Watoto Wa Nje Ya Ndoa Nini Hukmu Yake?

 

SWALI:

NINA SWALI MAWILI ,

1.ISLAM INASEMA NINI KWA WATOTO WA KUZALIWA INJE YA NDOWA? NASEMA KWA UZINIFU (OUTSIDE OF MARIAGE BEFORE AND AFTER)

 


 

 

 

JIBU

 

 

 

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Ahli zake, Sahaba zake (Radhiya Allaahu ‘Anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Katika Uislamu kitendo hicho cha zinaa ambacho kimefanywa na mwanaume na mwanamke ndio makosa na waliofanya wanafaa waadhibiwe hapa duniani ili wasafishwe kwa kosa lao hilo hadharani. Na Allah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Ametuagizia Tusikaribie kabisa zinaa (17: 32). Lakini tufahamu ya kwamba yule mtoto anayezaliwa hana hatia yoyote. Allah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema:

“Na kila nafsi haichumii ila nafsi yake. Na habebi mwenye kubeba mzigo wa mwenziwe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu  Naye Atakuambieni mliyo kuwa mkitofautiana” (6: 164).

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) amesema: ((Kila kinachozaliwa kinazaliwa katika Uislamu .....)) l-Bukhaariy).

Na haifai kwa Muislamu kumuita mtoto aliyezaliwa kwa jina la mwana-haramu kwa sababu mtoto mwenyewe si wa haramu bali kitendo chenyewe ndicho haramu. Na ieleweke kuwa mtoto huyu hataitwa kwa jina la huyu mwanaume aliyezini na mamake kwa sababu kisheria si mtoto wake wala hawa wawili hawarithiani kabisa. Mtoto huyu hatamrithi huyo mwanaume na huyo baba hatamrithi mtoto huyo. Lakini mtoto anaweza kumrithi mama yake na mama kumrithi mtoto wake.

 

Tanbihi kwa kila mmoja wetu ajichunge sana ili asiingie katika madhambi haya ya zinaa. Na ndio sheria ikafanya ndoa kuwa rahisi na ikaweka adhabu kali kwa wenye kuzini.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

Share