011-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Daraja Za Iymaan Ni Sabini Na; Ya Juu Ni Tawhiyd Ya Chini Kuondosha Taka..

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 11

Daraja Za Iymaan Ni Sabini Na Kitu; Ya Juu Ni Tawhiyd,

Ya Chini Ni Kuondosha Taka Njiani

www.alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ  (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم):  ((الإيمَانُ بِضْعٌ وَسَبْعُونَ)) أَوْ ((بِضْعٌ وَسِتُّونَ شُعْبَةً، فَأَفْضَلُهَا قَوْلُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ،  وَأَدْنَاهَا إِمَاطَةُ الأَذَى عَنْ الطَّرِيقِ، وَالْحَيَاءُ شُعْبَةٌ مِنْ الإِيمَانِ)) متفق عليه.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Iymaan ni sabiini na kitu)) au alisema ((Tanzu sitiini na kitu. Ilio bora kabisa ni kauli ya ‘Laa ilaaha illa-Allaah’, na ya chini kabisa ni kuondosha taka njiani. Na kuona hayaa ni utanzu katika tanzu za Iymaan)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Faida:  Bidhw’ ni idadi baina ya tatu na tisa.

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Waumini wanatofautiana katika daraja za Iymaan zao.

 

 

2. Umuhimu na fadhila ya tawhiyd yaani kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) ambayo ni asili ya Iymaan.

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

هُوَ الْحَيُّ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ ۗ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴿٦٥﴾

Yeye Ndiye Aliye hai daima hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye; basi muombeni Yeye wenye kumtakasia Dini. AlhamduliLLaah, Himidi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu. [Ghaafir (40: 65)]

 

 

Rejea pia: Al-An’aam (6: 102), Al-Baqarah (2: 163), Twaahaa (20: 14).

 

Na pia Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

وَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۘ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

Na wala usiombe pamoja na Allaah mwabudiwa mwingine. Hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye. Kila kitu ni chenye kuhiliki isipokuwa Wajihi Wake. Hukumu ni Yake Pekee na Kwake Pekee mtarejeshwa. [Al-Qaswasw (28: 88]

 

 

3. Iymaan na ‘amali vinakwenda sambamba, ni vitu viwili ambavyo haviwezi kutengana.

 

 

4. Kuona hayaa ni katika sifa za Waumini. Hayaa inahusiana na tabia njema kwa sababu inamzuia mtu kutenda maasi yote na inamweka kwenye hali ya utiifu wakati wote.

 

Rejea Hadiyth namba (68).

 

 

5. Kuwa na hayaa ni dalili ya ukweli wa Iymaan ya Muislamu.

 

 

6. Muumin asidharau kutenda jambo jema lolote hata dogo mno vipi kama kuondosha taka njiani kwani huenda hayo yakawa mazito katika miyzaan yake ya mambo mema Siku ya Qiyaamah.  

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا تُقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُم مِّنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِندَ اللَّـهِ هُوَ خَيْرًا وَأَعْظَمَ أَجْرًا ۚ  

Na chochote kile cha kheri mnachokadimisha kwa ajili ya nafsi zenu, mtakikuta kwa Allaah. Ni bora, na ujira mkubwa zaidi.  [Al-Muzzammil (73: 23)]

 

Na rejea pia:  Al-Baqarah (2: 110)

 

Na pia Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ﴿٧﴾

Basi yule atakayetenda kheri uzito wa chembe (au sisimizi) ataiona. [Az-Zalzalah (99: 7)]

 

 

Rejea:  Al-Anbiyaa (21: 47).

  

Pia Hadiyth:

 

 عَنْ أَبِي ذَرٍّ، قَالَ: قَالَ لِيَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لَا تَحْقِرَنَّ مِنَ الْمَعْرُوفِ شَيْئًا، وَلَوْ أَنْ تَلْقَى أَخَاكَ بِوَجْهٍ طَلْقٍ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Dharr  (رضي الله عنه) amesema: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Usidharau kufanya jambo jema lolote lile hata ikiwa kukutana na nduguyo kwa uso wa bashasha)) [Muslim]

 

 

7. Kukosekana haya ni kukosekana Iymaan, hivyo kunamfanya mja afanye lolote atakalo. Imepokewa kwa Abuu Mas-’uwd ‘Uqbah bin ‘Amr Al-Answaar Al-Badriy (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika katika maneno yaliyopatikana na watu kutokana na Manabii ni: Usipokuwa na hayaa, basi fanya utakalo)).[Al-Bukhaariy]

 

 

Share