume Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) havikuweka kiwango cha umbali wa kupunguza Swalah; kwani yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyopokelewa hakupata kusafiri safari yoyote ile isipokuwa alikuwa aliswali safar –alipunguza Swalah- na pia Swahaba zake, kama inavyothibitisha Hadiyth ya Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kusema:

“Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapotoka mwendo wa meli tatu (3) au faraasikh* tatu (3) hupunguza Swalah na huswali rakaa mbili” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swalah ya Wasafiri na namna ya kuipunguza, mlango wa Swalah ya Wasafiri na namna ya kuipunguza.

 

*Farsakh = mita 5541

 

Hata hivyo Maulamaa wameweka kiwango cha kuruhusiwa kupunguza Swalah na katika hilo lililo sahihi ni ile kauli iliyosema kuwa kila chenye kueleweka kama ni safari katika desturi ya watu basi inaruhusiwa kupunguza Swalah hata kama haijatimia kilomita 80, na kila wanachosema watu kuwa sio safari, basi sio safari hata kama kitafikilia kilomita mia (100).

 

Na kuhusiana na sharti -sababu- ya kuruhusiwa kupunguza Swalah iliyotaja katika aya ambayo ni kuwepo khofu

“… iwapo mnachelea wasije wale waliokufuru wakakuleteeni maudhi...”

 

Sharti hili limeondoshwa (hivyo imebakia kuwa kila safari katika ardhi mtu anaruhusiwa kupunguza Swalah) kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn Umayyah amesema: Nilimwambia ‘Umar bnul Khatwtwaab: Nipe habari kuna sababu gani ya watu kupunguza Swalah; kwani Allaah Amesema: “. iwapo mnachelea wasije wale waliokufuru wakakuleteeni maudhi...” na jambo hilo leo halipo? ‘Umar akasema: Mimi pia nashangazwa na kinachokushangaza, basi nikamuelezea Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hayo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ni Sadaqah Aliyokuleteeni Allaah, basi ipokeeni Sadaqah Yake” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swalah ya Wasafiri na namna ya kuipunguza, mlango wa Swalah ya Wasafiri na namna ya kuipunguza.

 

 

Je, inajuzu kuchanganya –kukusanya Swalah- bila ya kupunguza? Au je, inaruhusiwa kukusanya inaporuhusiwa kupunguza?

 

Na asli katika kukusanya Swalah kwa mkaazi ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema:

“Aliwahi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukusanya Dhuhri na ‘Asr pamoja na Maghrib na ‘Ishaa pamoja akiwa Madiynah -mkaazi- pasina kuwepo kwa khofu wala mvua” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swalah ya Wasafiri na namna ya kuipunguza, mlango wa kuchanganya Swalah katika hadhar.

 

Maulamaa wanasema kwa kusisitiza kuwa sababu iliyopelekea kuruhusiwa kukusanya ni haraj –taabu na matatizo- katika kutekeleza kila Swalah katika wakati wake, hivyo basi inaruhusiwa kwa mgonjwa kukusanya kati ya Swalah ya Dhuhur na ‘Asr au Maghrib na ‘Ishaa kama ataona taabu au mashaka kuswali kila Swalah kwa wakati wake; basi pale panapotokea mashaka au taabu -haraj- kwa Muislamu aliyepo mjini kwake –kama wewe muulizaji wetu kama ni haraj kuiswali kila Swalah kwa wakati wake – basi itajuzu kwako kukusanya Swalah au inasuniwa kwako hivyo, vyenginevyo kama huna matatizo wala haraj (kwani waweza kuiswali Swalah kazini kabla hujaondoka au hata njiani unaporudi, simamisha gari lako barabarani pembeni na uswali) ni wajibu wako kuswali kila Swalah katika wakati wake.

 

Hivyo basi ni vyema ieleweke kuwa kukusanya Swalah hakufungamani na kupunguzwa kwake, bali kunafungamana na haja; hivyo basi wakati wowote ule mtu akihitaji kuchanganya Swalah awe mkaazi -katika hadhar- au msafiri huruhusiwa kuchanganya, kama wanavyoruhusiwa wakazi wa mji kukusanya kati ya Swalah ya Maghrib na ‘Ishaa msikitini usiku wa mvua kubwa, au baridi kali, au upepo mkali; kama wataona ni vigumu na ni mashaka kurudi msikitini kwa Swalah ya ‘Ishaa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

  

 

 

Share