006-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kutawakali Kwa Allaah Na Kuwa Na Moyo Laini

 

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 6

Kutawakali Kwa Allah Na Kuwa Na Moyo Laini

www.alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ: ((يَدْخُلُ الْجَنَّةَ أَقْوَامٌ أَفْئِدَتُهُمْ مِثْلُ أَفْئِدَةِ الطَّيْرِ)) رواه مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Wataingia Jannah watu ambao nyoyo zao ni mithali ya nyoyo za ndege)). [Muslim.] Kwa maana: Wenye kutawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na nyoyo zao zikiwa laini.

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Waumini ni wenye nyoyo laini, kinyume na makafiri na wanafiki. Rejea: Al-Maaidah (5: 13).

 

 

2. Umuhimu wa kutawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na kuwa na moyo mlaini (wenye yaqini), ni sababu ya kumuingiza Muislamu Jannah.

 

 

2. Muumin anapaswa asishughulishwe hadi kujiangamiza au kuingia katika chumo la haramu katika kutafuta maisha na rizki yake, kwani rizki inakutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Anayemruzuku ndege anayekutoka asubuhi bila ya kujua rizki yake, akarudi jioni akiwa amepata mahitajio yake.  

 

Rejea: Huwd (11: 6), Al-An’aam (6: 38).

 

Na kughushi ni miongoni mwa chumo la haramu. Rejea Hadiyth namba (101) kuhusu kughushi.

 

 

4. Kutawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى), kuwa na yakini na moyo laini ni miongoni mwa sifa kuu za Muumin. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٢﴾

Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia iymaan, na kwa Rabb wao wanatawakali.

الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣﴾

Ambao wanasimamisha Swalaah na katika yale Tuliyowaruzuku hutoa.

 

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴿٤﴾

Hao ndio Waumini wa kweli!  Wana daraja (za Jannah) kwa Rabb wao na maghfirah na riziki karimu.  [Al-Anfaal 8: 2-4]

 

Na Anasema pia Allaah (عزّ وجلّ):

 

فَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٣٦﴾

Basi chochote mlichopewa katika kitu ni starehe ndogo za uhai wa dunia.  Na yale yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi na ni ya kudumu kwa wale walioamini na kwa Rabb wao wanatawakali.  [Ash-Shuwraa: 36]

 

Na rejea: Al-Ahzaab (33: 22), Aal-‘Imraan (3: 173-174).

 

5. Muumini anapaswa kutawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى) katika mambo yake yote kwani Allaah (سبحانه وتعالى) Anatosheleza kuwa mwenye kutegemewa kama Anavyosema:

 

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ  

((Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza)) [Atw-Twalaaq (65: 3)]

 

6-Muumini anapofikwa na hali ya khofu au hatari, atawakali kwa Allaah (عزّ وجلّ) ili apate kulindwa na madhara na shari zote anazozikhofia. Hivi ndivyo kama alivyofanya Nabiy Ibraahiym (عليه السلام)  na Maswahaba  (رضي الله عنهم)  kama ilivyotajwa katika Hadiyth:

 

عن ابن عباس رضي الله عنهما أيضًا، قَالَ: حَسْبُنَا اللهُ وَنِعْمَ الوَكِيلُ، قَالَهَا إِبرَاهيمُ عليه السلام حِينَ أُلقِيَ في النَّارِ، وَقَالَها مُحَمَّدٌ صلى الله عليه وسلم حِينَ قَالُوا: إنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إيْمانًا وَقَالُوا: حَسْبُنَا الله ونعْمَ الوَكيلُ. رواه البخاري.

وفي رواية لَهُ عن ابن عَبَّاسٍ رضي الله عنهما، قَالَ: كَانَ آخر قَول إبْرَاهِيمَ صلى الله عليه وسلم حِينَ أُلْقِيَ في النَّارِ: حَسْبِي الله ونِعْمَ الوَكِيلُ

‘Abdullaah bin ‘Abbaas (رضي الله عنه)  amesema:

حَسْبُنَا اللهُ وَنِعْمَ الوَكِيلُ

“Allaah Anatutosheleza na Mzuri Alioje Mdhamini Anayetegemewa kwa yote.”

Amesema hivi Nabiy Ibraahiym (عليه السلام)    alipotumbukizwa motoni, na alisema Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  pale watu (walipokodiwa na Maquraysh) walipowaambia (Waislaam): “Watu wamewakusanyikia, kwa hiyo waogopeni.” Lakini maneno hayo yaliwazidishia Iymaan (Waislamu) wakasema:

حَسْبُنَا اللهُ وَنِعْمَ الوَكِيلُ

“Allaah Anatutosheleza na Mzuri Alioje Mdhamini Anayetegemewa kwa yote.”  [Al-Bukhaariy]

Riwaayah nyingine; kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Abbaas  (رضي الله عنهما)  amesema: Kauli ya mwisho aliyotamka Nabiy Ibraahiym (عليه السلام)    wakati alipotumbukizwa kwenye moto ilikuwa ni kusema:

حَسْبِي الله ونِعْمَ الوَكِيلُ

“Allaah Ananitosheleza na Mzuri Alioje Mdhamini Anayetegemewa kwa yote.”

 

 

7. Kuomba du’aa ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu kutawakali:

 

عن ابن عباس رضي الله عنهما أيضًا: أنَّ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم كَانَ يقول: ((اللَّهُمَّ لَكَ أَسْلَمْتُ، وَبِكَ آمَنْتُ، وَعَليْك تَوَكَّلْتُ، وَإِلَيْكَ أنَبْتُ، وَبِكَ خَاصَمْتُ. اللَّهُمَّ إِنِّي أعُوذُ بعزَّتِكَ؛ لا إلهَ إلا أَنْتَ أنْ تُضلَّني، أَنْتَ الحَيُّ الَّذِي لا يَمُوتُ، وَالجِنُّ والإنْسُ يَمُوتُونَ)). مُتَّفَقٌ عَلَيهِ، وهذا لفظ مسلم واختصره البخاري

Abdullaah bin ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  amesimulia: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)   alikuwa akiomba: “Ee Allaah, kwa ajili Yako nimejisalimisha, Kwako tu nimeamini, na Kwako Pekee  natawakali, na Kwako tu nimerejea, kwa ajili Yako tu nakhasimiana. Ee Allaah, hakika mimi najilinda kwa utukufu Wako, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Usinipoteze. Wewe ni Hai Usiekufa, majini na wana-Aadam watakufa.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 
 

Share